1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON: Condoleezza Rice na Robert Gates wazuru Mashariki ya Kati

30 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBdo

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, na waziri wa ulinzi, Robert Gates, wameondoka leo mjini Washington kwenda Mashariki ya Kati.

Lengo la ziara yao ni kutafuta kuungwa mkono na nchi za kiarabu kuhusu Irak na kujadili uuzaji wa silaha kwa washirika wa Marekani katika eneo hilo.

Condoleezza Rice na Robert Gates watakutana na mawaziri wa baraza la ushirikiano wa nchi za Ghuba katika eneo la mapumziko la Sharm el Sheikh nchini Misri.

Viongozi hao watakutana na wajumbe kutoka Bahrain, Kuwaiti, Oman, Qatar, Saudi Arabia, jumiuya ya falme za kiarabu, Misri na Jordan. Waziri Rice na Gates wanatarajiwa pia kuwahakikishia viongozi wa nchi hizo kwamba Marekani imejitolea kikamilifu kuhakikisha usalama wa eneo hilo huku kukiwa na vitisho kutoka kwa Iran na mpango wake wa nyuklia.

Kwenye mkutano huo Marekani inatarajiwa kusisitiza wasiwasi wake juu ya baadhi ya nchi za Waarabu wa madhehebu ya Sunni kuwasaidia kifedha wapiganaji wa kigeni na kuchochea upinzani dhidi ya serikali ya Washia nchini Irak inayoungwa mkono na Marekani.

Condoleeza Rice na Robert Gates watazuru pia Saudi Arabia.