1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasemavyo wahari wa Ujerumani Jumatano

Admin.WagnerD20 Aprili 2016

Wahariri wa Ujerumani Jumatano wameangazia mkutano kati ya kiongozi wa Hungary Viktor Orban na Kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl, kukamatwa kwa washukiwa wa mashambulizi dhidi ya wakimbizi miongoni mwa mengine.

https://p.dw.com/p/1IYvi
Waziri Mkuu wa Hungary Viktor akiwa na mwenyeji wake Kansela Helmut Kohl nyumbani kwake.
Waziri Mkuu wa Hungary Viktor akiwa na mwenyeji wake Kansela Helmut Kohl nyumbani kwake.Picha: picture-alliance/dpa/D. Biskup

Mhariri wa gazeti la Ludwigsburger Kreiszeitung ameandika juu ya kukamatwa kwa washukiwa wa mashambulizi dhidi ya makazi ya wakimbizi mjini Freital katika jimbo la Saxony hapa Ujerumani. Mhariri huyo anasema mji huo umegeuka kituo cha manazi mamboleo na chuki dhidi ya wageni. Matukio ya uhalifu wa vurugu za mwelekeo wa chuki za siasa kali za mrengo wa kulia yameongezeka mara tatu zaidi katika mji huo. Lakini kukamatwa kwa washukiwa hao kunaonyesha kuwa serikali iko makini na inafuatilia mienendo ya watu hao.

Naye Mhariri wa gazeti la Allgemeine anasema itahitaji uchambuzi wa kina kubaini iwapo tukio la Freital lilikuwa la kipekee au ni mwamko wa kweli kuhusiana na tatizo halisi linalotukabili. Mhariri wa gazeti la Stuttgarter Zeitung amezungumzia ziara ya waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban nyumbani kwa Kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl. Mhariri huyu amesema:

Licha ya Kansela Merkel kuutaja mkutano kati ya Orban na Kohl kuwa wa maana na wenye tija, maneno matamu yaliyotolewa na wawili hao hayawezi kuficha utata uliopo kati yao na serikali mjini Berlin. Viktor Orban ndiye mkosoaji mkubwa zaidi wa sera ya wakimbizi ya Merkel miongoni mwa viongozi wakuu wa mataifa ya Umoja wa Ulaya. Lakini anapeana mikono na vigogo wa kihafidhina nchini Ujerumani, anakaribishwa na Seehorfer na Kohl. Kwa silika yake mahusiano ya kimadaraka, Helmut Kohl anafahamu fika kwamba Merkel amekuwa hatarini. Kwa kumualika Orban Kohl ametimiza lengo lake.

Manazi Mamboleo wakiandamana kupinga wakimbizi mjini Freital, jimboni Saxony.
Manazi Mamboleo wakiandamana kupinga wakimbizi mjini Freital, jimboni Saxony.Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Meyer

Mhariri wa gazeti la Die Welt ameandika juu ya kitisho cha kundi la Dola la Kiislamu IS kushambulia maeneo ya kitalii nchini Uhispania, Ufaransa na Italia. Mhariri huyo anasema

Ni kawaida kwa ripoti kama hizo kwamba uhalisia wa maudhui yake unathibitishwa tu baada ya mashambulizi kutokea. Lakini hatari hiyo ni ya kweli. Mashambulizi dhidi ya maeneo maarufu ya mapumziko ambayo ulinzi wake mara nyingi siyo imara, ni sehemu muhimu ya mkakati wa kundi la IS. Mashambulizi kama haya yana malengo mawili yanayokwenda sawia: kuzivuruga jamii ambazo tayari zimeparaganyika, na kuzidisha khofu. Ikiwa khofu na vitisho vitatawala mipango yetu ya mapumziko, basi magaidi wameshinda.

Mhariri wa gazeti la Stuttgarter Nachrichten anatilia maanani juhudi za umoja wa Ulaya kupambana na wasafirishaji watu kimagendo nchini Libya. Mhariri huyo anasema:

Baada ya kufungwa kwa njia ya Balkan, majanga ya Bahari ya Mediterrania yameanza kurundikana tena. Ishara za mwanzo za kutisha tayari zimeonekana, na Umoja wa Ulaya umeitikia. Unataka kupanua operesheni yake dhidi ya wasafirishaji watu kimagendo hadi kwenye pwani ya Libya kwa ridhaa ya serikali ya umoja wa kitaifa. Lakini maamuzi ya hilo yako mikononi mwa wanasiasa, ambao nao wanategemea nguvu nyingi zisizo dhahiri, lakini Umoja wa Ulaya hauna budi kushughulikia tatizo la uhamiaji kwenye chanzo chake. Hakuna mahala popopte duniani hilo linapodhihirika wazi kama nchini Libya.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Grace Patricia Kabogo