1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapenda mageuzi nchini Syria wajiandaa kwa maandamano

12 Agosti 2011

Raia 2 wameuliwa leo na vikosi vya usalama vya Syria, mmoja karibu na mji mkuu Damascus na wa pili , kaskazini magharibi ya Syria.Habari hizo zimetangazwa na shirika la haki za binaadam la Syria.

https://p.dw.com/p/12FVx
Vifaru vya jeshi la Syria katika mji wa Deir al ZorPicha: dapd

Mkurugenzi wa shirika la haki za binaadam la Syria,Rami Abdel Rahmane amesema mhanga wa kwanza ambaye ni mwanamume ameuliwa alipokuwa akikimbia kamata kamata ya vikosi vya usalama katika kitongoji cha Damascus, Sagba. "Mwili wake unaonyesha amepigwa tako la bunduki."

Mjini Sheikhoun, katika mkoa wa Idleb unaopakana na Uturuki, bibi mmoja ameuliwa pia wakati wa opereshini za vikosi vya usalama. Ameongeza kusema mkurugenzi wa shirika la haki za binaadam la Syria.

"Darzeni kadhaa za vifaru, magari ya kusafirishia wanajeshi na hata mabasi ya kiraia yaliyosheheni askari kanzu yameuvamia mji wa Sheikhoun alfajiri ya leo. Milio ya nguvu ya mizinga imekua ikisikika, anasema mwanaharakati mmoja.

Operesheni za kijeshi zilizofanywa jana na vikosi vya serikali dhidi ya wapenda mageuzi zimegharimu maisha ya watu wasiopungua 16 nchini Syria.

Demonstration in Syrien Latakia
Maandamano ya wapenda mageuziPicha: picture-alliance/dpa

Lakini wapenda mageuzi hawatishiki - mbali na maandamano ya kila siku mnamo wakati huu wa Ramadhan, na hii leo wametoa mwito kupitia facebook, wa kufanyika maandamano makubwa kabisa baada ya sala ya Ijumaa kauli mbiu ikiwa "Hatuna tunayemtii isipokuwa Mungu."

Jana jioni maafisa wa usalama wamemkamata mwenyekiti wa shirika la haki za binaadam la Syria Abdel Karim Rihaoui alipokuwa akizungumza na mwandishi habari mmoja wa kigeni katika mkahawa mmoja mjini Damascus.

"Rihaoui amekamatwa kuambatana na sheria ya hali ya hatari -ushahidi kwamba sheria hiyo haikubatilishwa,kinyume na ahadi iliyotolewa" amesema mwanaharakati mmoja wa haki za binaadam Ammar Qorabi.

Jumuiya ya kimataifa inazidi kupaza sauti dhidi ya Syria.

Syrien USA Hillary Clinton
Waziri wa mambo ya nchi za je wa Marekani Hillary ClintonPicha: dapd

Rais Barack Obama wa Marekani na waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan walizungumza kwa simu jana usiku na kusisitiza juu ya umuhimu wa kuwepo "kipindi cha mpito kuelekea demeokrasia nchini Syria. Naye waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton anasema:

""Lakini tunabidi tuzidi kumshinikiza Assad kwa kuweka vikwazo katika sekta ya mafuta na gesi na tunataka kuziona nchi za Ulaya zikichukua hatua zaidi kuelekea upande huo na tunataka kuiona China ikishirikiana na sisi.Tunataka kuiona India,kwasababu India na China zimewekeza katika sekta ya nishati nchini Syria."

Wizara ya mambo ya nchi za nje wa Marekani imesema jana balozi wake mjini Damascus Robert Ford alionana na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Syria Walid al-Moallem na kumuonya vikwazo vya ziada vitapitishwa na kushinikiza vyombo vya habari viruhusiwe kuripoti kuhusu maandamano.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Afp

Mhariri: Josephat Charo