1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapambe wa Khatami wafikishwa mahakamani Iran

Josephat Nyiro Charo25 Agosti 2009

Washtakiwa kwa kupanga machafuko baada ya uchaguzi

https://p.dw.com/p/JI6K
Rais wa zamani wa Iran Mohammad KhatamiPicha: picture-alliance / dpa

Wapambe kadhaa wa rais wa zamani wa Iran, Mohammed Khatami, wamefikishwa mahakamani hii leo mjini Tehran kujibu mashataka ya kupanga machafuko baada ya uchaguzi uliofanyika Juni 12 mwaka huu nchini humo. Washukiwa hao wanatuhumiwa pia kwa kula njama ya kutaka kuipundua serikali ya Jamhuri ya kiislamu ya Iran.

Miongoni mwa washukiwa takriban 20 waliokuwa kizimbani hii leo katika mahakama ya mapinduzi ya mjini Tehran, ni waziri wa zamani anayepigania mageuzi, wanasiasa wa ngazi ya juu, waandishi wa habari wanaopigania mageuzi na wasomi. Chombo cha habari cha serikali kimesema waongozaji mashataka wamedai kuwa baadhi ya makundi ya kisiasa yakisaidiwa na nchi za magharibi na balozi za kikoloni yalivuruga hali nchini Iran na kuwatumia vibaya wafuasi wa wagombea walioshindwa, kuanzisha mapinduzi ya kichinichini.

Waongoza mashtaka wametaka makundi yanayopigania mageuzi nchini Iran kama vile Islamic Participation Front, IIPF na Islamic Revolution Mujahedeen Organisation, yavunjwe. Wameyashutumu makundi hayo kwa udanganyifu na kueneza uvumi kuhusu kufanyika mizengwe katika uchaguzi wa urais wa Juni 12 mwaka huu.

Muongozaji mashtaka wa Iran ametaka mwanamageuzi mashuhuri wa nchi hiyo, Saaed Hajjarian, ambaye pia alikuwa mahakamani hii leo, apewe adhabu ya juu kabisa inayotolewa nchini humo, kwa kuhatarisha usalama wa taifa, uhalifu ambao unaweza kuadhibiwa kwa hukumu ya kifo. Mwanamageuzi huyo, ambaye sasa ni mlemavu kutokana na shambulio lililofanywa dhidi yake kutaka kumuua mnamo mwaka 2000, amekuwa akitumikia kifungo cha nyumbani tangu alipokamatwa mnamo Juni 16 mwaka huu.

Katika ushuhuda wake aliouandika na uliosomwa kwa niaba yake kutokana na matatizo ya kiafya yanayomkabili, Hajjarian ameomba radhi kwa makosa makubwa aliyoyafanya kutokana na uchambuzi mbaya wa hali nchini Iran. Waongoza mashtaka wanadai mwanamageuzi huyo ana mafungamano na Uingereza na wakfu wa Soros ambao ulipanga kufanya mapinduzi nchini Iran.

Vyombo vya habari vya Iran pekee ndivyo vinavyoruhusiwa kuripoti kusikilizwa kwa kesi dhidi ya wanamageuzi wa Iran. Kesi hiyo imeikasirisha jumuiya ya kimataifa na kuzidisha wasiwasi wa kisiasa nchini Iran, huku nchi hiyo ikikabiliana na mzozo mbaya zaidi kuwahi kutokea tangu mapinduzi ya kiislamu ya mwaka 1979.

Wakati huo huo, mbunge mmoja wa Iran aliyekuwa mwanachama wa tume maalum ya bunge kuchunguza ripoti za wafungwa kubakwa katika jela za Iran, amesema leo kuwa madai hayo hayana msingi. Farhad Tajari amesema hayo baada ya kukutana hapo jana na mgombea urais asiye na msimamo mkali wa kidini, Mehdi Karoubi, aliyeshindwa katika uchaguzi wa Juni 12 mwaka huu.

Kwa upande mwingine imeripotiwa kwamba wabunge wa Iran waligomea futari iliyoandaliwa na rais wa nchi hiyo, Mahmoud Ahmadinejad siku ya Jumapili jioni. Kwa mujibu wa gazeti la Etemad la Iran, wabunge 20 pekee kati ya wabunge 290 walikwenda kufuturu pamoja na rais Ahmadinejad kufungua saumu wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Wabunge wamenukuliwa wakisema rais Ahmadinejad amekuwa akipuuza miito yao kumtaka awashauri juu ya baraza jipya la mawaziri.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE

Mhariri:M.Abdul-Rahman