Wapalestia waanzisha kampeni kudai taifa lao | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.09.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wapalestia waanzisha kampeni kudai taifa lao

Wapalestina hii leo wameanzisha rasmi kampeni yao ya kujiunga na Umoja wa Mataifa kama taifa, wakisema kuwa watafanya mfululizo wa matukio ya amani kuelekea mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa baadaye mwezi huu.

default

Maelfu ya wapalestina wakipeperusha bendera yao huko Ukanda wa Gaza

Kampeni hiyo inataka kutambuliwa kwa Palestina huru huko Ukingo wa Magharibi, Ukanda wa Gaza na Jerusalem Mashariki, maeneo ambayo yalitekwa na Israel katika vita vya Mashariaki ya Kati mwaka 1967. Tokea wakati huo Israel imegoma kuyarejesha maeneo hayo.

Kampeni hizo za Paletsina kutaka kuwa taifa la 194 mwanachama wa Umoja wa Mataifa zitaanza siku ya Jumapili huko Ukanda wa Gaza kwa watoto kutembea kutoka Kusini hadi kaskazini mwa ukanda huo huku wakipeperusha bendera za Palestina na kuimba nyimbo za kuunga mkono kuanzishwa kwa taifa lao.

Lakini hata hivyo kimsingi kampeni hizo zilianza leo Alhamis ambapo kiasi cha maafisa wa mamlaka ya Palestina pamoja na wanaharakati wapatao 100 walikusanyika katika ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Ramallah na kukabidhi barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon kumuomba kuikubali Palestina kama taifa mwanachama kwenye umoja huo.

Hata hivyo ombi rasmi kutoka kwa serikali ya mamlaka ya ndani ya Palestina bado halijawasilishwa. Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, leo alikuwa na kikao na wakuu wa chama cha Palestine Liberation Organisation, PLO, kamati kuu ya chama chake cha Fatah pamoja na makatibu wakuu wa makundi mengine ya kisiasa ya kipalestina ili kukamilisha hatua hiyo ya kuomba rasmi uwanachama kwenye Umoja wa Mataifa.

Barua hiyo ya wanaharakati iliwasilishwa leo na bibi kizee mmoja mwenye umri wa miaka 70 Latifa Abu Hmeid ambaye mwanawe mmoja wa kiume aliuawa katika mapigano na Israel na wengine saba wanashikiliwa katika magereza ya Israel kwa tuhuma za ugaidi. Bibi huyo alichaguliwa kuwasilishwa barua hiyo kutoka na historia yake kuwa inaonesha dhahiri madhila wanayokabiliana nayo Wapalestina.

Kampeni hizo za amani zitaendelea hadi tarehe 21 mwezi huu wakati wa ufunguzi wa kikao cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani ambapo siku mbili baadaye Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas atalihutubia baraza hilo, na kuomba rasmi uwanachama wa umoja huo, ikiwa ni takriban miongo miwili ya juhudi za amani kushindikana.

Hata hivyo bado haijafahamika wazi iwapo ombi hilo litawasilishwa katika baraza kuu la umoja huo, au Baraza la Usalama. Baraza la Usalama linahitaji kura tisa kati ya wanachama 15 wa baraza hilo, bila ya kuwepo kwa kura yoyote ya turufu kutoka kwa wanachama watano wa kudumu wa baraza hilo. Marekani hata hivyo inatarajiwa kutumia kura yake ya veto kupinga ombi hilo la Palestina.

Ijapokuwa wapalestina wamesema kuwa kampeni yao hiyo itakuwa ya amani, maafisa wa jeshi la Israel wana wasiwasi kuwa maandamano katika ukingo wa magharibi huenda yakageuka na kuwa ghasia na vurugu.

Vikosi vya usalama vya Israel vimekaa katika hali ya tahadhari ya kuzuka kwa ghasia, kwa kufanya mazoezi pamoja na vifaa vya kukabiliana na ghasia

Mwandishi Aboubakary Liongo

Mhariri:Josepha Charo

 • Tarehe 08.09.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12Vb7
 • Tarehe 08.09.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12Vb7

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com