1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake Saudia marufuku Olympiki

4 Juni 2012

Wakati wanamichezo ulimwenguni wakiingia hatua ya mwisho ya mazoezi kwa ajiri ya mashindano ya Olympiki mjini London, Saudi Arabia imepiga marufuku ushiriki wa wanamichezo wake wa kike katika mashindano hayo.

https://p.dw.com/p/14oF3
Timu ya taifa ya mpira wa miguu ya wanawake wa Iran wakiwa wamevaa hijab
Timu ya taifa ya mpira wa miguu ya wanawake wa Iran wakiwa wamevaa hijabPicha: picture-alliance/abaca

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Kamati ya Olympiki nchini humo mwana wa mfalme Nawwaf bin Faisal na kusema wanawake watashiriki katika mashindano yoyote kama watavaa mavazi kulingana na maadili ya dini ya Kiislam. Lakini amesema hilo linaweza kufanyika kama wanamichezo hao watapewa mwaliko kutoka nje.

Saudia itatumia muda mrefu kuwa wanamichezo wa kimataifa

Rais huyo wa kamati ya Olympiki anasema ushiriki pekee kwa Saudia utakuwa wa wanaume tu. Hali ya ushiriki wa michezo kwa wanawake nchini humo ni ngumu kwani wanaweza kufanya mazoezi katika maeneo jirani na hospitali au katika vituo vya Afya tu wakati wanaume wakiwa na nafasi kubwa ya kushiriki michezo.

Kwa sasa kuna klabu 153 za michezo ambazo ni za wanaume tu, kulingana na Antony Billlingsley ambaye ni Mhadhiri wa masomo ya kimataifa kuhusu mashariki ya mbali katika Chuo Kikuu cha New South Wales huko Australia anasema hata kama Saudia itaruhusu wanawake kushiriki mashindano ya kimataifa, itawachukua miaka mingi kuweza kuwa na wanamichezo wa kimataifa.

Duara za kuonyesha mashindano ya Olympiki zilizotengenezwa kwa maua zaidi ya 25,000 huko London
Duara za kuonyesha mashindano ya Olympiki zilizotengenezwa kwa maua zaidi ya 25,000 huko LondonPicha: Reuters

Mtangazaji wa Redio ya ABC ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha RMIT mjini Melbourne Nasya Bahfen anasema hatua ya Saudia inatokana na sheria za dini ya kiislamu kukataza wanawake na wanaume kuchanganyika pamoja.

Kumuacha mwanamke anakimbia akiwa amevaa nguo fupi ni dhambi

dhambi kubwa na ni kinyume cha imani ya kiislamu lakini nchini Iran wanawake wanakatazwa kabisa kutazama mpira wa miguu wakiwa kiwanjani. Pamoja na hayo hali ya kimichezo ya Iran ni afadhali kidogo kuliko ya Saudia.

Christopher Wilcke ambaye ni mwandishi vitabu na mtafiti wa haki za binadamu anasema wanawake wanapenda michezo na wanapewa nafasi kubwa katika dini zote,ya kushiriki katika michezo. Hakuna dini inayokataza wanawake kushiriki michezo bali kinachofanyika, wanaume wanapenda kuwakandamiza wanawake. Basi wanatumia nafasi hiyo kuwataka wanawake wabaki nyumbani na wasitoke ndani ya makaazi yao.

Mtafiti huyo anaongeza kuwa kupiga marufuku ushiriki wa wanawake hakulitatui tatizo bali kunafanya hali kuwa mbaya zaidi. Anasema kitendo cha taifa hilo kutaka wanaume pekee yao kushiriki mashindano hayo ni kukiuka kabisa sheria na Olympiki na kunawanyima haki ya kushiriki.

Anasema kipindi kilichosalia ni muhimu kulitatua hilo. Hali kama hiyo iliikumba Afghanistan mwaka1999, na pia Qatar na Brunei ambazo zote mwaka huu watapeleka wakimbiaji wa kike kwa mara ya kwanza kwenye michezo hiyo.

Mchezaji mpira wa miguu wa timu ya wanawake wa Iran akipambana na wapinzani wake uwanjani
Mchezaji mpira wa miguu wa timu ya wanawake wa Iran akipambana na wapinzani wake uwanjaniPicha: picture-alliance/dpa

Hali hii haipo katika michezo tu bali wanawake wa Saudi Arabia hawaruhusiwi pia kuendesha gari. Chini ya kile kinachotajwa kuwa ni udhibiti wa mwanamme, mwanamke huhitaji hata ruhusa ili kutibiwa kufanya kazi, kusoma na hata katika masuala ya ndoa.

Nasya Bahfen anaongeza kuwa wanawake wanatakiwa kupata elimu sawa na wanaume, kwani sasa wanawake wanahitajika mno kuwa matabibu, wauguzi na walimu lakini kumekuwepo na ushawishi mdogo kufanya hivyo. Haya yanaweza kutokea kama patakuwepo na mabadiliko katika sera za taifa hilo katika sekta ya elimu kwa wanawake na katika siasa.

Mwandishi:Adeladius Makwega/IPS

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman