1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake kabla na baada ya ukuta kuporomoka

Oumilkher Hamidou2 Novemba 2009

Hali ya akinamama wa mashariki na magharibi ya Ujerumani miaka 20 baada ya ukuta kuporomoka

https://p.dw.com/p/KINe
Mwanamke anamshukuru polisi ukuta ulipoporomokaPicha: DW

Ukuta wa Berlin ulipoporomoka Novemba tisa mwaka 1989,wanaharakati wengi wa kike katika ile iliyokuwa zamani ikijulikana kama jamhuri ya kidemokrasi ya Ujerumani -GDR,walikuwa wakihofia wasije wakatengwa mageuzi yatakapofanyika.Makundi kadhaa ya wakinamama yaliyokuwa yakisimamiwa na kanisa ,yakaamua kuungana mnamo msimu wa mapukutiko wa mwaka 1989 na kuunda shirikisho huru linalopigania masilahi ya akinamama-UFV.Kupitia shirikisho hilo akinamama wakajipatia njia ya kutoa maoni yao kila wakati ambapo mikutano ilikua ikiitishwa.Miaka 20 baadae wakinamama wanatathmini kilichofikiwa.

Wakinamama katika Jamhuri ya Ujerumani mashariki ya zamani-GDR walikuwa wakivijunia haki sawa na wananchi wenzao wa jinsia ya kiume.Walikuwa wakiruhusiwa kufanya kazi zote.Katika viwanda,mashambani, wakifanyakazi kama wahandisi,walikuwa madaktari na hata matrekta walikuwa wakiendesha,sawa na waume zao,hata kama walikuwa na watoto.Serikali iliwarahisishia njia ya kutekeleza majukumu yote mawili - kazi na familia.Watoto walikuwa wakipelekwa na kushinda siku nzima shuleni na watoto wadogo zaidi wakilelewa katika shule za chekechea.Sura ya wakinamama katika enzi za siasa za ujamaa ilianza kuingia madoa tangu miaka ya 80, hata kabla ya ukuta kuporomoka,kama anavyosema mtaalam wa saikolojia Hildegard Maria Nickel katika uchunguzi wake.Wakinamama walizidi kukereka kwasababu wakirejea nyumbani kutoka kazini walilazimika pia kufanya kazi zote za nyumbani.Zaidi ya hayo walikuwa wakinyimwa nafasi ya kushikilia nyadhifa za kisiasa au serikalini.

Kwa namna hiyo hali ya maisha ya wakinamama wa mashariki ikawa sawa na ile ya wakinamama wenzao wa magharibi.Katika miaka ya 80,walikuwa wakinamama wachache tuu wa magharibi waliokuwa wakiwakilishwa katika bunge la shirikisho-Bundestag.Kanuni zilizokuwa zikidai hali ya usawa,mfano madai ya kutengwa idadi maalum ya wakinamama wanaobidi kuwakilishwa bungeni na kadhalika,mpaka leo bado zimesalia karatasini.Nafasi ya wakinamama wa magharibi ilikuwa pembezoni mwa waume zao.Walikuwa wakiangaliwa kuwa wao ni mama tuu wanaolea watoto ,wanaowatunza waume zao na kuzitunza nyumba zao.

Msimu wa mapukutiko mwaka 1989 ulipowadia ukuta ukaporomoka na sehemu mbili za Ujerumani kuungana-wakinamama wa mashariki na magharibi wakalinganisha hali zao.Wakinamama wa mashariki walihisi ni jambo la kawaida kwao kufanya kazi na kujipatia mshahara wao.Katika baadhi ya sekta walikuwa wakitoa madai ,hasa anasema Hildegard Maria Nickel:

"Novemba mosi mwaka 1989,kwa hivyo kabla ya ukuta kuporomoka,wanawake waliungana kutokana na juhudi za jarida la wakinamama la GDR-"Für Dich."Tukachapisha risala katika jarida hilo tukiuliza "mageuzi yanawezekana bila ya wakinamama?Hii leo nikiiangalia risala hiyo,basi nnaweza kusema ilikuwa ya kijasiri.Tulidai pawepo viwango.Tumetaka pawepo vuguvugu huru la wakinamama.Kimsingi,upuuzi mtupu kwa sababu tuliamini viongozi wa chama walilazimika kuturuhusu kwa sababu ni haki yetu.Kwa hivyo tukijiambia tuu,baba atafanya tuu."

Sauti za wakinamama tangu wa mashariki mpaka wa magharibi waliokuwa wakidai haki sawa kati ya wanawake na wanaume zilianza kupwaya tangu Machi 18 mwaka 1990.Wengi kati ya wanaharakati wakike wa Ujerumani mashariki ya zamani wamepoteza kazi walizokuwa nazo na kwa namna hiyo,wamepoteza pia uhuru wao wa kiuchumi.

Mwandishi:Wrege Henriette/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Abdul-Rahman