1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biwott, Keittany washinda New York Marathon

2 Novemba 2015

Wakenya Stanley Biwott na Mary Keitany wameshinda mataji ya wanaume na wanawake ya mbio maarufu kabisa duniani za New York Marathon zilizoandaliwa Jumapili nchini Marekani

https://p.dw.com/p/1GyR3
USA New York Marathon - Mary Keitany & Stanley Biwott
Picha: Reuters/M. Segar

Biwott ndiye mkenya wa 11 tofauti kushinda mbio za New York marathon. Bingwa huyo wa mwaka wa 2012 wa Paris marathon alikuwa wa pili katika mbio za London mwaka wa 2014 na wa tano katika mbio zilizopita za New York marathon mwaka wa 2013. Biwott alisema "katika mbio zilizopita za London Marathon na New York Marathon, nilishindwa kukimbia kilomita tano za mwisho katika kasi thabiti. Hivyo katika maandalizi yangu kwa ajili yam bio za mwaka huu za New York nilifanya mazoezi ya kilomita 42 na sio 35 ili kumaliza kwa kasi bila kukimbia polepole kuelekea mwisho. Hivyo nilikuwa na matumaini na furaha kuwa mshindi wa leo".

Biwott alitimka kwa kasi na kumwacha Mkenya mwenzake Geoffrey Kamworor maili ya mwisho na kushinda mbio za wanaume kwa kutumia saa mbili sekunde 34. Kamworor ndiye bingwa wa dunia wa mbio za nyika. Bingwa wa mbio za Boston Marathon Lelisa Desisa Muethiopia alimaliza wa tatu.

Katika upande wa wanawake, bingwa mara mbili wa London Marathon Keitany alikuwa mwanariadha wa kwanza kuhifadhi taji la New York Marathon baada ya Mwingereza Paula Radcliffe aliyefanikiwa kutwaa taji hilo 2007 na 2008. Keittany alisema "ninachoweza kusema ni kuwa nilikuwa na matumaini makubwa sana wakati nikija kushiriki katika mbio za New York marathon. Nilipokuwa nyumbani, mazoezi yangu yalikuwa sawa. Nilitaka kuja hapa na kujaribu kutetea taji langu. Nilijua ushindani ulikuwa mkali kwa sababu tulikuwa na bingwa wa London na pia bingwa wa 2013 wa mbio hizi. Lakini naifahamu barabara hii maana nimekuja New York mara nyingi. Hivyo nilifurahi sana kumaliza wa kwanza na namshukuru Mungu kwa hilo".

Keittany alimshinda Muethiopia Aselefech Mergia na kumaliza mbio hizo katika muda wa 2:24:25. Muethiopia mwingine, Tigist Tufa, aliridhika na nafasi ya tatu.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu