1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanariadha wa Kenya waandamana

24 Novemba 2015

Kundi la wanariadha wa Kenya limevamia makao makuu ya shirikisho la riadha Kenya – Athletics Kenya (AK) na kufunga milango wakilalamikia ufisadi katika shirikisho hilo mjini Nairobi

https://p.dw.com/p/1HB1G
China Leichtathletik WM in Peking - Männer 1500m - Asbel Kiprop
Picha: Getty Images/A. Lyons

Wanariadha hao waliwazuia maafisa wa shirikisho hilo la AK kuingia afisini mwao katika jumba la Riadha mjini Nairobi. Walibeba mabango yenye ujumbe wa kuwakashifu viongozi wa riadha wakisema ni wafisadi

Maandamano hayo yanafuatia madai ya hivi punde kuwa takriban dola laki saba za Marekani fedha za ustawishaji wa riadha nchini Kenya ziliporwa na maafisa wakuu watatu wa shirikisho hilo. Fedha hizo zilikuwa zimetolewa na kampuni ya kutengeneza bidhaa za michezo Nike.

Nike ndio iliyopewa zabuni ya kutengeza sare za timu ya taifa ya riadha ya Kenya. Naibu mwenyekiti wa shirikisho hilo David Okeyo ambaye anachunguzwa na idara ya kupambana na ufisadi anakana kuhusika na ufisadi.

Wanariadha hao wanalaumu Atheltics Kenya kwa kupokea hongo kutoka kwa mawakala wanaoshukiwa kuwashawishi wanariadha nchini humo kutumia dawa za kuongeza misuli nguvu.

Kenya ni moja ya mataifa yaliyotajwa kuwa na tatizo la matumizi ya dawa hizo za kuongeza nguvu mwilini na shirikisho la kupamabana na matumizi ya dawa hizo duniani - WADA.

Afisa aliyeongoza uchunguzi wa shirikisho la riadha duniani Dick Pound alishauri WADA iangazie kurunzi yake kwenye afisi za shirikisho la riadha la Kenya baada ya kuitimua Urusi.

Mwandishi: Sekione Kitojo/afp
Mhariri: Bruce Amani