1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanamgambo waiteka miji mingine miwili Iraq

Josephat Nyiro Charo13 Juni 2014

Wanamgambo wa Kisunni wamefaulu usiku wa kuamkia leo (13.06.2014) kuingia katika miji miwili ya mkoa wa mashariki wa Diyala, huku rais wa Marekani, Barack Obama, akitishia kutumia mashambulizi ya angani dhidi yao.

https://p.dw.com/p/1CHnT
ISIS Kämpfer Checkpoint bei Mosul 11.06.2014 Karussel
Picha: Reuters

Baada ya vikosi vya usalama kuondoka katika vituo vyao vya doria, duru za usalama zinasema miji ya Saadiyah na Jalawla, imeanguka mikononi mwa wanamgambo wa kundi la Islamic State of Iraq and Levant, ISIL - Dola la Kiislamu la Iraq na eneo la Shamu - pamoja na vijiji kadhaa vinavyoizunguka milima ya Himreen, ambayo kwa muda mrefu imetumiwa kama ngome ya wanamgambo. Kwa mujibu wa ripoti ya televisheni ya Al Arabiya, mji wa Jalula mashariki mwa Iraq nao pia umetekwa na wanamgambo hao.

Wanamgambo wa kundi hilo waliuteka mji wa Mosul mapema wiki hii na tangu wakati huo wamekuwa wakisonga mbele upande wa kusini kuelekea mji mkuu Baghdad, katika harakati dhidi ya serikali inayoongozwa na Washia.

Wakurdi, ambao wana eneo lao kaskazini mwa Iraq lenye utawala wa ndani wametumia machafuko hayo kutanua himaya yao, kwa kuudhibiti mji wa mafuta wa Tikrit na maeneo mengine nje ya mpaka rasmi wa eneo lao. Vikosi vya Kikurdi vimewatuma maafisa wake wa usalama kuzilinda ofisi za chama cha siasa mjini Jalawla kabla wanamgambo kuwasili mjini humo. Hakuna makabiliano yoyote yaliyoripotiwa.

Duru za usalama zinasema jeshi la Iraq limefyetua risasi na makombora katika miji ya Saadiya na Jalawla kutoka mji ulio karibu wa Muqdadiya, na kuzilazimu familia kadhaa kuukimbilia mji jirani wa Khaniqin, karibu na mpaka na Iran.

Iraq itahitaji msaada

Waziri wa mambo ya kigeni wa Iraq, Hoshiyar Zebari amekiri kwamba vikosi vya usalama ambavyo Marekani iliwekeza mabilioni ya dola kuwapa mafunzo na silaha, kabla kuwaondoa wanajeshi wake nchini humo mnamo mwaka 2011 vimesambaratika.

Barack Obama und Nouri al-Maliki
Rais Barack Obama, kulia, na waziri mkuu wa Iraq, Nuri al MalikiPicha: dapd

Rais wa Marekani, Barack Obama, amesema Iraq itahitaji msaada wa Marekani na jumuiya ya kimataifa na anatafakari hatua zote zinazoweza kuchukuliwa kuviokoa vikosi vya Iraq visivunjike. Akizungumza jana katika ikulu yake mjini Washington, Obama alisema, "Hatufutilii mbali hatua yoyote kwa sababu tuna masilahi kuhakikisha wapiganaji hawa wa Jihad hawapati udhibiti wa kudumu nchini Iraq au Syria." Obama aliyasema hayo alipoulizwa kama alikuwa anatafakari kutumia mashambulizi ya kijeshi ya angani. Maafisa baadaye walisisitiza kwamba wanajeshi w ardhini hawatatumwa Iraq.

Akizungumzia machafuko mapya nchini Iraq, waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema, "Tuna wasiwasi mkubwa sana kuhusu yanayoendelea nchini Iraq na hatukai tu kuikodolea macho hali ilivyo bali tunatoa msaada. Tuna mawasiliano ya moja kwa moja na waziri mkuu Nuri al Maliki na viongozi wengine wa ngazi ya juu. Nimekamilisha mazungumzo kwa njia ya simu na watu wa Iraq na nafahamu rais wa Marekani yuko tayari kupitisha maamuzi muhimu katika kipindi kifupi. Kama alivyoweka wazi hapo awali, kuna masuala yanayozingatiwa na kwa wakati muafaka nina hakika rais atatangaza uamuzi wake."

Wamarekani wahamishwa

Afisa wa wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, amesema kampuni za Marekani zinawaondoa mamia ya Wamarekani wanaofanya kazi na serikali ya Iraq katika kambi ya jeshi la angani ya Balad, yapata kilometa 70 kaskazini mwa mji mkuu, Baghdad. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Jen Psaki, amesema kampuni zinawahamisha wafanyakazi wake katika maeneo mengine kwa sababu ya hali mbaya ya usalama katika eneo hilo.

Lawrow PK in Moskau 12.05.2014
Waziri wa mambo wa kigeni wa Urusi, Sergei LavrovPicha: Yuri Kadobnov/AFP/Getty Images

Wakati huo huo, waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema ufanisi wa wanamgambo kuyadhibiti maeneo ya Iraq kunadhihirisha uvamizi dhidi ya Iraq mwaka 2003 ulioongozwa na Marekani kufuatia mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 mwaka 2001, katika miji ya Washington na New York nchini Marekani, haukuwa na maana yoyote.

Lavrov aidha amesema kusambaratika kabisa kwa jeshi la Iraq lililopewa mafunzo na nchi za magharibi kunadhihirisha dhahiri shahiri kushindwa kabisa kwa juhudi zilizozijumuisha Marekani na Uingereza nchini Iraq.

Wapinzani wa Obama wa chama cha Republican katika bunge la Marekani walikuwa haraka kumkosoa rais huyo kwa kuiacha mkono Iraq kwa kuwaondoa wanajeshi wake mwaka 2011. Seneta Lindsey Graham ameonya iwapo wapiganaji wa Jihad huenda watachukua usukani nchini Iraq na taifa jirani la Syria, patazuka machafuko makubwa na ametaka nguvu za jeshi la angal la Marekani zitumike kubadili mkondo wa mambo katika uwanja wa vita.

Mwandishi: Josephat Charo/DPAE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman