1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajweshi wa Ujerumani waingia midomoni magazetini

26 Oktoba 2006

Kashfa ya bufuru la kichwa cha binaadam nchini Afghanistan imechambuliwa kwa mapana na marefu na wahariri wa Ujerumani

https://p.dw.com/p/CHUb

Kashfa ya picha za wanajeshi wa Ujerumani wanaochezea bufuru la kichwa cha binaadam nchini Afghanistan na kuidhinishwa mageuzi ya mfumo wa afya ndizo mada zilizohanikiza magazeti ya Ujerumani hii leo.

Picha za wanajeshi wa Ujerumani,waliokua wakichezea fuvu la kichwa cha binaadam,bila ya hishma yoyote,na wakati mwengine kwa karaha na uchafu,zimewahuzunisha sana wanasiasa wa Ujerumani.Kansela Angela Merkel amesema picha hizo zinachusha na ni za kinyaa.Sawa na waziri wa ulinzi Franz Josef,kansela Angela Merkel amesema uchunguzi kamili unafanywa.

Kuhusu kashfa hiyo,gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG linaandika:

“Wanasiasa wa Ujerumani wamelaani kwa sauti moja picha za kukirihisha za baadhi ya wanajeshi wa Ujerumani-Bundeswehr waliokua wakichezea bila ya hishma bufuru la binaadam.Licha ya ghadhabu na mshtuko,baraza la mawaziri limefanya vizuri lakini kurefusha siku hiyo hiyo muda wa shughuli za wanajeshi wa Ujerumani nchini Afghanistan na kuafikiana juu ya waraka mpya ujulikanao kama Weißbuch-au kitabu cheupe.Kwa namna hiyo serikali kuu ya Ujerumani imedhihirisha kwamba imani ya serikali kwa jeshi la shirikisho Bundeswehr haijatetereka licha ya utovu wa baadhi ya wanajeshi.Hata hivyo kuna sababu za watu kuingiwa na wasi wasi,kwamba picha hizo zinaweza kuzusha zilzala nchini Afghanistan na katika nchi nyengine za kiislam.Maadui wa nchi za magharibi katika nchi hizo wanaweza kukitumia kisa hicho na kugeuka kashfa nyengine ya Abu Ghreib.”

Gazeti la HANDELSBLATT la mjini Düsseldorf limeandika yafuatayo kuhusu kashfa hiyo.



“Bila ya shaka uzembe wa kisiasa hauwezi kuhalalisha hata kidogo utovu kama ule uliofanywa na wanajeshi nchini Afghanistan.Hata hivyo lazma kitafutwe chanzo cha hali hiyo. Peter Struck alipodai kwamba wanajeshi wa Ujerumani kamwe hawawezi kufanya mambo kama yale yale yaliyofanywa na wanajeshi wa kimarekani GI’s huko Abu Ghraib,hajazingatia kile kinachoweza kuwasibu wanajeshi wanapokua katika haali ya kivita.Ni kweli kabisa kwamba kashfa ya Abu Ghraib mbaya zaidi na haiwezi kulinganishwa na hii ya sasa nchini Afghanistan.Lakini kwani neno mbaya zaidi si limetokana na mbaya?”LInajiuliza gazeti la Handelsblatt la mjini Düsseldorf.

Gazeti la mjini Rostock OSTSEE-ZEITUNG linaandika:

„Uchafu kama ule ambao bila ya shaka umejiri walipokua wakipiga doria saa za alfajiri katika vitongoji vya mji mkuu Kaboul,unahatarisha usalama wa Ujerumani nchi za nje.Utovu huo sio tuu unachafua maadili ya kimsingi ambayo wajerumani wanayathamini kupita kiasi,lakini pia umezusha ghadhabu na chuki miongoni mwa wananchi wa Afghanistan na kwengineko,na kuichafulia Ujerumani sifa yake.Picha hizi ni sawa na kunyunyizia mafuta katika cheche za moto unaopaliliwa na wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam,wapate kusema-Mnaona-huo ndio uhuru na demokrasia inayopigiwa upatu na nchi za magharibi.“

Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linahisi:

„Inaangia akilini pale wanasiasa wanapokasirishwa na visa vichafu vya wanajeshi wa Ujerumani.Lakini wanabidi pia wafanye kila liwezekanao kuepusha utovu kama huo.Mabishano halisi ya kutumwa nchi za nje wanajeshi wa Ujerumani bado hayajaanza.Ujerumani ilitaka kusaidia tuu,lakini tunajikuta tukitumbukia katika janga la vita.“

Sasa tuigeukie mada ya pili magazetini.Baada ya mvutano wa miezi kadhaa,serikali ya muungano wa vyama vikuu imekubaliana kuufanyia marekebisho mfumo wa bima ya afya.Serikali kuu hivi sasa imeingia mbioni kuhakikisha bunge la shirikisho linaidhinisha mopango huo.Wakati huo huo serikali kuu inaendelea kuwatanabahisha wapinzani wa mpango huo.Maoni ya wahariri yanatofautiana sana katika mada hiyo.