1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi watatu wa Kimarekani wauliwa Iraq, licha ya Wa-Iraqi wengi kufa.

17 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CBHy

Baghdad:

Bomu lililotegwa barabarani limewauwa wanajeshi watatu wa Kimarekani na kumjeruhi mwengine kaskazini ya mji wa Baghdad. Hiyo inafanya kuwa zaidi ya 60 idadi ya wanajeshi wa Kimarekani waliouliwa Iraq katika mwezi huu wa Disemba. Tangu Marekani ilipoivamia Iraq wanajeshi 2,950 wa Kimarekani wameuliwa. Licha ya hayo, si chini ya Wa-Iraqi 23 waliuliwa jana, akiwemo shehe na pia mwanasiasa wa madhehebu ya Sunni ambao walifyetuliwa risasi katika mji wa Iskandariya, kusini mwa Baghdad.

Na kwa upande mwengine, waziri mkuu wa Iraq, Nouri al-Maliki, amewahimiza wanachama wa zamani wa Chama cha Baath cha Saadam Hussein wajiunge na jeshi jipya la nchi hiyo. Pia alisema serekali itaizingatia upya ile amri iliowapiga marufuku wanachama wa zamani wa Chama cha Baath cha Saadam kuwemo jeshini na kukamata nyadhifa za juu serekalini. Bwana al-Maliki alisema hayo katika ufunguzi wa mkutano wa upatanishi wa taifa ulio na madhumuni ya kupambana na michafuko iliotapakaa baina ya makundi ya madhehebu ya kidini ya nchi hiyo. Hata hivyo, mkutano huo unasusiwa na Waislamu wa madhehebu ya Sunni na Shia walio na misimamo mikali. Marekani imeikaribisha taarifa hiyo ya Bwana al-Maliki.