1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamisri hawajatosheka na yampatayo Mubarak

13 Aprili 2011

Rais wa zamani wa Misri anayesumbuliwa na matatizo ya moyo Hosni Mubarak ,pamoja na wanawe wawili wa kiume wamekamatwa na kwa mujibu wa waendeshaji mashtaka wa serikali, wote wanazuiliwa kwa siku 15.

https://p.dw.com/p/10sRc
Waandamanaji nje ya hospitali ya Sharm-el-Shaikh
Waandamanaji nje ya hospitali ya Sharm-el-ShaikhPicha: AP

Taarifa kutoka kenye ukurasa wa mtandao wa Facebook wa mwendesha mashtaka ni kwamba mwendesha mashtaka mkuu wa serikali Abdel Maguid Mahmud alimamuru kuzuiliwa huko Kwa Mubarak na wanawe kama sehemu ya uchunguzi unaofanywa wa matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji wakati wa maandamano ya mageuzi yaliyofanywa nchini humo Januari na Februari mwaka huu.

Maafisa wa usalama wamesema kuwa Mubarak anazuiliwa katika hospitali moja ya eneo la Sharm El Sheikh kule eneo la mapumziko la bahari ya Shamu ambako inadaiwa alipatwa na mshtuko wa moyo hapo jana wakati akihojiwa na waendesha mashtaka.

Polisi imesema kuwa wanawawe wawili mubarak, gamal na alaa waliwasili katika gereza la Tora mjini Cairo nyumbani kwa maafisa wengine walioangushwa na pia baadhi ya wafungwa sugu wa kisiasa nchini humo.

Mubarak na wanawe wanashtakiwa kwa uchochezi wa kufyatuliwa risasi waandamanaji wakati wa maandamano ya mapinduzi ambayo yalidumu kutoka januari 25 hadi Februari 11 wakati mubarak alilazimika kusalimu amri na kujiuzulu. Kiasi ya watu 800 walifariki wakati wa vurumai hizo.

Awali runinga ya kitaifa ilisema kuwa nduguze mubarak wanazuiliwa kwa siku kumi na tano kwa ajili ya uchunguzi na walikuwa kwanza wamehojiwa katika eneo la Sharm El Sheikh.

Video zilizowekwa kwenye mtandao wa Youtube zilionyesha kile kilichoonekana kama waandamanaji nje ya mahakama ambako nduguze Mubarak walikuwa wakihojiwa.

Uchunguzi huo uliamrishwa siku ya Jumapili na mkuu wa mashtaka wa serikali kama sehemu ya uchunguzi wa tuhuma za ufisadi na matumizi mabada ya mamlaka.

Familia hiyo ya Mubarak inatarajiwa kuulizwa kuhusu madai kuwa walishiriki katika uhalifu wa dhulma dhidi ya waandamanaji na kusababisha vifo na majeraha kwa baadhi yao.

Waziri wa sheria Abdel Aziz Al Guindi alisema kuwa waendesha mashtaka walikuwa wameanza kumhoji Mubarak na mwanawe Gamal hapo jana, na kwamba mahojiano kuhusu unyakuzi wa mali hayakuwa yameanza kwa sababu swala hilo litashughulikiwa na idara ya kupambana na mapato bandia.

Runinga ya taifa iliripoti kuwa kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 82 alikuwa amesusia kula au kunywa tangu alipopokea habari jana asubuhi kuwa alipaswa kuhojiwa.

Baada ya kujizulu, Mubarak na familia yake walihamia katika makaazi ya Sharm El Sheikh. Kumekuwa na maandamano kila wiki ya kutaka ashtakiwe ambapo maelfu ya watu wamejitosa barabarani na kukabiliana na wanajeshi mapema Jumamosi katika uwanja wa Al Tahrir.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri:Abdul-Rahman