1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamarekani weusi 9 wauliwa

18 Juni 2015

Mwanamume wa Kimarekani aliyetekeleza shambulizi wakati wa maombi katika kanisa la kihistoria la Wamarekani weusi eneo la Charleston katika jimbo la South Carolina, ambapo watu 9 wameuliwa hajatiwa mbaroni.

https://p.dw.com/p/1FjEG
USA Schießerei in einer Kirche in South Carolina
Walofiwa wakiwa nje ya kanisaPicha: picture-alliance/epa/R. Ellis

Mwanamume wa Kimarekani aliyetekeleza shambulizi wakati wa maombi katika kanisa la kihistoria la Wamarekani weusi eneo la Charleston katika jimbo la South Carolina, ambapo watu 9 wameuliwa hajatiwa mbaroni.

Maafisa waliojihami kwa bunduki kwa usaidizi wa mbwa wa kunusa wameendeleza msako katika barabara na mitaa jimboni humo, huku maafisa hao wakisema mshukiwa ni kijana mwenye umri wa miaka 21 anayesemekana kuwa mwenye nywele za timtimu na alikuwa amevalia shatitao, dangarizi au jeans na buti.

Kwa mujibu wa Afisa Mkuu wa Polisi katika jimbo hilo, Gregory Mullen, milio ya risasi ilisikika ndani ya kanisa la Emanuel AME jimboni humo Jumatano usiku na kuongeza kuwa mshukiwa huyo ambaye hajatiwa mbaroni ni hatari kwa usalama. Mullen amewaambia wanahabari kuwa:

"Hatua ya mtu wa kuogofya kuingia kisha kufyatua risasi haielezeki, bila shaka ni kisa kisichovumilika wala kuaminika. Sababu ya pekee ya mtu kuingia hadi kanisani kuwapiga watu risasi ni chuki."

Kisa hiki kinavuta kumbukizi la shambulio la mwaka wa 1963 kwenye kanisa jingine la Wamarekani wenye asili ya Afrika katika mji wa Birmingham jimboni Alabama ambapo wasichana wanne waliouliwa, hali ambayo mwaka wa 1960 ilichochea kuanzishwa kwa vuguvugu la kupinga chuki dhidi ya Wamarekani weusi.

Charleston ni mojawapo la makanisa makuu na ya zamani zaidi ya Wamarekani weusi. Lina historia tokea karne ya 19 la jengo la sasa lililokamilika 1891 linatajwa kuwa la kihistoria kwa mujibu wa Idara ya Huduma ya Makavazi nchini Marekani, NPS.

Mauaji ya jana yanafuatia yale ya Aprili mwaka huu ambapo Mmarekani mweusi ambaye hakuwa amejihami alipigwa risasi na afisa wa polisi wa Kimarekani. Afisa huyo ameshtakiwa kwa tuhuma za mauaji, miongoni mauaji dhidi ya Wamarekani weusi wasiojihami yanayotekelezwa na maafisa wa polisi na kuzidisha hofu kuhusu ubaguzi nchini Marekani.

Punde baada ya shambulio hilo, kundi la wanaume lilikusanyika nje ya hoteli moja iliyoko karibu na kanisa hilo, mojawapo la majengo maarufu katika jimbo hilo.

"Tunaombea na familia za waliouliwa, wana kipindi kigumu cha majonzi mbele yao," amesema mchungaji wa kanisa, James Johnson ambaye pia ni mwanaharakati wa haki ya jamii.

Shirika la Ujasusi la Marekani FBI, Mamlaka ya Kudhibiti Vileo, Tumbaku, Silaha na Vilipuzi na mashirika mengine yameungana katika uchunguzi, amesema afisa Mkuu wa Polisi katika jimbo hilo, Gregory Mullen.

Mullen vilevile amewaambia wanahabari kuwa wanane miongoni mwa waliofariki walipatikana kanisani, huku mmoja akiaga dunia baada ya kufikishwa hospitalini. Mwengine mmoja amejeruhiwa na anatibiwa katika hospitali moja eneo la.

Walioathirika hawakutambuliwa mara moja japo Al Sharpton, kiongozi wanaharakati wa haki za binadamu kwenye ujumbe wa twitter amesema kuwa Clementa Pinckney, mchungaji wa kanisa la Kanisa la Charleston ambako shambulio hilo lilitokea ni miongoni mwa walioaga dunia.

Punde baada ya shambulio hilo la risasi, taarifa kuhusu kutegwa kwa bomu karibu na kanisa hilo ilitolewa, amesema afisa mmoja katika Kaunti ya Charleston, Eric Watson huku watu waliokusanyika eneo hilo wakiamriwa kuondoka. Afisa huyo alifika eneo hilo ambako ndege ya polisi ilikuwa ikiangaza taa kutoka angani huku polisi wakilizingira.

Kufuatia shambulio hilo, mgombea urais wa chama cha Republican Jeb Bush, aliyewahi kuwa Gavana wa Florida amefutilia mbali ziara yake eneo la Charleston iliyopangiwa kufanyika Alhamisi asubuhi.

Mwandishi: Geoffrey Mung'ou

Mhariri: Josephat Charo