1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamarekani wapiga kura uchaguzi wa katikati ya muhula

Sophia Chinyezi6 Novemba 2018

Wamarekani leo Novemba 6, watapiga kura katika uchaguzi wa katikati ya muhula ambao utasaidia kutoa mwelekeo wa  hatma ya miaka miwili iliyosalia ya uongozi wa Rais Donald Trump katika muhula wake wa kwanza. 

https://p.dw.com/p/37iq8
USA Midterm Wahlen 2018 Stimmauszählung
Picha: DW/B. Karakas

Viti  435 katika Baraza la Wawakilishi pamoja na viti 35 vya Senate na 39 vya ugavana vinagombewa kwenye uchaguzi huo. Chama cha Rais Trump cha Republican kwa sasa kina viti vingi katika Senati na baraza la wawakilishi, lakini iwapo kitashindwa kudhibiti viti hivyo katika uchaguzi huu huenda hali hiyo ikachangia mkwamo wa kisiasa kwa sera za Rais Trump.

Kulingana na kura za maoni za awali, Wademocrat wana nafasi nzuri ya kudhibiti Baraza la Wawakilishi, huku WaRepublican wakitabiriwa kudhibiti uongozi wa Senati. Maafisa wa serikali wamekuwa wakifanya juhudi kwa miaka miwili kuzuia mfumo wa uchaguzi wa Marekani dhidi ya kushambuliwa na raia wa Urusi au watu wengine wanaopanga kutatiza shughuli ya upigaji kura.

Donald Trump spricht über Einwanderungspolitik
Picha: picture-alliance/S. Walsh

Upigaji kura ulioanza mapema umesababisha wasiwasi wakati vifaa vya upigaji kura na usajili wa wapiga kura nchini Marekani, kuanzia mashine zilizobadili uteuzi wa wapiga kura hadi fomu za usajili kutupwa nje kutokana na hitilafu. Maafisa wa uchaguzi pamoja na makundi ya haki wanahofia Imani ya wapiga kura katika matokeo ya uhaguzi huo wa katikati ya muhula iwapo matatizo hayo yataendelea kushuhudiwa, huku mamilioni ya Wamarekani wakijiandaa kupiga kura.

Uchaguzi wa leo ni wa kwanza  nchini Marekani tangu Urusi ilipoilenga mifumo ya uchaguzi nchini humo mwaka 2016 wakati wa uchaguzi wa rais. Maafisa wote wa uchaguzi wamesema wameweka juhudi zote kuhakikisha mifumo hiyo iko salama.

Aidha Maafisa wa Ujasusi wa Marekani, Wizara ya Usalama wa Ndani na idara nyingine za shirikisho wamefungua kituo cha kuisaidia serikali pamoja na ofisi za uchaguzi pindi linatokea  tatizo lolote kubwa katika uchaguzi huo. Kulingana na maafisa hao, kufikia sasa hakuna ishara yoyote kuwa Urusi au taifa jingine ambalo limejaribu kushambulia mifumo yake ya uchaguzi katika jimbo lolote.

USA Donald Trumps Gestik
Picha: Getty Images/AFP/J. Raedle

Katika majimbo mengine kama Kansas, maeneo ya kupigia kura yamefungwa na mengine kuunganishwa, suala lililozua wasiwasi kwamba wapiga kura watakatishwa tamaa iwapo hawatopata njia ya kufikia vituo hivyo na kupiga kura.

Katika taifa zima la Marekani, jumla ya waangalizi 6,500 wa uchaguzi wamepelekwa katika majimbo yote kuwasaidia watu watakaopata  matatizo yoyote wakati wa kupiga kura. Idadi hiyo ni zaidi ya mara mbili ya idadi ya waangalizi waliosimamia uchaguzi mwaka 2016.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/APE

Mhariri: Saumu Yusuf