Waliokufa kwenye miripuko ya Nigeria wafikia 160 | Matukio ya Afrika | DW | 22.01.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Waliokufa kwenye miripuko ya Nigeria wafikia 160

Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na mashambulizi ya mabomu yaliyofanyika katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Nigeria, Kano, Ijumaa iliyopita (20.01.2012) nchini Nigeria imepanda na kufikia 160.

Mfanyakazi wa huduma za uokozi nchini Nigeria akikagua mabaki ya magari yaliyoripuliwa mjini Kano.

Mfanyakazi wa huduma za uokozi akikagua athari za miripuko mjini Kano.

Jana (21.01.2012), mji wa kaskazini wa Kano ulikuwa hauna watu , baada ya kuwekwa amri ya kutotoka nje. Mashambulizi hayo yalilenga kiasi cha maeneo sita katika mji huo ikiwa ni pamoja na ofisi za polisi na uhamiaji pamoja na eneo la kuegesha magari jioni ya Ijumaa.

Serikali ya Nigeria inawatuhumu wanamgambo wa kundi la Boko Haram kuhusika na mashambulizi hayo. Mwezi uliopita, mtu anayesemekana kuwa msemaji wa kundi hilo, alisema kwamba kundi lake lilihusika na mashambulizi ya mabomu katika siku ya Krismasi, ambayo yalielekezwa dhidi ya makanisa. Agosti mwaka jana, jengo la makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Abuja lilishambuliwa pia kwa mabomu, na tena kundi la Boko Haram likatajwa kuhusika.

Mwandishi: Sekione Kitojo
Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza