Walimwengu waishinikiza Syria izuwie damu isimwagike | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.05.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Walimwengu waishinikiza Syria izuwie damu isimwagike

Mjumbe maalum wa kimataifa kwa Syria,Kofi Annan amemtaka rais Bashar al Assad akomeshe haraka umwagaji damu,huku Marekani na Japan zikijiunga na nchi za magharibi na kuwafukuza mabalozi wa Syria.

default

Mjumbe maalum wa kimataifa Kofi Annan (kushoto) akizungumza na rais Bashar al Assad mjini Damascus Damaskus

Damu inaendelea kumwagika nchini Syria-jana tu,wakati mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa na jumuia ya nchi za kiarabu anaendeleza juhudi za kuuokoa mpango wake wa amani,watu wasiopungua 98 wanasemekana wameuliwa-wengi wao ni raia wa kawaida.Na leo pia watu wanne wanasemekana wameuliwa kufuatia mapigano kati ya jeshi na waasi katika kitongoji cha Sitt Zeinab karibu na mji mkuu Damascus.

Kwa upande wa kidiplomasia,uamuzi wa kuwafukuza mabalozi wa Syria, unaonyesha ni wa makubaliano miongoni mwa nchi za umoja wa Ulaya,zikifuatiwa na Marekani,na serikali nyengine za dunia mfano wa Australia,Canada,Uswisi na Japan-na ni jibu la mauwaji ya awali huko Houla ambako watu wasiopungua 108 waliuliwa.

Baada ya mazungumzo pamoja na rais Bashar Al Assad jana,mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa na jumuia ya nchi za kiarabu Kofi Annan ametahadharisha akisema hali inatisha na kuongeza"Wananchi wa Syria hawataki kuwa na mustakbal wao uwe wa umwagaji damu na mgawanyiko.Hata hivyo mauwaji yanaendelea kila kukicha sawa na haki za binaadam zinavyoendelea kuvunjwa."

Syrien UN Kofi Annan Pressekonferenz in Damaskus

Mjumbe maalum wa kimataifa Kofi Annan akizungumza na waandishi habari mjini Damascus

Mwanadiplomasia hiyo wa kutoka Ghana amewaambia waandishi habari amemhimiza rais Bashar al Assad apitishe hatua madhubuti,kama anavyosema" leo na sio kesho" ili mpango wa amani wa vifungu sita uheshimiwe.

Kofi Annan amesisitiza vikosi vya serikali na makundi yote ya wanamgambo yanayoungwa mkono na serikali yanalazimika kusitisha moja kwa moja harakati zao za kijeshi .

Serikali ya Syria inashinikizwa kutoka kila pembe.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema ataitisha mkutano wa kundi la marafiki wa Syria mwezi July ujao.Amefika hadi ya kusema haondoi uwezekano wa opereshini ya kijeshi,ikiwa itaidhinishwa na baraza la usalama la Umoja wa mataifa.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ametoa mwito wa kuitishwa kikao chengine cha baraza la usalama kuzungumzia hali namna ilivyo nchini Syria.

Russland Syrien Außenminister Lawrow Muallem

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Lawrow (kulia) na Syria Muallem

Urusi na China zimeshasema hazitoachia uamuzi wowote wa kuingiliwa kijeshi Syria.

Nchi hizi mbili zimekuwa zikilaumiwa kwa kulizuwia baraza la usalama lisipitishe maazimio yaliyopendekezwa na nchi za magharibi kuilaani serikali ya mjini Damascus.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com