1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakristo waadhimisha Krismasi dunia ikitatizwa na corona

Mohammed Khelef
25 Desemba 2020

Leo ni Sikukuu ya Krismasi, ambapo waumini wa dini ya Ukristo wanaadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo, lakini maadhimisho hayo mwaka huu yametandwa na janga la virusi vya corona linalozidi kuangamiza maisha ya watu.

https://p.dw.com/p/3nCgj
Vatikan Messe Papst Franziskus
Picha: Vincenzo Pinto/Getty Images/AFP

Hata kabla ya siku yenyewe kufika, tayari kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, alishatowa tamko la kuwataka waumini wa kanisa hilo kufuata maagizo yote ya mamlaka za kidunia juu ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona. 

Kiongozi wa kiroho wa Kanisa hilo kwenye Ukingo wa Magharibi, Pierbattista Pizzaballa, ametumia ibada ya Mkesha wa Krismasi kuiombea dunia iondokane na janga hilo. 

Kiongozi huyo alilazimika kuendesha misa ya Mkesha wa Krismasi mbele ya viongozi kidini pekee mjini Bethlehem, ambako inaaminika ndiko alikozaliwa Yesu Kristo. 

Hata Rais Mahmoud Abbas wa Palestina, ambaye kawaida huhudhuria maadhimisho hayo, safari hii ameshindwa kufika kwenye Kanisa la Nativity kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2005. 

Ukingo wa Magharibi umewekwa kwenye marufuku ya kutotoka nje kuanzia saa moja usiku hadi 12 asubuhi kwa wiki kadhaa sasa, ili kukabiliana na kasi ya maambukizo ya virusi vya corona. 

Eneo hilo linalokaliwa na Wapalestina milioni 4, limeshapoteza watu 800 hadi sasa kutokana na ugonjwa wa COVID-19.

Mikusanyiko yapigwa marufuku 

Israel | Heiligabend | Weihnachtsfeier in Bethlehem
Askofu Mkuu Pierbattista Pizzaballa (katikati) akiwasiki kwenye Kanisa la Nativiy katika eneo alilozaliwa Yesu Kristo katika siku ya Mkesha wa Krismasi.Picha: Nasser Nasser/AP Photo/picture alliance

Hali ya kusherehekea Krismasi bila mikusanyiko iliyozoeleka imeshuhudiwa pia kwengineko ulimwenguni. Nchini Australia, waumini walipaswa kununuwa tiketi mtandaoni ili kuweza kushiriki misa za kanisani lakini katika hali ya kuweka masafa. 

Ufilipino, ambayo pia imekabiliwa na tetemeko la ardhi asubuhi ya leo (25 Disemba), imepiga marufuku mikusanyiko mikubwa na mikutano ya kifamilia, ambayo ni sehemu muhimu ya maadhimisho ya Mkesha wa Krismasi.

Nchini Ugiriki, ambako kawaida watoto huwa wanapita nyumba kwa nyumba kutoa mkono wa kheri ya Krismasi, shughuli hiyo muhimu kwa mila za sikukuu hii nayo imesitishwa.

Katika Mkesha wa Krismasi nchini Italia, kengele za makanisani zililia mapema kuliko kawaida. Hiyo ni kwa sababu serikali imeweka marufuku ya kutotoka nje kuanzia saa nne usiku, na kwa hivyo viongozi wa makanisa wakaifanya sherehe ya mkesha kuanza mapema badala ya usiku wa manane.

Hata ibada maalum ya Krismasi kwenye uwanja maarufu wa Mtakatifu Petro, Basilica, ilirejeshwa nyuma - badala ya saa tatu na nusu usiku ikawa saa moja na nusu magharibi.