1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wakosoaji wa Mugabe wanaandamwa

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe anaimarisha madaraka yake huku akiwakabili wakosoaji wake wakuu kwa ukatili,kabla ya kufanywa uchaguzi mkuu mwaka 2008.

Muhanga wake wa hivi karibuni ni Askofu Mkuu wa zamani wa Bulawayo wa Kanisa Kikatoliki,Pius Ncube ambae ni mkosoaji mmojawapo mkubwa wa Rais Mugabe.Ncube alijiuzulu kama askofu mkuu siku ya Jumanne kufuatia kashfa ya madai ya uzinifu. Katika mwezi wa Julai,gazeti la Herald linaloongozwa na serikali,lilichapisha picha ambazo gazeti hilo lilisema ni za askofu huyo akiwa na mke wa mtu.

Ncube aliekuwa mkuu wa dayosisi ya Bulawayo tangu mwaka 1998 amesema,amejiuzulu kwa sababu anataka kuliepusha kanisa na tuhuma zaidi na vile vile anataka nafasi ya kujitetea dhidi ya tuhuma hizo kama mtu binafsi katika mahakama.

Wachambuzi wa kisiasa nchini Zimbabwe wanasema, alichotendewa Ncube ni onyo kwa wakosoaji wote na serikali itaendelea kuwaandama.Kwani mapema mwezi huu,kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha MDC,Morgan Tsvangirai,alizuiliwa na polisi kwa muda mfupi na baadae akashtakiwa kuwa mwezi uliopita,alisababisha vurugu alipotembelea maduka ya rejareja.

Kwa maoni ya Takura Zhangazha,alie mchambuzi wa masuala ya kisiasa mjini Harare,kumshtaki Tsvangirai kufanya ghasia ni njama ya chama tawala kulipiza kisasi ziara ya juma moja iliyofanywa na Tsvangirai nchini Australia,nchi iliyo adui wa Mugabe.Hivi karibuni,Australia ilifuta viza za wanafunzi wanane wa Zimbabwe. Wazazi wa wanafunzi hao wanahusika na serikali ya Mugabe.

Jumuiya ya kimataifa ikiendelea kutoa mwito kwa viongozi wa Kiafrika kuzingatia matatizo yanayokabiliwa na raia nchini Zimbabwe ambako mfumuko wa bei umekaribia asilimia 8,000,hivi juzi Askofu Mkuu wa York nchini Uingereza,John Sentamu pia ameitaka serikali mjini London ichukue hatua.Sentamu ameeleza maoni yake katika makala ya gazeti la Observer siku ya Jumapili. Amesema,haiwezekani tena kuitazama Zimbabwe kama ni tatizo la Afrika linalohitaji suluhisho la Waafrika.Sentamu akaongezea kuwa,licha ya Rais wa Afrika ya Kusini,Thabo Mbeki kujitahidi awezavyo, ameshindwa kumshawishi Rais Mugabe kufanya mageuzi katika serikali yake katili na isiyo na usawa.Kwa maoni ya Askofu Mkuu Sentamu, Rais Mugabe alifanikiwa kupata ushirikiano wa umma kusimama kidete dhidi ya mkoloni wa zamani-lakini hatimae akaiteketeza nchi kwa hamasa za kidikteta.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com