1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi na Mabadiliko ya Tabianchi Magazetini

Oumilkheir Hamidou
11 Novemba 2016

Juhudi za kukabiliana na wimbi la wakimbizi,madhara ya mabadiliko ya tabia nchi kwa Afrika na utumwa ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa Ujerumani kuhusu Afrika mnamo muda wa siku saba zilizopita.

https://p.dw.com/p/2SXu7
Libyen Irische  Navy Rettungsoperation Flüchtlinge
Picha: picture alliance / dpa

Juhudi za kukabiliana na wimbi la wakimbizi kutoka Afrika wanaoyatia hatarini maisha yao wakiwa njiani kuja Ulaya,madhara ya mabadiliko ya tabia nchi kwa Afrika na utumwa ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika mnamo muda wa siku saba zilizopita.

Tunaanza lakini na mada kuu magazetini: Wimbi la wakimbizi na namna ya kukabiliana nalo. Misaada zaidi kwa nchi wakimbizi wanakotokea,hatua za kuwarejesha makwao mara wanapookolewa na makadirio ya uhamiaji wa siku za mbele-yote hayo ni miongoni mwa yaliyochambuliwa na magazeti ya Ujerumani kuhusu mada ya wakimbizi na namna ya kukabiliana nao. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linazungumzia mipango ya wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ujerumani ya kutenga fedha zaidi kusaidia kupunguza kishindo kinachosababishwa na wakimbizi kutoka mashariki ya kati na Afrika.

Euro bilioni moja na nukta mbili zitatolewa mwaka unaokuja kama misaada ya dharura ya kiutu. Hayo,linaandika gazeti la Frankfuret Allgemeine yametajwa katika ripoti ya kurasa 365 iliyowasilishwa mbele ya kamati ya bajeti ya bunge la shirikisho Bundestag. Sehemu ya fedha hizo itatumika kujikinga dhidi ya mizozo,kuimarisha amani na kuzuwia wimbi la wakimbizi. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema bajeti ya wizara ya misaada ya maendeleo pia itazidishwa kwa Euro 550 milioni na sehemu ya fedha hizo itagharimia miradi ya maendeleo ili kupunguza kishindo cha wakimbizi.

Wakimbizi warejeshwe walikotokea wakiokolewa

Gazeti la Die Welt kwa upande wake linazungumzia kuhusu dhamiri za wizara ya mambo ya ndani inayopendelea wakimbizi wakiokolewa wasiachiwe kuutia mguu wao Ulaya,warejeshwe kule kule walikotokea. Bahari ya kati imegeuka kuwa njia hatari zaidi kwa wakimbizi wanaotaka kuja Ulaya. Kwa mujibu wa shirika la wahamiaji la kimataifa watu karibu 250 wamezama pekee mnamo siku za mwanzo huu wa November. Jumla ya watu 4000 watakuwa wamepoteza maisha yao katika bahari ya kati mnamo mwaka huu wa 2016. Ndio maana linasema gazeti la Die Welt wizara ya mambo ya ndani inafikiria uwezekano wa kupelekwa Afrika kaskazini wakimbizi watakaookolewa na kutoka huko,watume maombi ya ukimbizi,na yakikubaliwa ndipo watakaposafirishwa na kuletwa Ulaya.

Wizara ya mambo ya ndani inaamini mpango huo utawatisha wakimbizi na hawatoyatia tena maisha yao hatarini. Hata hivyo die Welt linainukuu wizara ya mambo ya ndani ikizungumzia "ugumu" wa kutekelezwa mpango huo kisheria kuambatana na makubaliano ya kuheshimu haki za binaadam.

Africa yaathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi

Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi unaendelea katika mji wa Moroko-Marakesh. Gazeti la Neues Deutschland linaandika kuhusu madhara makubwa ya mabadiliko ya tabia nchi yanayoliathiri zaidi bara la Afrika. Neues Deutschland limezitaja Msumbiji na Malawi kuwa nchi zinazosumbuliwa zaidi kwa kunukuu faharasa ya athari ya mabadiliko ya tabianchi kwa mwaka 2015. Mwishoni mwa mwaka 2014 watu milioni 24,wakaazi wa kusini mashariki mwa Afrika walisumbuliwa na ukame kwasababu mvua za masika hazikunyesha kama ilivyotarajiwa. Badala yake zilinyesha mwezi wa desemba kwa nguvu na kwa muda mrefu na kusababisha mafuriko huku malaki wakilazimika kuyapa kisogo maskani yao.

Msimu wa kiangazi mwaka 2015 ukame  mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 1980 ukapiga tena-wamsumbiji wengi wakalazimika kuuza kwa pupa mifugo yao,mbuzi,ng'ombe na kuku. Takriban kila familia moja kati ya tatu hawakuwa wakijua chakula watakipata wapi. Hakuna nchi yoyote ya dunia hii iliyoathirika vibaya zaidi na ukame mwaka jana kama Msumbiji-limeandika gazeti la Neues Deutchland lililonukuu ripoti ya shirika la ulinzi wa mazingira la Ujerumani iliyofikishwa katika mkutano wa mabadiliko ya tabianchi mjini Marakesh nchini Moroko. Mbali na Msumbiji,Malawi pia imeathirika vibaya sana na mabadiliko ya tabianchi,malaki wamevunjikiwa na nyumba zao kutokana na mafuriko,limemaliza kuandika Neues Deutschland lililozitaja pia Ghana na Madagascar kuwa miongoni mwa nchi za Afrika zilizoathirika vibaya pia na mabadiliko ya tabia nchi.

Utumwa mambo leo barani Afrika

Lilikuwa gazeti hilo hilo la Neues Deutschland lililomulika balaa la utumwa katika baadhi ya nchi za Afrika."Utumwa bado haujatoweka" ndio kichwa cha maneno cha gazeti hilo linalosema zaidi ya asili mia 80 ya nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara zimeorodheshwa katika kundi hatari linaloendeleza utumwa mamboleo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/Presse

Mhariri:Yusuf Saumu