1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakaguzi wa OSCE waachiwa huru

3 Mei 2014

Wakaguzi saba wa Shirika la Ushirikiano na Usalama (OSCE) wameachiliwa huru Jumamosi (03.05.2014) katika mji wa Slaviansk mashariki ya Ukraine ambapo waasi wanaoiunga mkono Urusi waliozingirwa wanapambana na jeshi.

https://p.dw.com/p/1BtJl
Wakaguzi wa OSCE baada ya kuachiliwa huru Slaviansk.
Wakaguzi wa OSCE baada ya kuachiliwa huru Slaviansk.Picha: picture-alliance/dpa

Kuachiliwa kwao huko kusikotarajiwa ni habari njema kwa nchi hiyo yenye kutumbukia kwa haraka kwenye machafuko baada ya kutwa moja ya uwamgaji damu ambapo watu zaidi ya hamsini waliuwawa wengi kutokana na moto wa kutisha katika mji wa kusini wa Odessa.

Katika viunga vya mji wa Sloviansk ambapo wakaguzi hao wa OSCE walikuwa wakishikiliwa, waandishi wa AFP wameshuhudia mapigano makali ya silaha kati ya waasi waliokuwa na bunduki za Kalashnikov na wanajeshi waliokuwa wamevizingira vituo vyao vya ukaguzi.

Magari ya deraya mara kwa mara yamekuwa yakifyatuwa risasi za bunduki dhidi ya waasi hao waliokuwa wamezidiwa nguvu. Ukraine nzima ilikuwa kwenye fadhaa leo hii kufuatia habari za vifo vya watu 42 hapo jana katika mji wa kusini wa Odessa ambapo wanamgambo wanaoiunga mkono na Urusi na wale wanaoiunga mkono Ukraine walipokuwa kwenye jengo la chama cha wafanya biashara lililowaka moto wakati pande hizo mbili zilipokuwa zikirushiana mabomu ya petroli.

Mzozo wapamba moto

Kuripuka ghafla kwa ghasia hizo kumeufanya mvutano wa kimataifa kati ya mahasimu wa zamani wa Vita Baridi Marekani na Urusi kuzidi kupamba moto. Marekani inasema iko kwenye hatua za mwisho kutangaza vikwazo dhidi ya Urusi ambavyo vitazidi kuuvuruga uchumi wa Urusi ambao tayari ni dhaifu iwapo uingiliaji kati wa nchi hiyo utakwamisha uchaguzi wa rais wa Mei 25 ambao unaonekana kuwa muhimu katika kuleta utulivu nchini Ukraine.

Mmojawapo wa wakagauzi wa OSCE aliyeachiliwa huru (kushoto).
Mmojawapo wa wakagauzi wa OSCE aliyeachiliwa huru (kushoto).Picha: Reuters

Lakini serikali ya Urusi inasema utakuwa ni upuuzi hivi sasa kuendelea kufanya uchaguzi huo na kuongeza kwamba nchi hiyo imepoteza ushawishi wake kwa wanamgambo hao wenye silaha wanaoiunga mkono Urusi. Rais Vladimir Putin wa Urusi ambaye mataifa ya magharibi yanamuona kuwa ndie anayepanga uasi wa Ukraine licha ya yeye mwenyewe kukanusha ameweka wanajeshi wake wanaokadiriwa kufikia 40,000 kwenye mpaka na Ukraine kwa miezi miwili sasa, kwa maandalizi ya uvamizi ambayo amesema anataraji sana hatalazimika kuyaamuru.

Serikali ya Urusi inadai waasi ni "waandamanaji" ambao wameunda vikosi vya kujihami wenyewe na kupinga shutuma kwamba jeshi la Urusi na makamanda wake wa ujasusi wanawaongoza waasi hao. Hata hivyo wakaguzi wa OSCE ambao wamekuwa wakishikiliwa katika mji wa Slaviansk kwa zaidi ya wiki moja ,waliachiliwa muda mfupi baada ya mjumbe wa serikali ya Urusi kuwasili mashariki ya Ukraine. Wakaguzi hao hawakuweza kuondoka kwenye mji huo mara moja kutokana na mapigano.

Katu sitowasamehe

Vladimir Lukin kamishna wa haki za binaadamu wa Urusi amesema leo hii kwamba amefanikisha kuachiliwa huru kwa kwa watu walio kwenye orodha yake. Lukin amekaririwa akisema na vyombo vya habari vya Urusi kwamba hilo lilikuwa ni tendo la nia njema la kibinaadamu na kwamba wanawashukuru watawala wa mji huo. Amesema hakuna mabadilishano yoyote yaliohusishwa lakini anataraji hatua hiyo itapelekea kusitishwa kwa mapigano ya risasi katika mji huo.

Mmojawapo wa wakagauzi wa OSCE aliyeachiliwa huru.
Mmojawapo wa wakagauzi wa OSCE aliyeachiliwa huru.Picha: picture-alliance/dpa

Hata hivyo wakaguzi hao wa Ulaya wana machungu kwa watekaji wao waliokuwa wakiwashikilia mateka ambao kuna wakati waliwapaleka kuzungumza na waandishi wa habari chini ya mtutu wa budukí. Mmojawapo wa wakaguzi wa OSCE aliyeachiliwa huru amewaambia waandishi wa habari "Katu sitawasamehe".

Hapo jana Urusi iliitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo imeilaumu serikali ya Ukraine inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi ambayo inaiona kuwa sio halali kwa kuhusika na machafuko nchini humo. Msemaji wa Putin leo hii amesema serikali ya Urusi imekuwa ikipokea " maelfu ya wito" kutoka mashariki ya Ukraine ikitaka msaada wa vitendo. Dmitry Peskov ameliambia shirika la habari la taifa RIA Novosti kwamba Putin " ana wasi wasi mkubwa sana kwa jinsi hali hiyo inavyoendelea ".

Umwagaji damu ulioanza tokea Ijumaa ni mbaya kabisa kuwahi kuikabili serikali ya Ukraine tokea ichukuwe madaraka mwishoni mwa mwezi wa Februari baada ya maandamano ya mitaani ya miezi kadhaa kulazimisha kuondolewa kwa rais Viktor Yanukovych aliekuwa na urafiki na Urusi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ AFP

Mhariri: Bruce Amani