Wajerumani wataka Deutschmark irudi | Magazetini | DW | 05.10.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Wajerumani wataka Deutschmark irudi

Bado suala la sarafu ya Euro linaendelea kutawala maoni ya wahariri, huku matokeo ya utafiti mpya yakionesha kuwa idadi kubwa ya Wajerumani wa kawaida hawataki tena sarafu ya euro bali sarafu yao ya zamani, Deutschmark.

Noti ya D-Mark 100

Noti ya D-Mark 100

Gazeti la Hamburger Abendblatt linanukuu matokeo ya utafiti wa taasisi ya Gruner+Jahr, ambayo yanaonesha kuwa asilimia 54 ya Wajerumani wangelipendelea kurudi kwa sarafu hiyo ya Deutschmark. Sababu ni kuwa, wamevunjwa moyo na mgogoro wa kifedha, unaoyakumba mataifa yanayotumia sarafu ya Euro, ikiwemo Ujerumani yenyewe.

Tena mhariri huyo anasema kwamba, watu wa mashariki ya Ujerumani, ndio hasa hawataki tena kubakia kwenye kanda ya euro, maana huko ni asilimia 67 waliotaka kurudi kwenye Deutschmark. Lakini si peke yao. Asilimia 73 ya wanafunzi wa sekondari ya kati na asilimia 37 ya wanafunzi wa sekondari ya juu waliiradua Deutschmark mbele ya Euro.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle.

Kwenye suala hilo hilo la sarafu ya Euro, gazeti la Rheinishe Post linazungumzia msimamo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, kwamba Ulaya sasa inahitaji mkataba mwengine wa kifedha na kiuchumi, ikiwa kweli inahitaji kupambana na tatizo la madeni kwenye kanda ya euro.

"Mkataba wa ule wa kwanza ulikuwa mzuri kwa miaka ya 1990, na Ulaya ilipiga hatua kubwa kupitia mkataba huo. Lakini kumekuwepo na changamoto mpya. Na sasa tunahitaji Mkataba namba mbili." Ndivyo alivyonukuliwa Westerwelle na gazeti hilo akizungumza kutokea mjini Düsseldorf.

Westerwelle ameendelea kusema kwamba, Ulaya inahitaji kutafuta njia mbadala kwa ajili ya kuwa na umoja ulio makini na wenye utulivu wa kifedha. Mhariri anasema kwamba, kwa kauli hii ya Westerwelle, mataifa 27 yaliyomo kwenye Umoja wa Ulaya bado yana tafauti nyingi baina yao, kuliko vile ilivyokuwa ikiaminika.

Mwalimu Tatjana Çukari na wanafunzi wake.

Mwalimu Tatjana Çukari na wanafunzi wake.

Na katika matokeo mengine ya utafiti, ambayo yamechapishwa na gazeti la Oldenburgische Volkszeitung, kazi ya ualimu haina mvuto. Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na taasisi ya DAK, ualimu ni kazi isiyopendelewa kabisa na watu.

Mhariri anaipa kazi hii ya ualimu majina mawili: kazi mbovu, kazi yenye fadhaa kubwa. Zaidi ya nusu ya walimu wanaendelea kufanya kazi hiyo wakiwa na malalamiko chungu nzima. Wengi wao wanatamani muda wao wa kustaafu ufike. Na hili si jambo geni, anaendelea mhariri huyo, kwani kama alivyowahi kusema aliyekuwa Kansela wa Ujerumani, Gerhard Schröder, ualimu ni kapu la kutupia mabovu yote.

Bila ya shaka si kwa kuwa ualimu ni kazi mbaya, lakini kwa kuwa linafanywa kimbilio la mwisho. Kijana aliyeshindwa kufanya vyema kwenye masomo yake, hukimbilia ualimu si kwa kuwa anaupenda, bali kwa kuwa hana njia nyengine ya kuishi.

Matokeo yake, ni kuwa kazi ya ualimu inaonekana kazi inayomkaribisha mtu haraka kwenye kuchanganyikiwa, na kupoteza malengo.

Vyanzo: Hamburger Abendblatt, Rheinishe Post, Oldenburgische Volkszeitung
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo

 • Tarehe 05.10.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12lqI
 • Tarehe 05.10.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12lqI