1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waisraeli waamua katika Uchaguzi

22 Januari 2013

Waisraeli wamepiga kura leo Jumanne katika uchaguzi unaotarajiwa kumpa ushindi wa kubakia katika muhula wa tatu waziri mkuu Benjamin Netanyahu,

https://p.dw.com/p/17PNY
Mwanajeshi wa Israeli akipiga kura yake katika kambi ya jeshi,kusini mwa nchi
Mwanajeshi wa Israeli akipiga kura yake katika kambi ya jeshi,kusini mwa nchiPicha: Reuters

Ushindi wa Netanyahu utafungua njia ya mapambano na Iran na kuongeza nguvu katika kambi inayopinga kuweko dola la Wapalestina.

Kura za maoni zilizofanywa kabla ya uchaguzi wa leo zimeonyesha kwamba chama cha waziri mkuu Netanyahu cha Likud kinachosimama sambamba na Chama cha Yisreal Beitenu kinajiandaa kushinda uchaguzi huu lakini kwa viti vichache bungeni ikilinganishwa na viti ilivyokuwa inashikilia katika bunge lililopita huku uungaji mkono ukiongezeka zaidi kuelekea mrengo wa kulia wa chama cha wahafidhina cha wayahudi (Jewish Home Party).

Muungano unaotarajiwa

Duru za kisiasi zinasema Netanyahu aliyeingiwa na wasiwasi juu ya kupwaya kwa umaarufu wake huenda akajiegemeza na vyama vya mrengo wa siasa za wastani baada ya uchaguzi huu ikiwa ni katika juhudi za kuupanua muungano wake na kuionyesha Marekani na washirika wake wengine kwamba imepata serikali ya watu wenye siasa za wastani.

Waziri mkuu Benjamin Netanjahu
Waziri mkuu Benjamin NetanjahuPicha: dapd

Akipiga kura mapema hii leo, Netanyahu amesema na hapa tunanukuu ''Tunataka Israel ifaulu, tunapiga kura kukichagua chama cha Likud na Beitenu, kadri muungano huu unavyokuwa mkubwa ndivyo Israel itakavyofanikiwa zaidi,'' mwisho wa kunukuu.

Kiasi waisraeli milioni 5.66 wana haki ya kupiga kura katika uchaguzi ambao umeshuhudia vituo vya kupiga kura vikifunguliwa tangu saa 10 asubuhi. Matokeo kamili ya uchaguzi huo wa bunge yanatarajiwa kutolewa kesho asubuhi na kufungua njia ya kufanyika mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto ambayo huenda yakachukua muda wa wiki kadhaa.

Idadi kubwa yajitokeza

Hadi kufikia mchana wa leo kamati ya uchaguzi nchini Israeli ilisema idadi ya waliojitokeza kupiga kura ilifikia asilimia 38.3 ikiwa ni kubwa zaidi ikilinganishwa na iliyoshuhudiwa wakati kama huo katika chaguzi za mwaka 2009 na pia ni kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 1999.

Naftali Bennett kiongozi wa chama cha kihafidhina cha
Naftali Bennett kiongozi wa chama cha kihafidhina chaPicha: Reuters

Kabla ya uchaguzi wachambuzi walibashiri kwamba ikiwa idadi ya wapiga kura itakuwa kubwa basi vyama vinavyotegemewa kunufaika na hilo ni vya mrengo wa kushoto ambavyo baadhi ya wakati vimekuwa vikijizatiti kuwashawishi wapiga kura wao. Hakuna chama kilichowahi kupata wingi mkubwa wa viti vinavyohitajika bungeni kuweza kuongoza bila kushirikiana hii ina maana kwamba Netanyahu ambaye anasema kulishughulikia suala la Iran ni ajenda yake muhimu atalazimika kuwa katika serikali ya mseto na vyama mbali mbali kuweza kulihodhi bunge la Knesset lenye viti 120.

Chama kikuu cha upinzani cha Labour ambacho kinatazamiwa kujinyakualia zaidi ya viti 17 kimeshaondowa uwezekano wa kurudia kilichofanyika mwaka 2009 wakati kilipoingia katika serikali ya muungano na Netanyahu kwa ahadi ya kuyapa nguvu mashauriano ya amani na Wapalestina. Mazungumzo hayo yaliyosiamamiwa na Marekani yalivunjika miezi michache baada ya kuanza mwaka 2010 kufuatia mvutano juu ya suala la ujenzi wa makaazi ya walowezi.

Mwandishi Saumu Yusuf

Mhariri:Josephat Charo