1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wairan kuamua nani zaidi

12 Juni 2009

Nchi za magharibi zinafuatilia kwa karibu uchaguzi huo

https://p.dw.com/p/I7zP
Mahmoud Ahmadinejad na Hossein MousaviPicha: picture alliance / abaca / dpa

Wairan wamejitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la kupiga kura katika uchaguzi wa rais unaofanyika hii leo. Mamia ya wapiga kura wamepiga foleni ndefu tangu asubuhi katika vituo mbali mbali vya kupigia kura wakati zoezi hilo lilipoanza.Taarifa zinasema Katika vituo vikubwa kwenye mji mkuu, Tehran, maelfu ya watu wamemiminika kuchagua kati ya wagombea wa urais kwenye uchaguzi huo unaofuatiliwa kwa karibu na nchi nyingi za magharibi. Mpambano mkali ni kati ya rais wa sasa, Mahmoud AhmedNejad, na Mir Hossein Mousavi, waziri mkuu wa zamani nchini humo.Wairan millioni 46.2 wana haki ya kupiga kura.

Ni uchaguzi uliojaa hamasa nyingi miongoni mwa wafuasi wa kila upande, hali ambayo ilijitokeza tangu mwanzo wakati wa Kampeini kati ya pande mbili kuu zinazopingana. Mpambano mkali upo kati ya waziri mkuu wa zamani, Mir Hossein Mousavi, ukiwakusanya wapiga kura wenye msimamo wa wastani dhidi ya wenye msimamo mkali wanaomuegemea rais wa sasa, MahmoudAhmedinejad.

Asubuhi hii Kiongozi mkuu wa Iran, Ali Khamenei, alikuwa mtu wa kwanza kupiga kura na alitoa mwito kwa Wairani kujitokeza kwa wingi kushiriki, akisema ni wajibu wa kila Muislamu.

''Ningependa kuwaambia watu wa Iran kushiriki katika uchaguzi.Nawaambia wapige kura kwa misingi ya mitazamo na uamuzi wao.Hii itakuwa na mchango katika utawala wa nchi yao na kuchangia katika kumchagua kiongozi wa juu serikali na pia hii ni haki yao na wajibu.Ni haki ya kila mmoja kutoka tabaka mbali mbali kutoa maoni yake na kwa mtazamo wangu hii ni haki ya kimsingi na kidini''

Rais Mahmoud Ahmedinejad na Mir Hossen Mousavi pia wameshapiga kura zao.Spika wa zamani wa bunge, Ali Akbar Nateq Nouri, pia ni miongoni mwa watu wa mwanzo kupiga kura asubuhi hii katika kituo cha kihistoria cha kupiga kura mjini Tehran cha Ershad, na ameliambia shirika la habari la AFP kwamba idadi ya waliojitokeza ni kubwa sana, ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Kabla hata ya kuanza zoezi la kupiga kura mapema hii leo. Mgombea wa Urais, Mir Hossein Mousavi, alionya dhidi ya kuingiliwa kwa shughuli hizo na jeshi la ulinzi la mapinduzi ya Kislamu pamoja na wanamgambo wa Basij na kutaka pia kulindwa kura za wananchi wanaofanya maamuzi. Moussavi ameyafikisha madai yake hayo kwa kiongozi wa juu wa nchi hiyo, Ayatollah Ali Khamenei, akisema kwamba kuna ushahidi wa baadhi ya makamanda na maafisa wa Basij na jeshi la ulinzi kutatiza uchaguzi huo, madai ambayo yametiwa pia katika tovuti yake ya kampeini.

Katika madai hayo inaarifiwa kwamba kuna uwezekano wa kura za watu kubadilishwa, hatua ambayo inakiuka sheria. Aidha mpinzani huyo mkuu wa rais AhmedNejad amesema kwamba uwezekano huo wa kutokea mizengwe unawatia wasiwasi wapiga kura kwa sababu hawajui ni kwa kiasi gani vitendo hivyo haramu vitafanyika na pia ikiwa baadhi ya maafisa wanaosimamia vituo vya kupiga kura pamoja na waangalizi wamechaguliwa miongoni mwa wafuasi wa wagombea fulani.

Hata hivyo, jeshi la ulinzi la mapinduzi limeyakanusha madai hayo, likisema hayana msingi na pia kumuonya Mousavi kwamba madai yake hayatapuuzwa na kwamba inabidi awasilishe ushahidi wa madai hao haraka iwezekanavyo, vinginevyo aombe msamaha kwa wananchi,j eshi la ulinzi pamoja na kikosi cha Basij.

Wakati huo huo, mgombea mwingine Mwanamageuzi, Mehdi Karroubi, ambaye pia aligombea mwaka 2005 ambapo Mahmoud Ahmedinejad aliingia madarakani, amelaumu kwamba kushindwa kwake kulisababishwa na kile alichokiita hatua haramu ya kuingilia kati shughuli za uchaguzi, jeshi la mapinduzi pamoja na wanamgambo wa Basij. Pia upande wake ameiomba serikali na kiongozi wa juu, Ayatollah Ali Khamenei, kuhakikisha tukio kama hilo halijirudii katika uchaguzi huu.

Mpaka sasa wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa wanaonekana kushindwa kubashiri mshindi katika uchaguzi, huku wengi wakisema pengine matokeo yanaweza kuwa kama ya mwaka 2005 wakati Ahmedinejad ambaye wakati huwa alikuwa mtu asiyetambulika sana aliibuka na ushindi baada ya uchaguzi kuingia katika duru ya pili dhidi ya kigogo kiongozi wa kidini, Akbar Hashemi Rafsanjani.

Mshindi anabidi kupata wingi wa asilimia 50 ya kura. Matokeo ya mwanzo ya uchaguzi huo wa urais yanatarajiwa hapo kesho, na ikiwa hakutapatikana mshindi wa wazi duru ya pili itafanyika tarehe 19 mwezi huu kati ya wagombea wawili wa mwanzo.

Mwandishi.Saumu Mwasimba/AFP/RTE

Mhariri Othman Miraji