1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahouthi wawekewa vikwazo

15 Aprili 2015

Wakati mataifa yenye nguvu duniani yakiungana dhidi ya waasi wa Kihouthi nchini Yemen kwa kuwawekea vikwazo vya Umoja wa Mataifa ,Saudi Arabia na Misri zinafikiria kuwa na luteka ya pamoja ya kijeshi.

https://p.dw.com/p/1F8jA
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.(14.04.2015)
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.(14.04.2015)Picha: REUTERS/L. Jackson

Azimio hilo lililopigiwa kura na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuja baada ya Iran ambayo inatuhumiwa kuwaunga mkono waasi hao wa Kihouthi kupendekeza usitishaji wa mapigano utakaofuatiwa na na mazungumzo ya upatanishi yatakayosimamiwa na mataifa ya kigeni.

Uasi huo wa Wahouthi umemlazimisha Rais Abedraboo Mansour Hadi kuikimbia nchi yake hiyo maskini kabisa ya Kiarabu na kutishia kuzuka kwa janga kubwa la kibinaadamu.

Mzozo huo pia umezidi kupalilia hali ya mvutano katika eneo zima la Mashariki ya Kati huku Saudi Arabia ikiishutumu Iran kwa kuuchochea uasi huo wa Wahouthi.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limechukuwa hatua ya kukabiliana na hali hiyo kwa kuwawekea vikwazo vya silaha waasi hao wa Kihouthi na kuwataka wapiganaji wao wandoke katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa.

Marekani yaongeza shinikizo

Azimio hilo limewajumuisha kwenye orodha ya vikwazo kiongozi wa Wahouthi Abdul Malik al Huthi na Ahmed mtoto wa kwanza wa kiume wa Rais wa zamani wa Yemen Ali Abdullah Saleh. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power ameunga mkono kikamilifu vikwazo hivyo wakati azimio hilo lilipopitishwa hapo Jumanne (14.04.2015) na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York.

Waasi wa Kihouthi nchini Yemen.
Waasi wa Kihouthi nchini Yemen.Picha: picture-alliance/dpa

Power amekaririwa akisema "Marekani inaunga mkono kwa nguvu zote kupitishwa kwa azimio hilo leo hii na kuwawekea hatua kali Wahouthi na rais Sale wa zamani na kutaka Wahouthi wasitishe operesheni zao za kijeshi na kuzitaka pande zote mbili kwa mara nyengine tena kurudi kwenye meza ya mazungumzo."

Urusi mshirika wa Iran haikushiriki katika kulipigia kura azimio hilo lakini haukulipinga kwa kura ya turufu.

Luteka za kijeshi

Wakati huo huo ofisi ya Rais Abdel Fatha al Sisi wa Misri imesema kwamba Misri na Saudi Arabia zinafikiria kufanya leteka ya pamoja ya kijeshi ambayo pia itazishirikisha nchi nyengine za Kiarabu.

Mwanajeshi wa Saudi Arabia mpakani na Yemen.
Mwanajeshi wa Saudi Arabia mpakani na Yemen.Picha: Reuters/F. Al Nasser

Taarifa hiyo iliyotolewa jana usiku wa manane baada ya Rais Sisi kukutana na waziri wa ulinzi wa Saudi Arabia Mwana Mfalme Mohammed bin Salman imesema imeamuliwa kuundwa kwa kamati ya pamoja ya kijeshi kuangalia uwezekano wa kufanya luteka kubwa za kijeshi katika ardhi ya Saudi Arabia.

Taarifa hiyo haikutowa ufafanuzi zaidi lakini afisa mmoja wa usalama amekaririwa akisema luteka hizo yatakuwa mazoezi ya kijeshi ya kiwango kikubwa sana.

Vikosi vya majini na vya anga vya Misri vinashiriki katika mashambulizi yanayoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi wa Kihouthi nchini Yemen na serikali ya Misri imeahidi kupeleka vikosi vya aradhini itakapobidi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ Reuters/AFP

Mhariri :Gakuba Daniel