1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahouthi wasonga mbele Aden

5 Aprili 2015

Waasi wa Kihouthi wapata ushindi mpya katika medani ya mapambano kwenye mji wa kusini wa Aden Jumapili (Aprili 5) wakati ushirika unaoongozwa na Saudi Arabia ukijaribu kuzuwiya kusonga mbele kwao.

https://p.dw.com/p/1F2zi
Waasi wa Kihouthi wakiwa katika mitaa ya mji wa Aden.
Waasi wa Kihouthi wakiwa katika mitaa ya mji wa Aden.Picha: picture-alliance/AP Photo/Wael Qubady

Waasi wa Kihouthi wapata ushindi mpya katika medani ya mapambano kwenye mji wa kusini wa Aden Jumapili (Aprili 5) wakati ushirika unaoongozwa na Saudi Arabia ukijaribu kuzuwiya kusonga mbele kwao.

Chama cha Msalaba Mwekundu kimeeleza kwamba hali ni mbaya sana na kimetowa wito wa kusitishwa mapigano mara moja ili kuziruhusu familia kutafuta maji,chakula na msaada wa matibabu.

Urusi imewasilisha rasimu ya azimio kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo Jumamosi lenye kutowa wito wa kusitishwa kwa mashambulizi ya anga yanayoongozwa na Wasaudi dhidi ya waasi wa Kishia wa jamii ya Wahouthi ambayo yameingia siku ya kumi na moja.

Ushirika huo umeendelea na mashambulizi yao ya usiku dhidi ya maeneo yanayoshikiliwa na waasi na bohari za silaha hususan karibu na mji mkuu wa Sanaa na Saada ambayo ni ngome kuu ya waasi ilioko kaskazini mwa Yemen.

Waasi wasonga mbele

Katika mji mkubwa wa kusini wa Aden waasi wamesonga mbele na kuingia wilaya ya kati wa Mualla ambapo wameteka makao makuu ya serikali ya jimbo.Mashahidi wamesema wameripua kwa mabomu maeneo ya wakaazi, kuyatia moto majengo kadhaa na kuyaharibu mengine.

Wanamgambo wanaomuunga mkono Rais Hadi mjini Aden.
Wanamgambo wanaomuunga mkono Rais Hadi mjini Aden.Picha: Getty Images

Wakaazi wameripoti kutokea kwa maafa na kusema kwamba familia nyingi zimekimbia nyumba zao katika mji huo wa bandari.Takriban watu 185 imeripotiwa kuuwawa katika mapigano ya Aden kati ya wafuasi wanaomunga mkono Rais Hadi na wale wanaompinga.

Vikosi hivyo vya waasi vilikuwa pia vimeikaribia bandari ya Mualla ambayo inalindwa na wanamgambo walio tiifu kwa Rais Abedrabbo Mansour Hadi ambaye amekimbilia nchi jirani ya Saudi Arabia.

Hali mbaya sana

Kwa mujibu wa chama cha Msalaba Mwekundu hospitali zenye kuwatibu majeruhi zinaishiwa na madawa na mitaa ya Aden imetapakaa miili ya watu waliopoteza maisha yao.

Wanamaji wa Kichina wakiagana na manowari iliokwemda Aden kuwaokowa raia wake na raia wengine wa kigeni.
Wanamaji wa Kichina wakiagana na manowari iliokwemda Aden kuwaokowa raia wake na raia wengine wa kigeni.Picha: Reuters

Robert Mardin mkuu wa operesheni wa Kamati ya Kimataifa ya chama cha Msalaba Mwekundu kwa Mashariki ya Kati amesema lazima wafanyakazi wao wa upasuaji na misaada yao ya dharura iruhusiwe kuingia nchini humo na kufika kwenye maeneo yalioathirika zaidi ili kutowa msaada.

Amekaririwa akisema "venginevyo watu wengi zaidi watakufa na kwa wale waliojeruhiwa nafasi ya kuweza kunusurika itategemea kuchukuliwa hatua kwa haraka isio zaidi masaa na sio siku."

Ushirika wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia unaozijumuisha nchi nyengine nne za Ghuba pamoja na Misri,Jordan, Morocco na Sudan umesema wafanyakazi hao wataruhusiwa kuingia nchini humo wakati hali itakaporuhusu.

Wahouthi tayari kwa mazungumzo

Habari zinasema waasi wa Kihouthi wako tayari kukaa chini kwa mazungumzo ya amani mara tu mashambulizi ya anga ya ushirika unaoongozwa na Saudi Arabia yatakapositishwa na mazungumzo hayo kusimamiwa na makundi yasiohusika na kile ilichokiita uvamizi wa nchi hiyo.

Maadamano dhidi ya Wahouthi katika mji wa kusini wa Taiz.
Maadamano dhidi ya Wahouthi katika mji wa kusini wa Taiz.Picha: Reuters/Anees Mahyoub

Saleh al - Sammad ambaye alikuwa mshauri wa Rais Hadi ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters katika majibu ya baruwa pepe kwamba wananchi wa Yemen wanakataa kurudi kwa Hadi nchini humo ambaye amekimbilia Saudi Arabia mwezi uliopita wakati wapiganaji wa Kihouthi walipokuwa wakiukaribia mji wa Aden ulioko kusini ambao ulikuwa makao yake.

Sammad amesema wanaendelea kushikilia msimamo wao katika mazungumzo hayo na kutaka yaendelee licha ya yote yale yaliyotokea chini ya msingi wa heshima na kila mmoja kukiri kumtambuwa mwenzake.

Ameongeza kusema kwamba anataka vikao vya mazungumzo hayo vionyeshwe kwa wananchi wa Yemen ili waweze kujuwa ni nani mkwamishaji.

Athari za machafuko

Ndege na meli za kivita kutoka kwa ushirika unaoongozwa na Saudi Arabia zimekuwa zikiwashambulia waasi wa Kihouthi kwa siku ya 11 mfululizo kwa kusema kwamba umekuwa ukijaribu kuwarudisha nyuma waasi hao wa Kishia na kumrudisha madarakani Hadi.Mazungumzo ya amani yaliosimamiwa na Umoja wa Mataifa kati ya Hadi na Wahouthi yaliofanyika huko nyuma yameshindwa.

Vifusi vya nyumba kufuatia mashambulizi ya anga mjini Sanaa.
Vifusi vya nyumba kufuatia mashambulizi ya anga mjini Sanaa.Picha: Reuters/K. Abdullah

Mfalme Salman wa Saudi Arabia alikaririwa akisema hapo Jumatatu kwamba nchi yake iko tayari kwa mkutano wa kisiasa kati ya makundi ya Yemen chini ya usimamizi wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba (GCC) ambapo nchi tano wanachama wa baraza hilo zinashiriki katika muungano wa kijeshi dhidi ya Wahouthi.

Machafuko hayo yanazusha hofu kwamba nchi hiyo ya kimaskini ya Yemen inaweza kusambaratishwa kutokana na vita vya mawakala kati ya Saudi Arabia taifa la Kisuni lenye nguvu Mashariki ya Kati na Iran taifa kubwa la Kishia.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri : Bruce Amani