1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wasisitiza ubanaji matumizi uende sambamba na kuleta ustawi

Abdu Said Mtullya23 Mei 2012

Wahariri wa magazeti wanazungumzia juu ya mkutano wa kilele wa viongozi wa Ulaya na juu ya ripoti ya Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo OECD.

https://p.dw.com/p/150Td
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Francois Hollande
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Francois Hollande.Picha: ap

Viongozi wa nchi 27 za Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels ili kujaribu kutafuta njia za kuepusha mgogoro wa madeni kwenda kombo zaidi, sambamba na kuendeleza juhudi za kuleta ustawi wa uchumi na kutenga nafasi za ajira.

Juu ya mkutano huo gazeti la "Neue Osnabrücker" linakumbusha kwamba sera ya pupa ya kuleta ustawi umeipeleka dunia hadi kwenye ukingo wa maafa.

Mhariri huyo anasema kuleta ustawi hala kulihali ni kosa kubwa.Kinachotakiwa sasa ni uchumi endelevu badala ya kukopa zaidi au kupandisha kodi.

Mhariri wa gazeti la"Badische Zeitung" pia anazungumzia juu ya pande mbili za hoja juu ya kuutatua mgogoro wa madeni barani Ulaya.Lakini anaizingatia ripoti ya Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, OECD. Anasema miito inayotolewa ya kuwataka watu katika nchi za kusini mwa Ulaya waendelee kukaza roho ili kubana matumizi,inakataliwa na watu wa nchi hizo. Sasa ni juu ya serikali za nchi hizo, siyo tu kurejesha imani ya mabenki bali pia zinapaswa kuwapa wananchi wao matumaini. Kwa hivyo katika miezi inayokuja viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya watapaswa kuonyesha umahiri wa kuleta wizani baina ya sera za kubana matumizi na za kuleta ustawi.

Gazeti la"Döbelner Anzeiger linatoa maoni juu ya hatua iliyochukuliwa na mtandao wa kijamii wa "Facebook" ya kuingia katika soko la hisa. Mhariri wa gazeti hilo anasema ndoto ya kampuni hiyo ya kuchuma fedha nyingi kwa haraka inaweza kugeuka jinamizi!

Mhariri huyo anaeleza kuwa ni jambo la nadra kuona jinsi mwekaji vitega uchumi mwenye uroho wa kuchuma fedha, anakiona kilichomtoa kanga manyoya haraka, kama ilivyotokea kwa mtandao wa kijamii wa "Facebook". Soko la biashara la mtandao huo haliwezi kushindana na mtandao wa Google wala na kampuni ya Apple.

Mtandao wa kijamii wa"Facebook" unajipa kimo kisicholingana na urefu wake. Ni kweli kwamba matangazo ya biashara yanaweza kusaidia, lakini yanategemea simu za mkononi- smart-phone.Kwa hivyo ndoto ya mtandao wa kijamii "Facebook" ya kuchuma fedha haraka haraka inaweza kugeuka jinamizi. Miamala kwenye masoko ya hisa ni ya mashaka wakati wote!

Mwandishi: Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Abdul-Rahman