Wahariri wasema Ugiriki itoke Umoja wa Euro | Magazetini | DW | 14.02.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Wahariri wasema Ugiriki itoke Umoja wa Euro

Wahariri wa magazeti leo wanauzungumzia mgogoro wa Ugiriki na mkasa wa kushambuliwa afisa wa kibalozi wa Israel nchini India.Wahariri wanasema itakuwa bora kwa Ugiriki kujitenga na Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Gazeti la "Rhein Necker" linashauri talaka baina ya Ugiriki na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya. Linasema yeyote anaezingatia kwa makini, haraka sana atatambua kwamba litakuwa jambo la busara ikiwa Ugiriki na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya zitatengana. Mhariri wa "Rhein Necker" anasema hatua hiyo itaiimarisha sarafu ya Euro na pia itakuwa rahisi kwa Umoja wa Ulaya kuisaidia Ugiriki.

Mhariri wa gazeti la "Westdeutsche Zeitung"hakubaliani na hoja juu ya Ugiriki kujitenga na Umoja wa Ulaya. Lakini anaishauri nchi hiyo iyatekeleze masharti yote ili iweze kuepuka kufilisika Mhariri wa "Westdeutsche" ansema ikiwa Ugiriki inataka kuepusha baa la kufilisika, itapaswa kuyatekeleza masharti yote bila ya kupinda kona hata chembe. Ikiwa Ugiriki itajaribu kukwepa hata thumni moja ya masharti hayo, matokeo yake yakuwa maafa.

Gazeti la "Berliner Zeitung" linazungumzia juu ya upinzani mkali wa wananchi wa Ugiriki dhidi ya hatua za kubana matumizi zilizopitishwa na serikali yao. Gazeti hilo linasema hatua hizo ni za lazima lakini zitawaathiri wale wenye vipato ambavyo tayari ni vya chini, wale wanaopokea mishahara ya kima cha chini na wastaafu wanaopokea pensheni. Gazeti linasema wale wenye vipato vya juu hawataguswa na hatua hizo za kubana matumizi. Watu hao ni wale wanaokwepa kulipa kodi au wale walioyaficha mabilioni yao nje, kwa kusaidiwa na serikali. Hilo ni jambo lisiloeleweka lakini huo ndio ukweli.

Mhariri wa gazeti la "Landeszeitung "anauzungumzia mkasa wa kushambuliwa mwakilishi wa kibalozi wa Israel nchini India. Mhariri huyo anakumbusha kwamba hivi karibuni mwanasayansi wa Iran pia aliuawa. Anaeleza kuwa mauaji ya mwanasayansi wa Iran sasa yanajibiwa kwa mashambulio ya mabalozi wa Israel . Iran na Israel tayari zinashambuliana kikatili, kiasi cha kukaribia vita. Iran inafanya juhudi za kuunda bomu la nyuklia siyo kwa lengo la kuiangamiza Israel bali inalitaka bomu hilo ili kuzifanya nchi nyingine ziogope kuishambulia.

Mwandishi/Mtullya abdu/ Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Abdul-Rahman