1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wataka Gaddafi achukuliwe hatua kali

Abdu Said Mtullya17 Mei 2011

Wahariri wa magazeti ya Ujeruman wasema asilani Gaddafi asiruhusiwe kuondoka kwa heshima!

https://p.dw.com/p/11HhR
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa inayopambana na uhalifu ,Luis Moreno Ocampo.Picha: dapd

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni juu ya maombi yaliyotolewa na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Makahama ya Kimataifa inayopambana na uhalifu ya ICC , Moreno Ocampo ya kumkamata Kiongozi wa Libya Kanali Gaddafi mwanawe, pamoja na Mkuu wa idara ya upelelezi. Ocampo anadai kwamba pana ushahidi wa kutosha unaothibitisha kuwa Gaddafi kwa kauli yake alitoa amri ya kuwashambulia raia.

Mhariri wa gazeti la Kölner Stadt Anzeiger anasema endapo Mahakama ya Kimataifa inayopambana na uhalifu ya mjini The Hague italikubali ombi la kutolewa waranti wa kuwezesha kumkamata Gaddafi, Mahakama hiyo itapaswa kuepuka njia fupi, na imkazie macho dikteta huyo.

Mhariri huyo anaeleza kuwa yumkini pana mazungumzo yanayofanyika pembe za chaki baina ya Gaddafi na Umoja wa Mataifa, kwani mwishoni mwa wiki utawala wa Gaddafi ulipendekeza ,kwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa, hatua ya kusimamisha mapambano. Waziri wa mambo ya nje wa Italia aliarifu kuwa Gaddafi anatafuta njia ya kuondoka kwa heshima. Na ikiwa Mahakama ya kimataiafa itatoa waranti wa kumkamata Gaddafi, asilani asipewe uwezekano huo wa kuondoka na taadhima. Anaelipiza kisasi kwa kumwaga damu ya watu wake hastahili kuyamaliza maisha yake kwa heshima.

Gazeti la Frankfurter Rundschau pia linasisitiza katika maoni yake kwamba Mahakama ya kimataifa lazima ihakikishe kuwa njia zote zinazoweza kumpa Gaddafi nafuu zinazibwa. Mhariri wa gazeti hilo anasema sasa wapinzani wa Gaddafi wamesogea karibu na ndoto ya kumwona Gaddafi akiwa jela. Lakini wakati huo huo, Mahakama ya ICC inayopambana na uhalifu ihakikishe kwamba inazifunga njia zote zinazoweza kumpa dikteta Gaddafi nafuu. Kwani yeyote anaemwaga damu ya raia wake, ati kwa sababu raia hao wanapigania haki ya kuwa huru, hastahili kukimbilia nchi ya jirani na kuishi maisha mazuri!

Gazeti la Handelsblatt linaeleza kuwa ingawa waranti wa Mahakama ya Kimataifa , hautachangia katika uwanja wa mapambano dhidi ya Gaddafi, waranti huo utamshinikiza dikteta huyo. Maombi juu ya hati ya kuwezesha kumkamata Gaddafi, yaliyotolewa haraka sana na mwendesha mashtaka bwana, Ocampo hayatabadili hali ya mapambano nchini Libya, lakini waranti huo utafanya iwe vigumu kwa Gaddafi kujificha kwengineko, licha ya nchini mwake. Kwa kuwa Baraza la Usalama limehusika, basi kila mwanachama wa Umoja wa Mataifa atakuwa na wajibu wa kumkamata Gaddafi na kumfikisha mbele ya Mahakama ya ICC ya mjini the Hague.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/- Josephat Charo