1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boti ya wahamiaji yazama Libya, 200 waangamia

28 Agosti 2015

Boti iliyojaa wahamiaji imezama karibu na pwani ya Libya, na inahofiwa kwamba watu 200 wamekufa katika ajali hiyo. Na Austria imesema idadi ya maiti za wahamiaji zilizokutwa nchini humo, imepindukia 70.

https://p.dw.com/p/1GNDt
Boti iliyojaa wahamiaji pwani ya Libya, wakitaka kwenda Italia
Boti iliyojaa wahamiaji pwani ya Libya, wakitaka kwenda ItaliaPicha: Reuters/D. Zammit Lupi

Afisa wa usalama katika mji wa Zuwara magharibi mwa Libya ambako boti hiyo iliyozama ilianzia safari yake, amesema iling'oa nanga ikiwa na watu zaidi ya 400 ndani yake.

Afisa huyo ameendelea kueleza kwamba hadi jana jioni walinzi wa mwambao wa Libya walikuwa wamefanikiwa kuwaokoa watu 201, na 147 miongoni mwao walipelekwa moja kwa moja kwenye kizuizi kwa ajili ya wahamiaji haramu, kilicho Sabratha magharibi mwa mji mkuu, Tripoli.

Wasema wamelazimika kuchukua njia hiyo

Wengi wa wahamiaji waliokuwa wakisafiri na boti hiyo wanatoka katika nchi za Afrika Kusini ya jangwa la Sahara, Pakistan, Syria na Morocco. Mmoja wa wahamiaji walionusurika ajali hiyo, Ayman Tallaal kutoka Syria amewashukuru waliomuokoa.

Baadhi ya wahanga wakiwa katika mifuko ya kuhifadhia maiti
Baadhi ya wahanga wakiwa katika mifuko ya kuhifadhia maitiPicha: Reuters/H. Amara

Amesema, ''Tumelazimika kuifuata njia hii, ambayo inaitwa njia ya kifo, na sasa inaitwa kaburi la bahari ya Mediterania. Boti ilikuwa katika hali mbaya, na watu wetu wamekufa. Walibya wametuokoa, Mungu awabariki''.

Msemaji wa shirika la msaada la Hialali nyekundu, Khamis bin Omar, amesema hadi jana watu 66 walikuwa wamethibitishwa kufariki.

''Leo hii tumepata taarifa taarifa kuhusu ajali ya boti ya wahamiaji kwenye ufuo wa mji wa Zuwara. Timu yetu imewaokoa watu 198 ambao wanatoka mataifa mbali mbali. Watu 66, pia kutoka nchi mbali mbali, wamekufa hadi sasa''. Amesema Omar.

Libya uchochoro

Libya imekuwa njia muhimu inayotumiwa na wasafirishaji haramu wa binadamu, wanaoapeleka wahamiaji nchini Italia. Walinzi wa pwani ya nchi hiyo wana vifaa duni, na hutegemea boti za kujazwa hewa, na meli za uvuvi.

Shirika la Kimataifa linaloshughulikia wahamiaji, IOM limesema watu 2,300 wamezama katika bahari ya Mediterania mwaka huu, na mwaka jana wengine 3,279 walikufa katika bahari hiyo wakijaribu kuvuka kwenda Ulaya.

Maiti 70 ndani ya lori Austria

Wakati huo huo, wizara ya mambo ya ndani ya Austria imesema leo kuwa idadi ya maiti zilizopatikana katika lori lililotelekezwa kwenye barabara kuu nchini humo imepindukia 70.

Lori lililotelekezwa barabarani Austria, likiwa na maiti za wahamiaji zaidi ya 70
Lori lililotelekezwa barabarani Austria, likiwa na maiti za wahamiaji zaidi ya 70Picha: Reuters/H-P Bader

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye yuko nchini Austria kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Ulaya kuhusu mzozo wa wahamiaji, amesema ameshtushwa na taarifa za mkasa huo wa wahamiaji, na kusema anayo matumaini Ulaya itaushughulikia kwa pamoja mzozo huu wa wahamiaji unaozidi kupamba moto.

Bado yapo maswali mengi yasio na majibu kuhusu kisa hicho cha maiti za wahamiaji zilizokutwa ndani ya lori, kama wapi walikotoka wahamiaji hao, na nani aliyekuwa akiwasafirisha.

Wakaguzi wa barabara walilikuta barabarani lori hilo likiwa limetelekezwa, likiwa na nembo ya kampuni ya ufugaji wa kuku ya Slovakia, na nambari za usajili za Hungary. Tarifa za hivi karibuni zimeeleza kuwa Austria imewatia mbaroni watu watatu kuhusiana na kisa hicho.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/dpae

Mhariri: Iddi Ssessanga