1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahafidhina na wasocial Democrats wataunda serikali

18 Oktoba 2013

Viongozi wa vyama ndugu vya kihafidhina vya Christian Democratic Union-CDU na Christian Social Union CSU na wale wa chama cha Social Democratic-SPD wataanza mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto jumatano ijayo.

https://p.dw.com/p/1A224
Kansela Angela Merkel (kushoto)waziri mkuu wa jimbo la Bavaria,Seehofer na waziri wa usafiri Peter Ramauer baada ya mazungumzo pamoja na SPD mjini BerlinPicha: Reuters

Mazungumzo hayo ya kuunda serikali ya muungano wa vyama vikuu yanatarajiwa kudumu mwezi mmoja au miwili.Pande zote mbili zinaonyesha kuridhika na jinsi duru ya tatu ya mazungumzo ya kupima uwezekano wa kuunda serikali hiyo, ya tatu ya aina yake katika historia ya vyama hivyo,yalivyopita.

Alikuwa waziri mkuu wa jimbo la kusini la Bavaria Horst Seehofer aliyetangulia kutoa maoni yake aliposema:"Nimeridhika sana na nawatakia nyote wikiendi njema"

Hata kansela Angela Merkel ameonyesha kuridhika na jinsi mazungumzo hayo yalivyoendelea.

Badala yake mwenyekiti wa chama cha Social Democratic Sigmar Gabriel amesema wanaamini ufumbuzi wa maana kwa pande zote mbili utapatikana kuhusu masuala ambayo bado hayajatatuliwa.Sigmar Gabriel ameendelea kusema:"Hatukufika mbali hivyo kuweza kusema matukio thabiti yamepatikana wakati wa mazungumzo.Lakini tunaamini tunaweza kubuni msingi wa pamoja,pamoja na vyama ndugu vya CDU/CSU ili kuweza kukamilisha mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano kwa ufanisi."

Sigmar Gabriel Sondierungsgespräche CDU SPD 17.10.2013 in Berlin
Mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel (kati)akifuatana na mkuu wa kundi la wabunge wa chama chake Frank-Walther Steinmeier,waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westfalia Hannelore Kraft na Peer Steinbrück baada ya mazungumzo pamoja na wawakilishi wa CDU/CSU mjini BerlinPicha: picture-alliance/dpa

Mkutano mkuu wa SPD jumapili

Wakuu wa chama cha SPD watakutana jumapili ijayo kwa mkutano maalum unaotarajiwa kutoa ridhaa ya kuendelezwa mazungumzo ya kuunda serikali pamoja na vyama ndugu vya kihafidhina vya CDU/CSU.

Baadhi ya vigogo vya SPD,akiwemo pia waziri mkuu wa jimbo lenye wakaazi wengi zaidi la North Rhine Westfalia,bibi Hannelore Kraft,ambao awali walikuwa wakipinga kuundwa serikali ya muungano pamoja na CDU/CSU,wamebadilisha msimamo wao,

Merkel Gabriel Sondierungsgespräch
Kansela Angela Merkel na mwenyekiti wa SPD Sigmar GabrielPicha: picture-alliance/dpa

Maridhiano yasemekana yamefikiwa

Katibu mkuu wa chama cha kansela cha Christian Democratic Union,Herman Gröhe amesema anaamini,baada ya duru tatu za mazungumzo pamoja na Wasocial Democrats,kambi hizi mbili zinaweza kufikia maridhiano ya kutosha kuiongoza nchi kwa ufanisi."

Hadharani pande hizi mbili zinakwepa kutamka kwamba maridhiano yameweza kufikiwa hata hivyo duru za kuaminika

zinasema maridhiano yamefikiwa katika mada zilizokuwa zikizusha mabishano:SPD wamekubaliwa madai yao ya kuwepo kiwango cha chini cha mshahara kwa wote huku CDU/CSU wakifanikiwa kuzuwia mpango wa matajiri kutozwa kodi kubwa zaidi za mapato.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu