1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea wa urais Nigeria wakubaliana kudumisha amani

26 Machi 2015

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan anayegombea pamoja na mpinzani wake mkuu Muhammadu Buhari wametia saini hii leo makubaliano ya kuahidi kudumisha amani wakati na baada ya uchaguzi wa urais Jumamosi hii.

https://p.dw.com/p/1Ey5L
Picha: DW/Ubale Musa

Makubaliano hayo ya amani ni ya pili kufikiwa kwa pamoja na wagombea hao wawili wakuu wa Nigeria katika kipindi cha miezi mitatu. Hali ya usalama ni suala kuu linaloangaziwa katika uchaguzi huo wa Rais kutokana na kitisho kutoka kwa waasi wa kundi la Boko Haram ambao wameahidi kuutatiza uchaguzi huo na wasiwasi wa kutokea ghasia za baada ya uchaguzi kutoka kwa wafuasi wa makundi pinzani.

Katika uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2011, kiasi ya watu 1,000 waliuawa katika ghasia za baada ya uchaguzi baada ya Jonathan kumshinda Buhari katika kinyang'anyiro cha urais.

Makubaliano hayo ya leo ya kuahidi kudumisha amani yameshuhudiwa na aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan katika hoteli moja mjini Abuja na kutangazwa moja kwa moja katika vituo vya televisheni vya nchini humo.

Matokeo ya uchaguzi kuheshimiwa

Taarifa iliyotiwa saini na wagombea hao wawili imesema wamekubaliana kukariri kujitolea kwao kuzingatia na kuheshimu kuwepo chaguzi za amani hata baada ya kipindi cha kampeini kukamilika na kwa hivyo wanatoa wito kwa raia na wafuasi wao kujiepusha na vitendo vya ghasia vitakavyohujumu kuendeshwa chaguzi huru na za haki.

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan
Rais wa Nigeria Goodluck JonathanPicha: picture-alliance/AP

Viongozi hao wawili pia wameahidi kuheshimu matokeo ya uchaguzi huo wa Jumamosi. Makubaliano hayo muhimu pia yalitiwa saini na mwenyekiti wa kamati ya taifa ya amani Abdulsalami Abubakar ambaye kama Buhari, ni kiongozi wa zamani wa jeshi la Nigeria.

Aidha kutiwa saini kwa makubaliano hayo kulishuhudiwa na viongozi wa kidini, Sultan Sokoto Sa'ad Abubakar na askofu mkuu wa kanisa Katoliki mjini Abuja John Onaiyekan.

Jonathan mgombea wa chama tawala cha Peoples Democratic Party PDP, Buhari anayewania urais kupitia chama cha All Progressive Congress APC na wagombea wengine wa urais walitia saini makubaliano ya kwanza ya kuhakikisha hakutakuwa na ghasia wakati wa uchaguzi yajulikanayo Azimio la Abuja mnamo tarehe 14 mwezi Januari yaliyosimamiwa na Annan.

Ni kinyanganyiro kikali kati ya Jonathan na Buhari

Uchaguzi wa kipindi hiki unasemekana kuwa kinyang'anyiro kikali zaidi kuwahi kushuhudiwa Nigeria tangu kurejea kwa utawala wa kidemokrasia. Jonathan ambaye anashutumiwa vikali kutokana na jinsi alivoshughulikia kitisho cha uasi wa Boko Haram kaskazini mwa Nigeria na kutoukabili ufisadi serikalini ameahidi iwapo atachaguliwa kwa kipindi kingine cha miaka minne, atabuni nafasi milioni mbili za ajira kushughulikia tatizo la ukosefu wa kazi.

Mgombea urais nchini Nigeria Muhammadu Buhari
Mgombea urais nchini Nigeria Muhammadu BuhariPicha: Getty Images/P. Ekpei

Ushindi kwa upande wa upinzani ukiongozwa na Buhari utafungua ukurasa mpya wa mabadiliko ya kidemokrasia katika taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu na uchumi imara zaidi barani Afrika.

Chama cha Buhari cha APC kimekuwa kikiendesha kampeini zake kwa kauli mbiu ya kuleta mabadiliko Nigeria na kimeapa kufanya mageuzi serikalini ili kuweza kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi katika sekta mbali mbali zikiwemo elimu na usalama wa taifa.

Iwapo katika uchaguzi wa Jumamosi hakuna mgombea atakayefanikiwa kupata wingi wa kura na kupata asilimia 25 ya uungwaji mkono katika majimbo 24 nchini humo, Buhari na Jonathan watagombea katika duru ya pili ya uchaguzi ambayo haijawi kutokea katika chaguzi zilizopita nchini Nigeria. Kwa jumla kuna wagombea 14 wa urais katika uchaguzi huo.

Mwandishi:Caro Robi/Afp/Reuters

Mhariri:Josephat Charo