1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zoezi la upigaji kura laanza kuchelewa Uganda

Mjahida 18 Februari 2016

Waganda wanapiga kura katika uchaguzi wa rais na bunge, unaofanyika huku kukiwa na malalamiko ya masanduku ya kupigia kura kufika kuchelewa katika baadhi ya vituo vya kupigia kura na kufungwa kwa mitandao ya kijamii.

https://p.dw.com/p/1HxFw
Raia wakipiga kura katika uchaguzi wa rais na bunge Uganda
Raia wakipiga kura katika uchaguzi wa rais na bunge UgandaPicha: Getty Images/AFP/I. Kasamani

Hii leo asubuhi misururu mirefu ya watu ilionekana katika vituo vya kupigia kura mjini Kampala ambapo zoezi la kupiga kura lilianza kuchelewa kwa zaidi ya saa moja na nusu kufuatia maafisa wa uchaguzi kuendelea na matayarisho ya vifaa vya kupigia kura.

"Iwapo uchaguzi utachelewa namna hii, kutakuwa na watu wengi ambao hawatapata nafasi ya kupiga kura," alisema Dickson Mamber, mwalimu wa somo la historia, aliyekuwa katika foleni ya kupiga kura kwa zaidi ya saa mbili katika kituo cha Muyembe mjini Kampala.

Raia mwingine Joel Nyonyintono amesema anasikia aibu namna barabara na hospitali za Uganda zilivyo na kusema kwamba amekuja kupiga kura ili ampate kiongozi atakayewajibika. Nyonyintono anasema waganda ni lazima wafungue macho na waanze kuishi katika wakati wa sasa kuliko jana.

Raia wa Uganda wakisimama katika misururu mirefu ili kushiriki zoezi la upigaji kura
Raia wa Uganda wakisimama katika misururu mirefu ili kushiriki zoezi la upigaji kuraPicha: DW/E. Lubega

Zoezi hilo la upigaji kura linatazamiwa kukamilika saa kumi jioni saa za Afrika Mashariki bado hapajakuwa na taarifa zozote iwapo zoezi hilo litarefushwa kufuatia baadhi ya vituo kuanza shughuli hiyo kuchelewa.

Mawasiliano ya yamitandao ya jamii yafungwa kwasababu za kiusalama.

Huku hayo yakiarifiwa mdhibiti wa mawasiliano wa serikali ametangaza kufungwa kwa mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter na kufunga mifumo ya kutuma pesa kupitia njia ya simu. Kulingana na mkuu wa kamisheni ya mawasiliano nchini Uganda Godfrey

Mutabaazi aliyezungumza na kituo cha radio cha CBS, hatua hiyo imechukuliwa kwa sababu za kiusalama.

Kwengineko msemaji wa wizara ya nje ya Marekani Mark Toner amesema Washington ina wasiwasi kuwa vikwazo hivyovya mawasiliano huenda vikasababisha mivutano zaidi katika nchi ambayo tayari inakumbwa na joto kali la uchaguzi.

Wagombewa wa Urais Amama Mbabazi, Kizza Besigye na Rais Yoweri Museveni
Wagombewa wa Urais Amama Mbabazi, Kizza Besigye na Rais Yoweri MuseveniPicha: DW/Reuters/picture-alliance/dpa

Kwa upande mwengine wanaharakati wa haki za binaadamu wameelezea wasiwasi wao pia juu ya madai ya kuundwa kwa makundi ya vijana wenye silaha wanaohusishwa na vyama pamoja na wanasiasa mbali mbali kwa ajili ya kulinda maslahi ya vyama vyao kwenye uchaguzi huu.

Museveni aliye na miaka 71 aliyechukua madaraka kwa mara ya kwanza nchini Uganda mwaka wa 1986 na aliyeshinda uchaguzi mara nne kuanzia mwaka wa 1996, anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa wagombea wawili kati ya wagombea saba waliopo katika kinyang'anyiro cha urais.

Kizza Besigye, aliye na miaka 59, aliyekuwa daktari wa Museveni ndiye mgombea wa kwanza anayempa tumbo joto Museveni. Besigye ameshashindwa mara tatu katika safari yake ya kuwania urais nchini Uganda. Mwengine anayeonekana kutoa ushindani mkali ni Waziri Mkuu wa zamani Amama Mbabazi aliye na miaka 67.

Mike Sebalu, msemaji wa kampeni za chama tawala NRM amesema wanatarajia rais Museveni kushinda katika duru ya kwanza ya uchaguzi. Kiongozi wa Upinzani kutoka chama cha FDC Kizza Besigye pia alitoa tamko kama hilo katika kampeni zake za uchaguzi. Iwapo Museveni au mgombea mwengine yoyote atapata zaidi ya nusu ya idadi ya kura zitakazopigwa katika duru ya kwanza ya uchaguzi, uchaguzi huo hautarejewa katika duru ya pili.

Mwandishi Amina Abubakar/dpa/Reuters

Mhariri Daniel Gakuba