1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafadhili wachangisha fedha kuwasaidia Wasyria

Admin.WagnerD31 Machi 2015

Mfalme wa Kuwait ameahidi kuipa Syria msaada wa dola nusu bilioni katika ufunguzi wa mkutano wa wafadhili kwa ajili ya wasyria ambao wanakabiliwa na mzozo wa kibinadamu unaotajwa kuwa mbaya zaidi katika historia ya sasa.

https://p.dw.com/p/1Ezxh
Picha: Reuters/S. McGehee

Mflame wa Kuwait Sheikh Sabah al Ahmad al- Sabah ametangaza kutoa msaada wa kifedha wa dola milioni 500 kutoka kwa serikali yake na kutoka kwa sekta ya kibinafsi kusaidia katika juhudi za kutoa misaada ya kibinadamu Syria.

Akizungumza katika mkutano huo wa siku moja wa wafadhili unaofanyika leo nchini Kuwait, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema kati ya wasyria watano, wanne wamekuwa maskini kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza miaka minne iliyopita na taifa hilo limerudi nyuma kimaendeleo kutokana na mzozo huo.

Wasyria wengi wamekuwa maskini

Ban ambaye ni mwenyekiti wa mkutano huo wa wafadhili, amesema watu wa Syria ni waathiriwa wa mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu wa historia ya wakati huu.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: picture-alliance/dpa/Karim Kadim

Umoja wa Mataifa unatumai kuchangisha dola bilioni 8.4 katika mkutano huo wa wafadhili wa kutoka nchi zaidi ya 78 na ambao pia unayashirikisha mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu ili kuweza kukidhia mahitaji ya mamilioni ya watu wa Syria walioachwa bila ya makaazi.

Katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema karibu nusu ya idadi ya watu wa taifa hilo, wanaume, wanawake na watoto wamelazimika kuyatoroka makaazi yao na takriban watu milioni 18 nchini Syria na katika nchi jirani wanahitaji misaada ya kibinadamu.

Kuwait imekuwa mwenyeji wa mikutano ya wafadhili kwa ajili ya Syria kwa miaka miwili iliyopita ambayo imechangisha mabilioni ya fedha kupitia ahadi zinazotolewa na wahisani.

Misaada zaidi inahitajika

Katika mkutano wa wafadhili ulioandaliwa mwaka 2013, wahisani walichangisha kiasi cha dola bilioni moja na nusu lakini mwaka jana mkutano huo uliweza tu kupokea ahadi za michango cha kima cha dola 2.4 kati ya bilioni 6.5 zilizokuwa zikihitajika kukidhia mahitaji ya waathiriwa wa Syria na mashirika ya kutoa misaada yameonya huenda yakalazimika kukatiza operesheni zao kutokana na ukosefu wa ufadhili wa kutosha.

Wafadhili wa kimataifa kwa ajili ya Syria wakikutana Kuwait
Wafadhili wa kimataifa kwa ajili ya Syria wakikutana KuwaitPicha: Reuters/Egyptian Presidency

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, kiasi ya watu laki mbili wameuawa katika vita hivyo vya Syria, 850,000 wamejeruhiwa na takriban watu milioni kumi na moja wameachwa bila ya makaazi tangu kuzuka kwa wimbi la kutaka mageuzi ya uongozi yaliyoanza mwaka 2011 kupitia maandamano ya kumshinikiza Rais Bashar Al Assad aondoke madarakani.

Idadi ya wasyria wanaohitaji msaada wa kibinadamu imeongezeka kwa watu milioni 2.9 katika kipindi cha miezi kumi iliyopita. Kabla ya mkutano huo wa wahisani ulioanza leo, serikali ya Ujerumani iliahidi msaada wa dola milioni 277, wakati Marekani ikiahidi kutoa dola milioni 507.

Mwandishi:Caro Robi/Afp/Reuters/Ap

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman