1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge nchini Zimbabwe waanza kuapishwa leo.

Nyanza, Halima25 Agosti 2008

Wabunge nchini Zimbabwe wameanza kuapishwa, huku wabunge wawili wa upinzani wakikamatwa, hali ambayo imelalamikiwa kwamba ni hila ya kupunguza idadi yao bungeni, katika kipindi ambacho Spika mpya anatarajia kuapishwa.

https://p.dw.com/p/F4Mv
Rais Robert Mugabe na kiongozi wa upinzani nchini humo, Morgan Tsvangirai, ambao wawakilishi wao bungeni wameanza kuapishwa leo.Picha: AP

Msemaji wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini humo cha Movement for Democtratic Change MDC, Nelson Chamisa amewataja wabunge hao kuwa ni Eliah Jembere na mwenzake Shuah Mudiwa walikamatwa na polisi mapema leo wakati wakiingia katika eneo la bunge siku ambayo wabunge walikuwa wakianza kuapishwa.

Amefahamisha pia kwamba wamepata habari kuwa wabunge wengine 15 wa chama hicho wanataka kukamatwa, na kuongeza kuwa hali hiyo inaonesha mpango wa wazi wa kutaka kuwaondoa bungeni ama kupunguza wingi wao, katiika kipindi ambacho Spika mpya wa bunge anatarajia kuchaguliwa.

Kufuatia kukamatwa kwa wabunge wake wawili chama kikuu cha upinzani nchini humo kimeonya kuwa hali hiyo inatishia mazungumzo ya kugawana madaraka.

Aidha chama hicho cha upinzani pia, kimepinga uamuzi wa Rais Robert Mugabe wa kufungua rasmi bunge la nchi hiyo kesho kwamba hali hiyo pia itasababisha kuvunjika kwa mazungumzo hayo ya kuunda kwa serikali ya pamoja ili kumaliza mzozo wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo kwa sasa.

Uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge nchini Zimbabwe ulifanyika mwezi Machi mwaka huu, na kusababisha machafuko ya kisiasa baada ya kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai kudai kuwa Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo alipanga matokeo ya uchaguzi wa Rais na kwamba alikuwa akiwatishia wafuasi wake.

Katika uchaguzi huo wa bunge kwa mara ya kwanza chama tawala nchini humo cha ZANU PF kilipata pigo kubwa badala ya kuambulia viti 97 bungeni, wakati chama kikuu cha upinzani cha MDC kikipata viti 100, huku chama kingine cha MDC kilichojitenga ambacho kinaongozwa na Arthur Mutambara kikijipatia viti 10.

Muda mfupi baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu nchini humo uliofanyika mwezi Machi, polisi walitangaza msako kwa wanasiasa kadhaa wa chama hicho cha kwa tuhuma za mauaji, ubakaji na kusababisha ghasia katika kipindi cha kampeni za uchaguzi.

Kwa sasa pande hizo mbili zinazopingana kisiasa nchini Zimbabwe zimekuwa katika mazungumzo hayo ya kugawana madaraka ambayo yameshindwa kukamilika kutokana na viongozi, kushindwa kuafikiana katika kugawana madaraka ambapo Rais Mugabe amekuwa akidai kuwa Bwana Tsvangirai anataka kumnyang'anya madaraka yote, huku Tsvangirai naye, akidai kuwa Rais Mugabe hataki kuachilia nyadhfa zenye mamlaka ya juu.

Katika hatua nyingine Baraza la Usalama na amani la Umoja wa Afrika limemaliza jana mkutano wake nchini Misri bila kutoa taarifa kuhusu mzozo wa Zimbabwe, badala yake baraza hilo limetoa wito kwa bara la Afrika kwa ujumla kushughulikia suala la Zimbabwe.

Wakati huohuo Rais George Bush wa Marekani na Rais Blaise Compaore wa Bukina Faso ambaye yuko nchini Marekani wamezungumzia juhudi za kuleta amani na kukomesha mizozo inayoikumba Zimbabwe na pia nchini Sudan.