1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Ukraine kuendelea na kura ya maoni

Josephat Nyiro Charo8 Mei 2014

Waasi mashariki ya Ukraine wamesema kura ya maoni kuhusu kujitenga itaendelea kama ilivyopangwa licha ya mwito wa rais wa Urusi, Vladimir Putin, kutaka iahirishwe ili kutoa nafasi mazungumzo yafanyike.

https://p.dw.com/p/1Bvt5
Ostukraine Krise doch Referendum 08.05.2014 Donezk
Picha: Reuters

"Kura ya maoni itafanyika Mei 11," amesema kiongozi wa waasi wa Jamhuri ya watu wa Donetsk, Denis Pushilin, wakati alipozungumza na waandishi wa habari. Msemaji wa wanamgambo katika mji wa Slavyansk amelithibitishia shirika la habari la AFP kwamba kura hiyo ya maoni itafanyika siku ya Jumapili kama ilivyopangwa.

Wanamgambo katika jamhuri nyingine iliyojitangazia uhuru wake katika mji wa Lugansk wamesema nao pia watafanya kura yao maoni siku hiyo ya Jumapili. Maamuzi hayo yanakuja siku moja tu baada ya rais Putin kuwataka waasi waahirishe kura za maoni kutoa fursa ya kufanyika mazungumzo kuutanzua mzozo wa Ukraine. Baada ya kupigwa na butwaa na kauli hiyo ya rais Putin waasi wameshauriana na kuamua kulikataa kata kata pendekezo la kiongozi huyo. Urusi imesema inahitaji taarifa zaidi kuweza kuutathmini uamuzi huo.

Russland Schweiz Präsident und Außenminster Didier Burkhalter bei Wladimir Putin in Moskau
Rais Vladimir Putin, kulia, na rais wa Uswisi, Didier BurkhalterPicha: Reuters

Awali waziri mkuu wa Ukraine, Arseniy Yatsenyuk, akizungumzia kuhusu kura hiyo ya maoni. "Rais wa Urusi anahitaji kufahamishwa kwamba hakukuwa na kura ya maoni iliyopangwa kufanyika Mei 11. Lakini kama magaidi na waasi wanaotaka kujitenga na wanaoungwa mkono na Urusi wamepewa amri kuahirisha kitu ambacho hakipo, hilo ni suala lao la ndani.

Uuamuzi wa waasi wakosolewa

Umoja wa Ulaya umesema uamuzi wa kuendelea na kura hiyo ya maoni ambao hauna uhalali unaweza tu kuzidi kuivuruga hali ya mambo. Akizungumza baada ya uamuzi wa waasi mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, amesema "Kura kama hiyo haitakuwa na uhalali wa kidemokrasia na itazidi kuifanya hali kuwa mbaya."

Umoja wa Ulaya pia umesema unafuatilia kwa karibu yanayoendelea nchini Ukraine kuona kama rais Putin atachukua hatua baada ya kusema anaondoa majeshi ya nchi yake kutoka mipaka ya Ukraine. Jumuiya ya NATO imesema ingali inasubiri kuona dalili zozote kuashiriia Urusi imeviondoa vikosi vyake. "Nataka niwahakikishie tutakapopata ushahidi wa kutosha kwamba kweli wanaondoa wanajeshi wao, nitakuwa wa kwanza kuikaribisha hatua hiyo," amesema katibu mkuu wa NATO, Anders Fogh Rassmussen, mjini Warsaw nchini Poland leo baada ya kukutana na waziri mkuu wa nchi hiyo, Donald Tusk.

Rasmussen und Tusk PK in Warschau 08.05.2014
Katibu mkuu wa NATO, Anders Fogh Rassmussen, kushoto, na waziri mkuu wa Poland, Donald TuskPicha: picture-alliance/dpa

Marekani na NATO zinakadiria Urusi ina wanajeshi 40,000 katika mpaka wa Ukraine huku serikali ya mjini Kiev ikipambana na wanamgambo wanaoiunga mkono Urusi.

Putin kuhudhuria kumbukumbu za D-Day

Wakati haya yakijiri, rais Putin atakutana na viongozi wa nchi za magharibi kwa mara ya kwanza tangu kuzuka mzozo wa Ukraine wakati atakapohudhuria kumbukumbu ya miaka 70 tangu wanajeshi wa kwanza wa muungano walipowasili Normandy, Ufaransa, hatua iliyoashiria mwanzo wa ukombozi wa bara la Ulaya kutokana na manazi wa Ujerumani wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia. Rais wa Marekani, Barack Obama, na kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, ni miongoni mwa viongozi watakaodhudhuria kumbukumbu hizo za D-Day Juni 6.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/AFPE/APE

Mhariri: Yusuf Saumu