1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Waasi wa Tuareg watafuta suluhu na Ansar Dine

Waasi wa Tuareg na viongozi wa kundi la Kiislamu kaskazini mwa Mali wanajaribu kupunguza kupata muafaka, baada ya Watuareg kuukataa mpango wa kuanzisha taifa lililojitenga na Mali lenye kufuata Sharia

Wapiganaji wa Ansar Dine kaskazini mwa Mali.

Wapiganaji wa Ansar Dine kaskazini mwa Mali.

Viongozi wa Vuguvugu la Tuareg la Ukombozi wa Azawad (MNLA) na wale wa kundi la Ansar Dine walikutana katika mji wa kaskazini mashariki wa Gao hapo jana (Ijumaa, 1 Juni 2012) baada ya MNLA kusema kwamba imeachana na mpango wa makubaliano yaliyodumu kwa wiki moja kwa sababu kundi la Ansar Dine kusisitiza utumiaji wa Sharia.

Walil Ag Cherif wa Ansar Dine ameiambia Shirika la Habari la AFP kwa njia ya simu kuhusiana na mazungumzo hayo kwa njia ya simu bila ya kutaja undani wake. Mkutano huo umethibitishwa kufanyika na upande wa Tuareg. Ansar Dine (Walinzi wa Imani) walikuwa wamekataa kubadilisha msimamo wao wa kutumia mfumo wa Sharia, na ambao ulikataliwa na kundi la MLNA.

"Uongozi wa kisiasa wa MNLA ulipingana na msimamo wa Ansar Dine kutumia Sharia katika Azawad na kubakia na azimio lake la kutochanganya dini na siasa, unakataa makubaliano ya tarehe 26 Mei 2012 uliofanya na kundi hilo na unatangaza chochote kuhusiana na makubaliano hayo kimefutwa," ilisema taarifa ya MLNA.

Tamko la Alhamis lililosainiwa na mwanachama wa ngazi ya juu wa MNLA, Hamma Ag Mahmoud katika mji mkuu wa Azawad, Gao, lilikuwa la mwanzo rasmi kuthibitisha kujitoa kwa waasi hao kwenye makubaliano na Ansar Dine.

Makundi hayo hasimu, ambayo yaliiteka miji mikuu kaskazini mwa mwali baada ya mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 22 Machi katika mji mkuu, Bamako, yana itikadi na malengo tafauti na mahusiano yao yamekuwa ya mashaka.

Mgawanyiko wa MNLA na Ansar Dine

Wapiganaji wa Ansar Dine wakilinda eneo la kaskazini.

Wapiganaji wa Ansar Dine wakilinda eneo la kaskazini.

Dhamira iliyodumu muda mchache ya kuyaunganisha ilikufa haraka kutokana na hamu ya Ansar Dine kulazimisha utawala wa sharia katika dola hilo mpya, ambalo hadi sasa halitambuliki kimataifa.

Msemaji wa MLNA anayeishi mjini Paris, Mossa Ag Attaher, aliiambia Afpa kwamba walikuwa wamekubali wazo la kuwa na Dola ya Kiislamu "lakini ilipaswa kuandikwa kwamba tutatekeleza Uislamu usio wa misimamo mikali na wenye ustahmilivu, bila ya kutaja sharia. Hatuko tayari kujikuta sisi wenyewe tumefungwa na sharia kutoka siku hadi siku," aliongeza.

Lakini ambapo MLNA ilikuwa tayari kupambana na ugaidi, alisema Watuareg hawatowacha dhamira yao ya kuwa na dola huru ya Azawad, jina wanalotumia kwa nchi kaskazini mwa Mali, ambalo ni eneo kubwa zaidi kuliko nchi nzima ya Ufaransa. Tayari waasi wa Tuareg wameshapoteza wapiganaji wengi kwa Ansar Dine.

Mgawanyiko ndani ya MNLA

Msemaji wa MLNA, Moussa Ag Assarid.

Msemaji wa MLNA, Moussa Ag Assarid.

Chanzo kimoja cha usalama kwenye eneo hilo, akizungumza kwa sharti la kutokutajwa jina, aliiambia AFP kwamba kujiunga na Ansar Dine kumewagawa waasi wa MLNA, ambao wengi wao walirudi kwenye eneo hilo mwezi Januari wakiwa na silaha nzito kutoka kwa aliyekuwa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, na kufufua mapambano yao ya muda mrefu ya kudai uhuru.

Waasi hao waliwasukuma wanajeshi wa serikali kutoka kaskazini mwa nchi hiyo na kupelekea mapinduzi yaliyoiondoa serikali ya Mali, baada ya maafisa wa jeshi kulalamika kwamba walikuwa hawapati vifaa walivyohitaji kupambana.

Katika kulitumia ombe la kisiasa, waasi hao walifanikiwa kuchukuwa udhibiti wa eneo la kaskazini la nchi hiyo ambalo ni karibuni nusu nzima ya Mali. Lakini kundi la Ansar Dine, linaloungwa mkono na tawi la al-Qaida katika eneo la Sahel (AQIM), walichukuwa udhibiti wa mapambano hayo, kwa kuichukua miji muhimu yote kama vile Timbuktu na kuanzisha sharia ya Kiislamu.

Viongozi wa eneo hilo la mataifa ya magharibi wamekuwa wakihofia kwamba dola iliyojitenga na Mali kaskazini mwa nchi hiyo inaweza kuwa ngome imara ya al-Qaida. Tayari kiongozi wa juu wa AQIM amewashauri Ansar Dine kuunda dola la Kiislamu.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Sudi Mnette