1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makundi ya waasi Syria yatofautiana kuhusu kukutana na Urusi

Admin.WagnerD5 Novemba 2015

Ujumbe wa makundi ya waasi nchini Syria umekubali kukutana na maafisa wa Urusi wiki ijayo kuujadili mzozo wa Syria. Hata hivyo wawakilishi wa baadhi ya makundi ya waasi wamepuuzilia mbali ripoti hizo za kuwepo mkutano.

https://p.dw.com/p/1H0T0
Picha: picture alliance/Photoshot

Kulingana na mratibu wa muungano huo wa makundi ya waasi wa Syria yakijulikanayo Free Syrian Army-FSA, Mahmoud al Afandi, vikosi 28 vya FSA vinavyopigana Damascus, Quneitra, Hama, Homs, Aleppo na Idlib vimekubaliana kukutana na maafisa wa Urusi.

Hata hivyo wawakilishi wa makundi manne ya waasi hao wa Syria yamekanusha ripoti zilizotolewa na shirika la habari la Urusi kuwa wamekubali kukutana na maafisa wa Urusi.

Wawakilishi wa makundi hayo waliowasiliana na shirika la habari la Reuters wamesema ripoti hiyo ni ya uongo na kuongeza maafisa wa Urusi wamekuwa wakikutana na wasyria wanaojidai kuwa waasi wa jeshi la ukombozi wa Syria.

Urusi yaongeza juhudi za kidiplomasia

Hivi karibuni, Urusi imeongeza juhudi zake za kujaribu kuupatanisha utawala wa Rais Bashar al Assad na waasi wanaotaka kumng'oa madarakani. Naibu wa waziri wa mambo ya nje wa Urusi Mikhail Bogdanov amesema Ikulu ya Rais itawaalika wawakilishi wa pande zote mbili zinazozana Syria kwa mkutano mjini Moscow wiki ijayo.

Rais wa Syria Bashar al Assad na Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Syria Bashar al Assad na Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Reuters/RIA Novosti/Kremlin/A. Druzhinin

Hayo yanakuja huku Urusi ikituma makombora ya kinga dhidi ya mashambulizi ya ndege Syria kupiga jeki kampeini yake ya mashambulizi ya angani dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la dola la kiislamu IS.

Kamanda wa kikosi cha wanajeshi wa angani wa Urusi Viktor Bondarev amesema waliamua kutuma makombora hayo Syria kwa kuzingatia vitisho vyote vilivyopo na kuongeza wana zaidi ya ndege na helikopta hamsini Syria kwa ajili ya operesheni.

Marekani imesema mashambulizi ya angani yanayofanywa na Urusi, yameuzidisha mzozo wa Syria na kuishutumu kwa kujaribu kumsaidia Rais Bashar al Assad kusalia madarakani badala ya kupambana dhidi ya wanamgambo wa IS.

Wakati huo huo, shirika la kutetea haki za binadamu la Syria limesema waasi wa kundi la Jund al Aqsa wameyadhibiti maeneo mengi ya mji wa Morek katika jimbo la Hama.

Kudhibitiwa kwa mji huo kunafuatia mapigano ya miezi kadhaa kati ya waasi wa kundi hilo la Jund al Aqsa wakisaidiwa na waasi wa makundi mengine na wanajeshi wa serikali.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri: Yusuf Saumu