1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Libya waukaribia mji wa Sirte

Halima Nyanza(ZPR)28 Agosti 2011

Baraza la Mpito la waasi wa Libya limesema, vikosi vyake viko umbali wa kiasi ya kilomita 30 kutoka mji wa Sirte, alikozaliwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi.

https://p.dw.com/p/12P3D
Wapiganaji waasiPicha: picture alliance / dpa

Kwa mujibu wa msemaji mmoja, mazungumzo yanafanywa, kumtaka Gaddafi ajisalimishe, lakini ikiwa  hayatofanikiwa, basi waasi watashambulia.

Lakini, msemaji wa Baraza la Mpito la waasi, Mahmoud Shammam amesema, hakuna uhakika kuwa waasi watamkuta Gaddafi katika mji huo na wala hawajui kwa hakika, kule aliko.

Libyen Muammar Gaddafi Moammar Gadhafi
Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi asakwa kwa udi na uvumbaPicha: picture-alliance/dpa

Wakati huohuo, Shirika la Haki za Binadamu la Human Right Watch limesema, majeshi ya Gaddafi huenda ikawa, yaliwaua wafungwa na raia kadhaa, wakati waasi walipokuwa wakiingia mji mkuu Tripoli, wiki iliyopita.

Shirika hilo limesema, miili kadhaa iliyokuwa imepigwa risasi iligunduliwa ufukweni mwa mto karibu na eneo la makaazi ya Gaddafi.

Umoja wa Nchi za Kiarabu umetoa mwito kwa nchi wanachama wake na Umoja wa Mataifa kuachia mali ya Libya iliyozuiliwa, kwani sasa kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi ameondolewa madarakani.