1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi Syria wakabiliana vikali na serikali

2 Desemba 2016

Waasi nchini Syria wamekabiliana vikali katika mji wa Aleppo, ambapo mashambulizi yaliyofanywa na vikosi vya serikali yamesababisha vifo, na kuacha miili yao ikitapakaa kwenye viunga vya mji huo

https://p.dw.com/p/2TeNk
Syrien Offensive der Armee in Aleppo
Picha: picture-alliance/abaca/AA/J. al Rifai

Hali hii inaendelea kutoa msukumo kwa jumuiya ya kimataifa kutoa mwito wa kumalizwa kwa mapigano hayo. 

Mashambulizi yanayofanywa na serikali kwenye mji uliopo Kaskazini mwa Syria na kusambaa yamesababisha vifo vya maelfu ya raia wanaoishi kwenye mji huo unaoshikiliwa na upinzani wa Aleppo ulioko eneo la mashariki na kuibua mwito mpya kwa Urusi kutaka kufunguliwa kwa njia salama za kupitisha misaada ya kiutu.

Majeshi ya Rais Bashar al-Assad wiki hii yamefanikiwa kulikamata eneo la Kaskazini Mashariki la mji huo na yalikuwa yakielekea kuukamata mji mwingine wa Sheikh Saeed ambao ni mkubwa katika eneo la pembe la Kusini Mashariki. Hata hivyo wapiganaji wanaoipinga serikali wameweka ulinzi mkali kwenye eneo hilo kwa usiku mzima, na kuyarejesha nyuma majeshi ya serikali, hii ikiwa ni kulingana na taarifa kutoka shirika la waangalizi la haki za binaadamu la nchini Syria.

Majeshi ya serikali pamoja na wapiganaji wanaoyaunga mkono walitaka kuuchukua mji huo kwa gharama yoyote, kwa kuwa hatua hiyo itawarahisishia kuyalenga maeneo yote yaliyosalia ambayo yanashikiliwa na serikali, amesema msimamizi wa shirika hilo Rami Abdel Rahman. Hata hivyo waasi wameweka upinzani mkubwa kwa kuwa wanajua watakamatwa kiurahisi wakiruhusu majeshi hayo kuukamata mji huo, amesema.

TOPSHOT-SYRIA-CONFLICT
Mmoja wa watoto wa Syria anayeishi kwenye mji jirani wa Jibrin baada ya familia yake kukimbia mapigano Mjini AleppoPicha: Getty Images/AFP/Y. Karwashan

Msemaji kutoka shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto, UNICEF, Christophe Boulierac amesema hali ya watoto nchini Syria ni ya kusitikisha. Wengi miongoni mwao walio chini ya miaka mitano, hawajui kingine zaidi ya vita.

Afisa kutoka shirika la waangalizi lenye makao yake nchini Uingereza amesema, majeshi ya serikali kwa sasa yanashikilia angalau asilimia 70 ya maeneo ya jirani. Wilaya ya Sheikh Saed, linalopakana na sehemu ya mwisho ya mji wa Aleppo ndilo pekee linaloendelea kushikiliwa na waasi na linalokaliwa na maelfu ya raia walioomba hifadhi baada ya kukimbia mashambulizi ya majeshi ya serikali yanayozidi kusonga mbele.

Taarifa kutoka shirika la waangalizi zinasema, zaidi ya raia 300, ambao ni pamoja na idadi kubwa ya watoto wameuwawa katika eneo la Mashariki mwa Aleppo tangu serikali ilipoanzisha uvamizi Novemba 15. Kulingana na shirika la habari la Syria, SANA, raia mmoja aliuwawa na watatu kujeruhiwa leo hii kufuatia shambulizi la roketi lililofanywa na waasi. 

Kusambaa kwa mashambulizi hayo mjini Aleppo kumeibua wasiwasi wa jumuiya ya kimataifa, na Alhamisi hii Umoja wa Mataifa ulionya kuhusu mji huo kuwa eneo kubwa la kaburi. Urusi nayo ilitaka kuwekwa kwa njia salama nne za kupitisha misaada ya kiutu kuingia mjini Aleppo na kuwezesha kuwaondoa majeruhi. Awali, iliwahi kutoa mwito wa kusimamishwa kwa mapigano ili kuruhusu raia kuondoka kwenye mji huo, lakini hadi wakati majeshi ya serikali yalipoanzisha tena mashambulizi ni wachache tu waliokuwa wamefanikiwa kuondoka.

Mwandishi:Lilian Mtono/ AFPE
Mhariri:Josephat Charo