Waandishi habari wauwawa Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.02.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waandishi habari wauwawa Syria

Vikosi vya rais wa Syria Bashar al Assad vinaendelea kufanya mashambulizi zaidi katika mji wa Homs ambapo hii leo watu 19 wameuwawa wakiwemo waandishi habari wawili kutoka nchi za magharibi.

Mwandishi Marie Colvin aliyeuwawa mjini Homs, Syria

Mwandishi Marie Colvin aliyeuwawa mjini Homs, Syria

Kuuwawa kwa waandishi hao wawili wa habari katika mji wa Homs nchini Syria kumezua hisia mbali mbali kutoka kwa jamii ya kimataifa inayotaka juhudi zaidi kufanyika ili kukomesha mapigano nchini humo. 

Marie Colvin, mwandishi wa Kimataifa kutoka Marekani anayefanyia kazi gazeti la Uingereza la Sunday Times pamoja na mpiga picha raia wa Ufaransa, Remi Ochlik, waliuwawa wakati kombora moja liliporushwa na kuangukia nyumba waliyokuwa wakifanyia kazi iliyoko katika kitongoji cha Baba Amr, mwanaharakati mmoja mashuhuri nchini humo pia aliuwawa huku waandishi wengine kadhaa wakijeruhiwa.

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy

Akizungumza bungeni hii leo waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron, alitoa heshima zake za mwisho kwa mwandishi Marie Colvin. Cameron amesema kifo chake kinaashiria misukosuko na changamoto kubwa wanayopata wanahabari wanapokuwa mbioni kutoa habari kwa Ummah.

Kwa upande wake rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, amesema kuuwawa kwa waandishi hao kunamaanisha kwamba imefikia wakati ambapo utawala wa rais Bashar Al Assad unapaswa kuondoka.

Marekani kupitia msemaji wa wizara ya mambo ya nje, Victoria Nuland, imesema huu ni mfano wa matukio ya kinyama yanayofanywa na utawala wa Assad.

Mauaji zaidi Baba Amr

Vikosi vya serikali vyazidi kuvurumisha makombora Baba Amr

Vikosi vya serikali vyazidi kuvurumisha makombora Baba Amr

Mamia ya watu wanaendelea kuuwawa katika mashambulizi ya mara kwa mara mjini Homs yanayotekelezwa na vikosi vya rais Assad. Hatua hii imezua wasiwasi kwamba huenda rais huyo akataka kuangamiza mji huo kama alivyofanya babake miaka 30 iliyopita katika mji wa Hama kwenye machafuko yaliyosababisha vifo vya watu 10,000.

Marekani sasa inaonekana kutaka kuwapa silaha wapinzani nchini humo. Marekani imesema iwapo suluhu juu ya mzozo wa Syria haiwezi kupatikana haraka itazingatia mbinu nyengine. Kitongoji cha Baba Amr katika mji wa Homs kimekuwa ngome ya mashambulizi tangu Februari 3.

Huku hayo yakiarifiwa shirika la msalaba mwekundu limeomba kusimamishwa kwa mapigano ili kutoa nafasi ya kupeleka misaada ya kibinaadamu hasaa katika mji wa Homs ambapo watu wanakufa na njaa na kutegemea maji ya mvua kwa mahitaji yao ya kila siku.

Jana wanaharakati nchini humo walisema vikosi na jeshi la Assad liliwateka nyara na kuwauwa wanaume 27 katika vijiji vya kaskazini mwa nchi hiyo. Ghasia nchi Syria zimeanza miezi 11 iliyopita wakati waandamanaji walipoanza maandamano ya kutaka demokrasia na mabadiliko nchini humo. Watu zaidi ya 6000 tayari wameshauwawa katika ghasia hizo

Mwandishi Amina Abubakar/DPAE/AFPE

Mhariri Josephat Charo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com