1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji wakamatwa na polisi Urusi

6 Machi 2012

Mamia ya watu waliandamana jana katika mitaa ya Urusi kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika nchini humo Jumapili iliyopita. Waandamanaji hao wanapinga matokeo yaliyomtangaza Vladimir Putin kama rais mpya wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/14FeB
Polisi wakiwa katika Uwanja wa Puschkin, Moscow
Polisi wakiwa katika Uwanja wa Puschkin, MoscowPicha: DW

Itakumbukwa kwamba tayari Putin ambaye sasa ni waziri mkuu hadi pale atakapoapishwa, aliwahi kuwa rais kuanzia mwaka 200 hadi 2008.

Jana wizara ya mambo ya ndani ya Urusi iliwatuma polisi wake maalum kwenda katika uwanja wa Puschkin uliopo katikati ya mji mkuu Moscow, ambapo maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi yalikuwa yakifanyika. Polisi hao waliwakamata zaidi ya waandamanaji 160. Mara kwa mara polisi walitoa amri kupitia spika wakiwataka waandamanaji waache maandamano na kurudi majumbani kwao. Lakini matangazo hayo yalipuuzwa. Hadi kufikia saa moja jioni, watu 20.000 walikua wamekwishafika katika uwanja wa Puschkin. Idadi hiyo ni kulingana na wapinzani, lakini polisi wa Moscow wanasema kwamba idadi ya waandamanaji ilikuwa 14.000. Waandamanaji hao walipiga kelele na kusema kwamba wanataka kuwa na Urusi bila Putin. Vladimir Ryschow anayeuunga mkono upande wa upinzani alikuwa mtu wa kwanza kuzungumza katika maandamano hayo:

"Tunataka ugandamizwaji wa kisisasa ukomeshwe," alisema Ryschow. "Tunataka waliofanya hila katika kamati ya uchaguzi wajiuzulu. Na la muhimu zaidi: tunataka pawepo na uchaguzi mpya wa bunge na wa rais. Uchaguzi huu haukuwa halali."

Waandamanaji wanaopinga matokeo ya uchaguzi
Waandamanaji wanaopinga matokeo ya uchaguziPicha: Reuters

Hata kabla ya maandamano kufanyika, polisi walijaribu kuwazuia waandamanaji kufika katika uwanja wa Puschkin. Waandamanaji wengi walionyesha kuwa na hasira na mara kwa mara walipaza sauti na kusema "Putin ni mwizi, Putin lazima apelekwe gerezani." Wengi wamesema kwamba Putin alipolia hadharani baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi kulikuwa na kuigiza tu. Sergej Udalzow mwenye mtazamo mkali wa mrengo wa kushoto anaeleza: "Ninashikwa na hasira ninapotazama mchezo mchafu unaochezwa na ikulu ya Kremlin ambao wao wanauita kuwa ni uchaguzi."

Maandamano katika uwanja wa Puschkin yalikuwa yamepangwa kuisha saa tatu usiku. Udzaldow alikamatwa na polisi kwa kuwa alikataa kuondoka kwenye uwanja huo baada ya maandamano kuisha. Miongoni mwa waliokamatwa pia alikuwemo mwandishi maarufu wa Blogu, aitwaye Alexei Nawalny.

Leo wapinzani wamepanga kuandamana tena, na inatarajiwa kwamba mamia kwa maelfu ya watu watashiriki.

Mwandishi: Hermann Krause/Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman