1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waafrika wa 'Kiyahudi' wapata tabu Uganda

9 Juni 2014

Watoto wa Sudan Kusini waliokuwa wakiishi Israel na ambao sasa wamepelekwa Uganda wanakabiliwa na changamoto kubwa la kutangamana upya na jamii kwa kuwa lugha pekee wanayoijua ni Kiabrenia.

https://p.dw.com/p/1CEx5
Watoto wa Kiafrika wakiandamana nchini Israel kupinga kurejeshwa kwao kwa nguvu.
Watoto wa Kiafrika wakiandamana nchini Israel kupinga kurejeshwa kwao kwa nguvu.Picha: picture-alliance/dpa

"Musizugumze Kiabrenia", ndivyo walimu wa Kiganda wanavyorejea mara kwa mara kuwaambia vijana hawa, lakini ni Kiabrenia ndicho wanachozungumza wanapokuwa hawaangaliwi na mtu, maana ndiyo lugha waliyokulia nayo kama wahamiaji nchini Israel.

Vijana hawa wapatao 70 sasa wanapaita Uganda kuwa ndipo nyumbani pao baada ya kuhamishwa Israel kwa hiyari yao, nchi ambayo inajaribu kuwaondosha maelfu ya wahamiaji wa Kiafrika.

Katika miaka ya hivi karibuni, Waafrika wamekuwa wakimiminika nchini Israel, wakisababisha mvutano na wenyeji na kuzua taharuki kwa viongozi wa serikalik wanaosema kuwa ule uasili wa Kiyahudi wa dola hiyo unatishiwa na kuwepo kwa Waafrika.

"Aibu kwa Israel"

Baada ya kuondoka Israel, vijana hao walikaa kwenye nchi yao ya uzawa kwa miezi michache, ambako waliteseka sana kutokana na kitisho cha njaa, maradhi ya nchi za joto na hali mbaya ya kisiasa.

Watoto wa Sudan ya Kusini wakiwa ukimbizini Uganda.
Watoto wa Sudan ya Kusini wakiwa ukimbizini Uganda.Picha: Reuters

Baadaye wakahamishiwa Uganda, kutokana na kazi ya mwanaharakati mmoja wa Kiisraili, ambaye amekuwa akiikosoa sera ya nchi yake kuelekea wahamiaji wa Kiafrika kama "aibu kwa Israel."

Mwanaharakati huyo mwenye umri wa miaka 44, Rami Gudovitch, anachukuliwa na vijana hao kama baba na rafiki. Awali alijaribu kuzuia kabisa kuhamishwa kwao Israel na aliposhidwa kwenye hilo akatafuta familia ambazo zilikuwa tayari kugharamikia elimu yao wawapo Afrika.

Mwezi Disemba 2012, alilitia kundi moja kwenye basi kutoka mji mkuu wa Sudan ya Kusini, Juba, kuelekea mji mkuu wa Uganda, Kampala, ambako watoto hao walitazamia kurejea skuli na kuanza maisha upya kama wakimbizi.

Masomo magumu Kampala

Wengi kati ya hao waliosajiliwa kwenye skuli ya binafsi ya dakhalia mjini Kampala, wana walezi wa Kiisraili ambao wanawalipia masomo yao kwa kiasi cha dola 1,000. Wanaushukuru sana msaada huu, lakini hauwezi kufuta kumbukumbu zao kwa nchi ambayo walikuwa wakiita kwao kwa sehemu kubwa ya maisha yao.

Sehemu ya maisha ya watu wa vijini Uganda.
Sehemu ya maisha ya watu wa vijini Uganda.Picha: picture-alliance/dpa

Wanajikuta wakilazimika kutangamana na utamaduni na mfumo tafauti wa elimu, huku wakiwa hawana msaada wa kifamilia. Wanafunzi wengi ambao walipaswa kuwa tayari wameshafanya mitihani ya kuijngia chuoni kwa miaka miwili iliyopita, ndiyo kwanza wameganda kwenye kiwango cha chini cha alama, kwa sababu Kiingereza chao hakitoshi.

Hili linatokana na kung'olewa Israel bila matayarisho hayo, kwani huko walikuwa wakisoma kwa Kiabrenia tu.

Mwalimu wa Sayansi anayeongoza programu za kitaaluma kwenye Skuli ya Trinity, Alex Gumisiriza, anasema kwamba watoto hao walijikuta wakikabiliana na kikwazo cha lugha tangu siku ya mwanzo kuwasili hapo, ingawa wanajitahidi kukichupa.

Kumbukumbu za 'nyumbani'

Wanafunzi kadhaa waliozungumza na shirika la habari la AP, waliondoka Israel baina ya mwaka 2011 na 2012 na wakaishi kwanza Sudan ya Kusini kabla ya kwenda Uganda.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu (kushoto), ambaye serikali yake inawafukuza wahamiaji wa Kiafrika.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu (kushoto), ambaye serikali yake inawafukuza wahamiaji wa Kiafrika.Picha: Reuters

Hatua hii imezinvunja kabisa familia zao, ambapo miezi kadhaa hupita bila kuonana na wazazi wao. Ingawa wazazi wao wameamua kurejea Sudan ya Kusini kwa hiyari yao kutokana na kuongezeka kwa chuki dhidi ya wakimbizi nchini Israel, wengi walirejeshwa kwa nguvu.

Victoria James, mwenye umri wa miaka 16, anasema waliambiwa kwamba nchini Israel hawataki wakimbizi, kwani tayari kulishakuwa na wakimbizi wengi.

"Lilikuwa jambo baya kulazimishwa kuondoka. Nilikuwa nalazimishwa kurudi nchi ambayo siku nikiijua hata kidogo." Analalamika Victoria, ambaye anasema anawakumbuka sana marafiki na walimu wake, ambao huwasiliana nao mara kwa mara kupitia mtandao wa Facebook.

Wengi wa wenzake waliopo Uganda wanasema wanakumbuka sana majengo ya maduka makubwa mjini Tel Aviv na viwanja vya mpira wa vikapu, ambavyo havipo vingi Kampala.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman