1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyombo vya usalama DRC vinazuwia uchunguzi

Sekione Kitojo
2 Mei 2018

Idara za usalama za Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo zinaingilia uchunguzi kuhusiana na mauaji ya wataalamu wawili wa  Umoja wa Mataifa,huku zikiizuwia maafisa wa Umoja wa Mataifa kuwahoji mashahidi muhimu na watuhumiwa.

https://p.dw.com/p/2x0hK
UN-Mitarbeiterin Zaida Catalan im Kongo getötet
Picha: AFP/Getty Images/B. Ericson

Katibu  mkuu  wa  Umoja  wa  Mataifa  Antonio Guterres  ametuma wachunguzi  wa  Umoja  huo  kwenda  Jamhuri  ya  Kidemokrasi  ya Congo  kusaidia  maafisa  nchini  humo  kuwabaini  watu waliohusika   katika  mauaji  mwaka  jana  ya  Mmarekani  Michael Sharp na  Zaida Catalan  raia  wa  Sweden  katika  jimbo  la  Kasai.

Ikiongozwa  na  Robert Petit kutoka  Canada, timu  hiyo imekuwa ikifanyakazi  tangu  mwezi  Novemba  na  mwendesha  mashitaka wa  jeshi  la  Congo  katika  mji  wa  Kananga  katika  jimbo  la Kasai, lakini  mafanikio  yamekuwa  madogo, imesema  ripoti  hiyo iliyotumwa  katika  baraza  la  Usalama  la  Umoja  wa  Mataifa wiki mbili  zilizopita.

USA UN-Sicherheitsrat - Syrienkonflikt - Guterres
Katibu mkuu wa UN Antonio GuterresPicha: Reuters/E. Munoz

Mwezi  Agosti, uchunguzi  wa  Umoja  wa  mataifa  uiligundua kwamba  wanamgambo  wa  eneo  hilo  huenda wanahusika  katika mauaji  ya  watu  hao  wawili  waliokuwa  wakifanya  uchunguzi  wa machafuko  katika  eneo  hilo  kati  ya  majeshi  ya  serikali  na wanamgambo.

Sharp  na  Catalan  walikuwa  wakifanya  uchunguzi  kuhusiana  na makaburi  yaliyozikwa  watu  wengi  na  uhalifu  ulioambatana  na uasi  katika  jimbo  la  Kasai  ambako  walitekwa  pamoja  na wenzao raia  wa  Congo  Machi  mwaka  2017.

Miili  ya  Sharp, mratibu  wa  kundi  hilo  na  mtaalamu  wa  silaha, na Catalan , ambaye  alikuwa  mtaalamu wa masuala  ya  kiutu, iligunduliwa  katika  kaburi  na  wanajeshi  wa  kulinda  amani  wiki kadhaa  baada ya  kutoweka. Catalan  alikatwakatwa.

Oberster Gerichtshof des Kongos weist Wahlbeschwerde Bembas zurück Polizei
Polisi wa Congo Picha: picture-alliance/ dpa

Watuhumiwa wahamishwa

Baada  ya  kukamatwa  kwa  wanaodaiwa  kuwa  wanachama  wa kundi  la  wanamgambo, Vincent Manga  na  Francois Badibanga, mwezi  Machi, uchunguzi  wa  Umoja  wa  Mataifa  uliweza  kwa muda  mfupi  kuwahoji  mjini  Kananga  kabla  ya  ghafla  kuhamishwa kwenda  Kinshasa, "wakiwa  katika  mahabusu  ya  jeshi  la  polisi," ripoti  hiyo  imesema.

Timu  ya  Umoja  wa  Mataifa  inataka  kumhoji mkalimani ambaye alikuwa  ameongozana  na  wataalamu  hao  waliouwawa, Thomas Nkashama, lakini "duru  kadhaa  za  kuaminika zimemuweka  mtu huyo  mikononi  mwa  polisi kwa  muda,"  ripoti  imeeleza.

"Ni  wazi  kabisa  kwamba  vyombo  vya  usalama  mjini  Kinshasa vinaendelea  kuingilia  kati  na  hatua  za  mahakama  na  vinadhibiti njia  ya  kuwapata  mashahidi  muhimu  na  watuhumiwa," imesema ripoti  hiyo  iliyotayarishwa  na  idara  ya  masuala  ya  kisiasa  ya Umoja  wa  mataifa.

Joseph Kabila Präsident der Demokratischen Republik Kongo
Rais wa DRC Joseph KabilaPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Wachunguzi  wa  Umoja  wa  Mataifa  wamewaomba  maafisa  wa Congo  ruhusa  ya  kuwahoji  watuhumiwa  wanne  wengine waliokamatwa  mwezi  Desemba  na  kuwekwa  kizuwizini  mjini Kinshasa, lakini  kwa  sasa  wanasubiriwa  kupelekwa  mjini Kananga  licha  ya  uhakikisho  kutoka  waziri  wa  sheria. Jumla  ya watuhumiwa  26 wanakabiliwa  na  mashitaka  kwa  mauaji  ya Sharp  na  Catalan, 14  kati  yao  wanashitakiwa  wakiwa  hawapo mahakamani,  lakini  ripoti  hiyo  imeeleza  kuwapo  na  matundui kadhaa  katika  kesi  hiyo  iliyowasilishwa  na  mwendesha mashitaka.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman