1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyama vya Kadima na Likud vyaendelea kukabana.

Halima Nyanza/AFP11 Februari 2009

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Tzipi Livni na Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu, leo wamejikuta katika kiny'ang'anyiro cha kuwania madaraka, kufuatia matokeo ya uchaguzi yaliyokaribiana.

https://p.dw.com/p/Grwo
Kiongozi wa chama cha siasa cha Kadima cha Israel Tzipi Livni, (kulia) na kiongozi wa chama cha siasa cha Likud Benjamin Netanyahu, (kushoto), wako katika mvutano wa kuwania nafasi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo.Picha: AP

Chama cha Tzipi Livni chenye kufuata mrengo wa kati cha Kadima kimeshinda viti 28 katika bunge lenye wajumbe 120, ikiwa kinaongoza kwa kiti kimoja zaidi mbele ya chama cha Likud kinachoongozwa na Benjamin Netanyahu, hali ambayo imeacha nchi hiyo pengine kukabiliwa na mashaka ya kisiasa kwa wiki kadhaa.


Matokeo hayo ambayo yanaelemea sana upande wa mrengo wa kulia yanatoa uwezekano wa Benjamin Netanyahu kurejea katika wadhfa huo muhimu.

Lakini kwa upande wake Tzipi Livni tayari ameanza mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano baada ya kukutana na kiongozi wa chama cha Yisrael Beiteinu, ambacho kilishika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo uliofanyika jana, Avigdor Lieberman.


Awali, akizungumza mbele ya wafuasi wake kwenye makao makuu ya chama cha Kadima Tzipi Livni amesema, wananchi wa Israel wameamua kukichagua chama chake na kumuomba Benjamin Netanyau ajiunge, katika kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.


Kwa upande wake, Benjamin Netanyahu amesema chama chake kimekubaliana na washirika wake kuunda serikali ya pamoja, na hivyo atazungumza kwanza na washirika wao, vyama vya mrengo wa kulia, ambapo tayari amekwisha kuzungumza na baadhi yao, na wameafikiana kuanza mazungumzo haraka ya kuunda serikali mpya.


Viongozi hao wote wawili, Benjamin Netanyahu, ambaye ameweka rekodi ya kuwa waziri mkuu mwenye umri mdogo nchini Israel mwaka 1996, na Tzipi Livni, wote kwa pamoja wamekuwa wakitaka kushika wadhfa huo wa Waziri Mkuu.


Chini ya mfumo wa siasa za Israel, ni chama kinazingatiwa kuunda serikali ya mseto, na chama hicho hupewa jukumu na Rais kuunda serikali mpya.


Rais wa Isreal, Shimon Peres, tayari amesema kuwa ataanza mashauriano hayo wiki ijayo.


Katika hatua nyingine viongozi wa Mamlaka ya Palestina, wakizungumzia kuhusu uchaguzi huo wameelezea kushangazwa na nguvu iliyooneshwa na mrengo wa kulia, ambapo kiongozi wa ujumbe wa Palestina katika mazungumzo ya kutafuta suluhu katika mzozo wao na Israel, Saeb Erakat amesema hiyo ni dhahiri kuwa Waisrael wamepiga kura kudhoofisha mpango wa amani katika eneo hilo, huku Msemaji wa Hamas akisema kuwa wapiga kura wamechagua wagombea wenye msimamo mkali kabisa.


Kupata nguvu kwa vyama vyenye siasa kali nchini Israel, kutokana na vita vya Gaza na wasiwasi wa Waisrael juu ya usalama wao, na uwezekano wa vyama hivyo vya mrengo wa kulia kuunda serikali, kunaweza kuvuruga juhudi zinazoungwa mkono na Marekani kufufua juhudi za kuleta amani katika eneo hilo la mashariki ya kati ambazo zinalega lega.