1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vizingiti katika mpango wa amani kati ya Israel na Palestina

Mwakideu, Alex6 Mei 2008

Idadi kubwa ya wayahudi hawaamini kama kuna siku Israel itaishi kwa amani na wapalestina

https://p.dw.com/p/Dudw
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas na waziri mkuu wa Israeli Ehud Olmert wakaa katika meza moja wakiongozwa na wapatanishi wengine katika mazungumzo ya amani kati ya nchi hizo mbili.Picha: AP

Idadi kubwa ya wayahudi haiamini kama amani itapatikana kati yao na wapalestina.


Hayo ni kulingana na kura ya maoni iliyofanywa na chuo kikuu cha Tel Aviv. Baadhi ya sababu zinazowanyima amani wapalestina na wayahudi ni usalama, mipaka na mji wa Jerusalem.


Wakati Marekani inaendelea na juhudi za kutafuta amani ya mashariki ya kati imedhibitishwa kwamba asilimia 70 ya wayahudi hawaamini kwamba swala hilo linaweza kufaulu kati yao na wapalestina.


Asilimia 54 ya wale walioshiriki katika kura hiyo ya maoni wameonyesha kuridhishwa na mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina ilhali asilimia 34 kati yao walipinga mazungumzo hayo.


Asilimia sabini ya wayahudi imeunga mkono kuundwa kwa taifa la Palestina kando ya Israel kama ilivyopendekezwa katika mpango wa kimataifa wa amani ya mashariki ya kati.


Katika maswala nyeti zaidi asilimia 55 ya wayahudi wamepinga kupeanwa kwa maeneo ya kiarabu ya Jerusalem mashariki kwa Palestina.


Palestina inataka kulifanya eneo la Jerusalem Mashariki ambalo Israel ililiteka mwaka wa 1967 kuwa jiji kuu la nchi hiyo katika siku za usoni.


Kura ya maoni iliyofanywa na chuo kikuu cha Tel Aviv imeendelea kusema kwamba asilimia 66 ya wayahudi hawana imani kwamba Israel itafikia makubaliano ya amani kati yake na Syria.


Mazungumzo hayo kati ya Israel na jirani yake wa kaskazini yalikwama miaka nane iliyopita lakini katika wiki chache zilizopita pande hizo mbili zimekuwa zikitumiana jumbe za kuonyesha kwamba ziko tayari kurejea katika mazungumzo ya mapatano


Wayahudu asilimia 75 wanahofia kwamba nchi yao itajikuta vitani dhidi ya nchi moja au zaidi za kiarabu katika miaka michache ijayo.


Kura hii ya maoni imetolewa wiki moja kabla ya Rais wa Marekani George Bush kuanza ziara yake nchini Israel anakotarajiwa kujiunga na wayahudi kusherehekea miaka 60 ya taifa hilo.


Rais huyo anatarajiwa kujadili mazungumzo ya amani kati ya Rais wa Palestina Mahmoud Abbas na waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert.


Lakini baada ya miezi tano ya mazungumzo kati ya pande hizi mbili wadadisi wanasema maswala ya Jerusalem, usalama, mipaka na wakimbizi ndio yamekuwa yakizua tofauti inayochelewesha mapatano.


Katika maswala ya usalama Israel tayari imeweka mamia ya walinda usalama wake katika maeneo ya mji wa Jenin ulioko katika ukingo wa magharibi na vijiji vinavouzunguka kama ishara ya kwamba serikali yake inaweza kusimamia mji huo baada ya kuusimamia ule wa Nablus mwaka uliopita.


Nchi hiyo imesema hakuna maelewano yoyote ya amani yatakayoafikiwa hadi pale wanamgambo wa Palestina watakaposalimisha silaha zao. Na kwa upande wake Palestina inasema vikwazo vya Israel na mashambuliio yake ya mara kwa mara ndio sababu ya kutopatikana amani.


Kuhusu mipaka Israel imeripoti kwamba imepiga hatua kubwa ili kumaliza mzozo huo; jambo linalopingwa na Palestina.


Maafisa wa ulaya wanasema Olmert ameonyesha nia ya kupeana takribani asilimia 90 ya ukingo wa magharibi na asilimia nyingine 100 ya ukanda wa gaza kwa wapalestina kama njia ya kutafuta suluhusho la kudumu kati ya nchi hizo.


Abbas amekuwa akiitisha asilimia mia ya ukingo wa magharibi na ukanda wa gaza. Ambayo ni sawa na kilomita 6, 205 mraba eneo ambalo anasema Israel ililiteka mwaka wa 1967 wakati wa vita vya mashariki ya kati.


Katika swala la mji wa Jerusalem Abbas anataka Jerusalem Mashariki iwe jiji kuu la Palestina katika siku za usoni ilhali Israel inasisitiza kwamba Jerusalem yote ni mji wake mkuu jambo ambalo halijapasishwa na jamii ya kimataifa.


Kuhusu wakimbizi Israel imekataa kukubali mamilioni ya wapalestina kurudi katika ardhi yake. Nchi hiyo inaitaka Palestina iwache kupigania Jerusalem na mipaka yake kabla ya kupokea wakimbizi hao.


Wakati hayo mpatanishi kutoka Misri Omar Suleiman ambaye anajaribu kuleta matano ya kuzuia mashambulio kati ya Israel na Hamas anatarajiwa kuwasilini inchini Israel wiki ijayo.