1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viwanda vya kusafishia mafuta barani Afrika

8 Machi 2008
https://p.dw.com/p/DL0B

Kiwanda kipya cha kusafishia mafuta nchini Afrika Kusini huenda kikawa kiwanda pekee kitakachojengwa kusini mwa Sahara kutoka miradi mingi iliyopendekezwa katika kanda hiyo.

Katika miaka ya hivi karibuni,miradi fulani ya maendeleo ilitangazwa katika nchi za Kiafrika kama Angola,Nigeria na Zimbabwe.Lakini baadhi kubwa ya miradi hiyo itakwama kwa sababu ya gharama zinazozidi kuongezeka,ukosefu wa utulivu wa kisiasa pamoja na matatizo ya pesa za kusimamia miradi hiyo.

Bara la Afrika linazidi kuwa msafirishaji muhimu wa mafuta lakini pia ni mnunuzi mkubwa wa mafuta yaliyosafishwa kwa sababu mahitaji yake yanaongezeka na kuna uhaba wa viwanda vya kusafishia mafuta.Kwa mfano katika mwaka 2003, Nigeria inayochukua nafasi ya nane miongoni mwa wauzaji wakubwa kabisa wa mafuta duniani,ilitoa leseni 18 kwa wawekezaji wa binafsi kujenga viwanda vya kusafishia mafuta,lakini baadhi kubwa ya leseni hizo zimefutwa kwani viwanda hivyo havikujengwa.

Wawekezaji wengi waliokubali kujenga viwanda hivyo,waliachilia mbali miradi hiyo kwani usafishji wa mafuta nchini Nigeria ni biashara iliyo na hasara kwa sababu bei za mafuta hudhibitiwa.Kiwanda kimoja kidogo tu ndio kinajengwa katika jimbo la Akwa Ibom kusini mwa Nigeria ambako serikali imeshindwa kubinafsisha viwanda vyake vinne vya kusafishia mafuta.

Mradi mmoja mkubwa unaotazamiwa kusonga mbele ni ule uliotangazwa mwaka jana na kampuni ya mafuta ya Afrika Kusini PeteroSA kujenga kiwanda kitakachogharimu Dola bilioni 5.85 katika bandari ya Coega karibu na mji wa Port Elizabeth kwenye pwani ya kusini.Kiwanda hicho kitaweza kusafisha mapipa laki mbili na nusu kwa siku na hivyo Afrika Kusini itaongeza uwezo wake wa kusafisha mafuta kwa asilimia 30.Kampuni hiyo imeajiri wahandisi wa kampuni ya Kimarekani-KBR kufanya upembuzi yakinifu.Uamuzi wa uwekezaji utapitishwa mwaka 2010 na kiwanda hicho kinatazamiwa kuanza kufanya kazi katika mwaka 2014 au 2015.Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kutimiza mahitaji ya nishati ya Afrika Kusini yanayozidi kuongezeka kwa sababu ya ukuaji wa kiuchumi ulio imara.Nchi za jirani pia huenda zikauziwa mafuta hayo.

Wakati ambapo mashirika makuu ya mafuta yanajitenga na shughuli za usafishaji wa mafuta barani Afrika,makampuni ya China yenye mahitaji makubwa ya nishati yametia saini makubaliano ya kusafisha mafuta lakini maendeleo ni madogo.Mwaka jana serikali ya Angola ilisema imeamua kujenga peke yake kiwanda cha kusafishia mafuta,baada ya kufuta makubaliano na kampuni ya Kichina Sinopec iliyotazamiwa kukijenga kiwanda hicho.Msumbiji, Ivory Coast na Zimbabwe ni nchi zingine kusini mwa sahara zinazotazamia kujenga viwanda vya kusafishia mafuta.