1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vyazuka kati ya Georgia na jimbo la Ossetia Kusini

Charo, Josephat8 Agosti 2008

Marekani na Umoja wa Ulaya zataka mapigano yakomeshwe mara moja

https://p.dw.com/p/Espd
Wanajeshi wa Georgia wakishika doria katika kijiji cha ErgnetiPicha: AP

Rais wa Georgia Mikhail Saakashvili ametangaza kulishirikisha jeshi lote la taifa huku vikosi vikipania kulidhibiti jimbo lililojitenga la Osssetia Kusini. Rais Saakasvhili amewatole amwito raia wa Georgia waungane pamoja kuinusuru Georgia. Aidha kiongozi huyo amesema atawataka askari wa akiba kuingia vitani huku mapigano makali yakiendelea katika mji mkuu wa jimbo la Ossetia Kusini, Tskhinvali.

Maafisa wa jimbo la Ossetia Kusini wamesema watu 18 wameuwawa katika mapigano ya usiku wa kuamkia leo baada ya Georgia kushambulia kutumia ndege za kivita na silaha nzito za kisasa. Afisa mmoja katika jimbo hilo amesema wanajeshi wa Georgia wamevurumisha makombora katika mji mkuu wa Ossetia Kusini na majengo mengi yanawaka moto. Moshi mweusi umetanda katika anga ya mji wa Tshinvali na milio ya risasi na silaha bado inaendelea kusikika.

Wizara ya mambo ya ndani ya Georgia imesema ndege tatu za kivita za Urusi aina ya Sukhoi 24 zimeingia katika anga ya Georgia na kuvurumisha mabomu kuyalenga maeneo mawili ya Georgia hii leo, kusini mwa jimbo la Ossetia ambako mapigano yamechacha. Rais wa Georgia Mikhail Saakashvili amethibitisha kufanywa kwa mashambulio hayo na ameishutumu Urusi kwa uchokozi.

Wanajeshi wa Urusi wauwawa

Jeshi la Urusi limesema kambi ya jeshi lake la kulinda amani katika jimbo la Ossetia Kusini imeshambuliwa na wanajeshi kadhaa wameuwawa.

Waziri mkuu wa Urusi, Vladamir Putin amelaani vikali uchokozi unaofanywa na wanajeshi wa Georgia na kuonya kwamba nchi yake italipiza kisasi dhidi ya harakati ya kijeshi ya Georgia. Akiwa mjini Beijing China kuhudhuria ufunguzi wa michezo ya Olimpiki, waziri mkuu Putin ameilaumu Georgia kwa kujaribu kuliteka jimbo la Ossetia Kusini lakini hakusema Urusi inapanga kuchukua hatua gani.

Mazungumzo kati ya mjumbe maalumu wa Urusi, na mwenzake wa Georgia kujaribu kuzuia kuzuka kwa mapigano kati ya Georgia na jimbo la Ossetia Kusini yaligonga mwamba.

Mjumbe wa Georgia katika mazungumzo hayo, Jakobaschwili anasema ´´Ni wazi kwamba waasi katika mji mkuu wa Ossetia Kusini wanataka kuyavuruga mazungumzo. Wanajaribu kuuchokoza upande wa Georgia ili kuzusha vita. Wanajaribu kwa njia hii kudhihirisha nguvu na uwezo wao.´´

Miito yatolewa

Hii leo Marekani imetaka umwagajaji damu ukomeshwe mara moja na pande husika zifanye mazungumzo kuutanzua mgogoro kuhusu jimbo la Georgia lililojitenga la Ossetia Kusini.

Umoja wa Ulaya umeeleza wasiwasi wake kuhusu mapigano kati ya Geogia na jimbo la Ossetia Kusini na kutaka mapigano yasitishwe. Afisa mmoja wa umoja huo ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema Umoja wa Ulaya unawasiliana na washirika wake wa kimataifa wakiwemo Urusi, Marekani, Georgia na muungano wa usalama na ushirikiano barani Ulaya.

Mashauriano yameanza kati ya muungano huo na Ufaransa ambayo kwa sasa inashikilia urasi wa Umoja wa Ulaya.