1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Syria viko kwenye ''mkwamo''

20 Septemba 2013

Naibu waziri Mkuu wa Syria amesema vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini mwake vimefika kwenye mkwamo, na kwamba serikali inaweza kutoa pendekezo la mapatano ya kusimamisha mapigano.

https://p.dw.com/p/19kxI
Qadri Jamal amesema hakuna upande unaoweza kupata ushindi katika vita vya Syria
Qadri Jamal amesema hakuna upande unaoweza kupata ushindi katika vita vya SyriaPicha: Reuters

Kiongozi huyo, Qadri Jamal ameyasema hayo katika mahojiano na gazeti la The Guardian linalochapishwa nchini Uingereza. Katika mahojiano hayo amesema hakuna upande wowote kati ya serikali na waasi wanaoipinga, ambao unao uwezo wa kuushinda mwingine. Jamal amesema hali hii ya mkwamo katika vita vya zaidi ya miaka miwili nchini Syria inaweza kuendelea kwa muda mrefu.

Vile vile Jamal alitaja yale ambayo serikali ya Syria ingeyapeleka katika mkutano utakaohusu mustakhari wa nchi hiyo, ambao unatarajiwa kufanyika mjini Geneva kwa tarehe ambayo bado haijapangwa. Amesema serikali ya rais Bashar al-Assad itataka kusitishwa kwa uingiliaji wa kigeni katika mzozo wa Syria, kusimamishwa kwa uhasama na kuanzishwa kwa mchakato wa kisiasa kwa njia ya amani.

Qadri Jamal amesema watataka mchakato huo ufanyike katika mazingira ya kidemokrasia ambamo wasyria wote watatoa mawazo yao bila uingiliaji wa kigeni. Aidha, naibu waziri mkuu huyo ambaye ni mmoja wa watu wawili walio katika baraza la mawaziri kutoka nje ya chama tawala cha Ba'ath, alisema ripoti ya wataalamu wa silaha wa Umoja wa Mataifa kuhusu shambulio la silaha za kemikali, iliegemea upande mmoja.

Muungano wa upinzani walaani wanamgambo

Huku hayo yakiarifiwa, Muungano wa upinzani nchini Syria umelaani mashambulizi yaliyofanywa na kundi lenye mafungamano na mtandao wa al-Qaida liitwalo ISIS dhidi ya jeshi la muungano huo, linalojulikana kama Jeshi Huru La Syria.

Muungano wa upinzani wa Syria umesema mienendo ya ISIS ni kinyume cha mapinduzi
Muungano wa upinzani wa Syria umesema mienendo ya ISIS ni kinyume cha mapinduziPicha: picture alliance/Photoshot

Tangazo lililotolewa na upinzani leo Ijumaa, limesema na hapa nanukuu, ''Muungano wetu unalaani uchokozi dhidi ya jeshi la mapinduzi ya Syria, na ukiukaji wa mara kwa mara wa haki ya maisha ya wasyria, na unaichukulia mienendo hiyo kuwa kinyume cha maadili na malengo ya mapinduzi''. Mwisho wa kunukuu.

Tangazo hilo lililaani hasa hatua ya kundi hilo la ISIS kuuteka mji wa Azaz ulio kwenye mpaka baina ya Syria na Uturuki, baada ya mapigano ya saa nzima na jeshi huru la Syria Jumatano wiki hii, na jaribio la kundi hilo kukikamata kivuko kingine cha mpakani cha Bab as-Salameh.

Iran yajitolea kusuluhisha

Na rais mpya wa Iran Hasan Rouhani amejitolea kusaidia kuzileta pamoja pande zinazohasimiana nchini Syria. Katika makalayake iliyochapishwa katika gazeti la The Washington Post la Marekani, toleo lake la leo, Rouhani amesema eneo la mashariki ya kati linapaswa kuweka mazingira yanayoruhusu watu wake kujiamulia mambo yao wenyewe.

Rais wa Iran Hasan Rouhani mwenye dhamira ya usuluhishi
Rais wa Iran Hasan Rouhani mwenye dhamira ya usuluhishiPicha: Behrouz/AFP/Getty Images

''Katika kuelekea kwenye hali hiyo, natangaza kujitolea kwa serikali yangu kuikutanisha serikali ya Syria na waasi wanaoipinga'', alisema Rouhani katika makala hiyo.

Tangu alipoingia madarakani mwezi Agosti, Rais Hasan Rouhani ameonyesha dhamira ya mazungumzo na Marekani pamoja na pande nyingine ambazo kwa muda mrefu zimekuwa na tofauti na Iran. Vile vile ametoa wito wa kuanzishwa upya mazungumzo kati ya nchi yake na mataifa yenye nguvu ulimwenguni, kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran ambao unaandamwa na utata.

Mwandishi: Daniel Gakuba/DPA/AFP

Mhariri: Josephat Charo