1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Libya vyazidi kuugawa ulimwengu

27 Aprili 2011

Vita vya Libya vinachukuwa sura ya vita vya kidiplomasia kwenye jamii ya kimataifa, huku Urusi na Umoja wa Afrika zikisimama upande mmoja na Umoja wa Mataifa na nchi za magharibi zikisimama upande mwengine.

https://p.dw.com/p/114dx
Waombolezaji wakiibeba maiti baada ya mabomu ya Misrata
Waombolezaji wakiibeba maiti baada ya mabomu ya MisrataPicha: AP

Ushindi wa waasi wa Libya mjini Misrata dhidi ya vikosi vya kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi, unaelezwa kuwa ni wa hatua moja mbele, moja nyuma, kutokana na vikosi vya Gaddafi kuendelea kuushambulia mji huo na kuongezeka kwa idadi ya wahanga.

Taarifa za asubuhi ya Jumatano zimethibitisha kuwa maroketi kadhaa yamerushwa kutoka upande wa vikosi vya Gaddafi kuelekea bandari ya Misrata na kuilazimisha meli ya Shirika la Kimataifa la Wahamiaji ishindwe kutia nanga kuwaokoa wakimbizi.

Meli hii ilikusudiwa kuchukua wakimbizi 550 wa Kiafrika, kati ya 2,000 waliokwama katikati ya vita. Kwa mujibu wa madaktari, wakimbizi watatu wa Kiafrika wameuawa na 20 kujeruhiwa kutokana na mashambulizi haya.

Katika mji wa Kabao, ripoti zinasema kuwa mapigano makali ya Jumanne jioni yalimalizika kwa ushindi wa waasi, ambapo wanajeshi 45 wa serikali waliuawa na wengine 17 kukamatwa mateka. Waasi wamepoteza wapiganaji wawili na watatu kujeruhiwa.

Jumuiya ya Kimataifa mapande mawili

Viongozi wa Umoja wa Afrika wakiwa katika picha ya pamoja na Muammar Gaddafi kabla ya vita kuanza
Viongozi wa Umoja wa Afrika wakiwa katika picha ya pamoja na Muammar Gaddafi kabla ya vita kuanzaPicha: AP

Kimataifa, vita hivi vimeendelea kuigawa dunia mapande mawili. Umoja wa Afrika, kwa upande wake, umeyalaumu mataifa ya magharibi kwa kuzihujumu kwa makusudi jitihada zake za kutafuta amani nchini Libya.

Kamishna wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja huo, Ramtane Lamamra, amesema mataifa hayo yanauchukulia mpango wa amani wa Umoja wake kama usio na maana, huku yakiendelea na mashambulizi yake dhidi ya Libya, akikusudia zaidi mashambulizi ya .

Mapema baada ya mazungumzo yao na Lamamra hapo jana mjini Addis Ababa, pande mbili zinazozozana zilieleza maoni tafauti, ingawa pia zilielezea nia ya kuendelea na mazungumzo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya, Abdelati Obeidi, alitaka jitihada za Umoja wa Afrika zipewe fursa, huku wawakilishi wa waasi wakiahidi kuendelea na mazungumzo, alimradi tu 'matakwa ya watu ya Libya' yanatimizwa. Kwa waasi, matakwa hayo ya watu wa Libya ni Gaddafi kuondoka madarakani.

Katika taarifa yake iliyotolewa hivi leo, Umoja huo umezitaka pande zinazohusika na mapigano kutokuwalenga maafisa wa serikali au miundombinu, kwani mambo hayo yataifanya jitihada ya kutafuta maridhiano kimataifa kuwa ngumu zaidi.

Urusi yaja juu

Waziri Mkuu wa Urusi, Vladimir Putin
Waziri Mkuu wa Urusi, Vladimir PutinPicha: AP

Naye Waziri Mkuu wa Urusi, Vladimir Putin, akiwa ziarani nchini Denmark, ameyaita mashambulizi ya juzi ya NATO dhidi ya makaazi ya Gaddafi kama kitendo kisichokubalika, kwani ni njama ya kumuua kiongozi wa nchi.

"Dunia ina mataifa mengi yenye hali kama ya Libya. Je, tutakwenda kote huko kupiga mabomu. Kimazungumzo, wanatekeleza azimio la kuzuia ndege kuruka, ambalo ni sawa. Lakini azimio hilo liko wapi ikiwa kila usiku nyumba anayoishi Gaddafi inapigwa kwa mabomu? Nani ameyaruhusu haya?" Ameuliza Putin.

Lugha kama hii imetumiwa pia na rais wa Venezuela, Hugo Chavez, ambaye ameyaita mashambulizi haya ni "kuchanganyikiwa kwa mataifa ya magharibi", aliyoyashutumu kumchukia Gaddafi ili yapate mafuta. Ujumbe wa serikali ya Libya uko Venezuela katika jitihada za kutafuta uungwaji mkono wa kimataifa.

NATO yashikilia msimamo wake

Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen
Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh RasmussenPicha: dapd

Hata hivyo, mataifa wanachama wa NATO yanasema yataendelea na operesheni yao ya kuwalinda raia wa Libya, na kwamba yatafanya hivyo kwa kuviharibu vyanzo vyote vya mashambulizi ya Gaddafi.

Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, Liam Fox, ameiita operesheni hiyo ya NATO kuwa ya mafanikio. Akizungumza kwenye wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, hapo jana baada ya mazungumzo na waziri mwenzake wa ulinzi, Robert Gates, Fox alisema na hapa ninamnukuu:

"Tumeshuhudia maendeleo yakipatikana katika siku chache zilizopita. Na ni wazi kwamba utawala wa Gaddafi umeshikwa pabaya. Na madhali serikali inawashambulia raia, nasi tutaendelea kuvichukulia vituo vyao vya kuendeshea mashambulizi hayo kuwa shabaha halali za makombora yetu." Mwisho wa kumnukuu.

Ndani ya Libya, milio ya mizinga na risasi inaendelea kuwa sehemu ya maisha ya kawaida. Nje ya Libya vita vya maneno vimekuwa mtindo wa sasa. Na tafauti na ilivyokuwa kwa Tunisia na Misri, ngoma ya Libya inaonekana kuwa na mpigaji zaidi ya mmoja na wachezaji wasio idadi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Othman Miraji